Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moto, uvamizi watishia urithi wa dunia nchini

Meneja wa kituo cha michoro ya Mapango Kondoa, Zuberi Mabiye (kulia) akizungumza na Waandishi wa habari juu ya  hatari ya moto wa mstuni unaotishia kutoweka kwa urithi huo wa dunia. Picha na Samwel Mwanga

Muktasari:

  • Majanga ya moto na uvamizi wa watu katika maeneo ya hifadhi za Taifa, vimetajwa kuendelea kuwa tishio kwa maeneo ya urithi wa dunia na vituo vya urithi wa Taifa hapa nchini.

Serengeti. Majanga ya moto na uvamizi wa watu katika maeneo ya hifadhi za Taifa yameendelea kuwa tishio kwa maeneo ya urithi wa dunia na vituo vya urithi wa Taifa hapa nchini.

Wataalamu wanataka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuyalinda maeneo hayo dhidi ya uharibifu wa kudumu.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Stephano Msumi ameyasema hayo leo Jumapili, Mei 4, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia Afrika isemayo; “Majanga na migogoro ni tishio kwa urithi wa dunia.”

Amesema maeneo kama ya Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro na mapango ya Kondoa yanakabiliwa na changamoto za moto wa porini na uvamizi wa binadamu kwa ajili ya kilimo, uchomaji mkaa na makazi yasiyo rasmi.

“Moto na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ni tishio kubwa kwa urithi wetu wa dunia, ikiwa hatutachukua hatua sasa, tunaweza kupoteza maeneo haya,” amesema Msumi.

Amesema ni vizuri wataalamu wa mazingira kuweka mipango madhubuti ya usimamizi wa majanga, ikiwemo elimu kwa jamii, uwekaji wa mipaka ya hifadhi na vituo vyote vya urithi wa dunia, uboreshaji wa vifaa vya kuzima moto na ushirikishwaji wa wanavijiji katika ulinzi wa maeneo hayo muhimu.

Zuberi Mabiye ni Meneja wa kituo cha michoro ya mapango ya Kondoa Irangi, amesema baadhi ya maeneo hayo yako hatarini kupoteza michoro ya miambani inayodaiwa kuwa na zaidi ya miaka 2,000 kutokana na joto kali na hatari ya moto wa msituni.

“Urithi huu ni hazina ya Taifa, tunapaswa kuwekeza katika ulinzi wake kwa sasa ili vizazi vijavyo vinufaike,” amesema.

Naye Asha Hassan ambaye ni Mkurugenzi wa idara ya elimu tafiti na uwekezaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar, ambao ni sehemu ya Urithi wa Dunia, amesema kumekuwa na msongamano wa makazi ya watu waliovamia eneo hilo.

Asha amesema kuwepo kwa wafanyabiashara ndogondogo katika eneo la Mji Mkongwe ambao wamevamia, wanaweza kusababisha historia nzuri ya mji huo kutoweka.

“Katika mji Mkongwe wa Zanzibar, pale kuna msongamano wa makazi pamoja na wafanyabiashara katika eneo hilo la kihistoria. Hilo ni janga linaloweza kusababisha kutoweka kwa urithi wa dunia, hivyo kuna mipango inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutafuta eneo la kuwahamishia wafanyabiashara hao.”

“Urithi huu si wa kizazi kimoja, ni hazina ya Taifa na dunia. Tukichelewa kuchukua hatua, tunaweza kupoteza historia isiyoweza kurudi tena,” amesema.

Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika kesho Mei 5,2025 mjini Mugumu Wilaya ya Serengeti na mgeni rasmi anatarajia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Ntambi.