MNF kuadhimisha wiki ya kumbukizi ya kuzaliwa Hayati Mwalimu Nyerere

Muktasari:
Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) imeandaa maadhimisho ya wiki ya kumbukizi na uhuishaji maisha na falsafa za Hayati Mwalimu Julius Nyerere itakayoanza Aprili 13, 2023 tarehe ambayo alizaliwa miaka 101 iliyopita.
Musoma. Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) inatarajia kufanya midahalo kwa siku nne mfululizo ikiwa ni kuadhimisha wiki ya kumbukizi na uhuishaji maisha na falsafa za Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumanne Aprili 11, 2023, Mkurgenzi Mtendaji wa MNF, Profesa Francis Matambalya amesema maadhimisho hayo yanaanza Aprili 13 mwaka huu, tarehe ambayo alizaliwa Mwalimu Nyerere miaka 101 iliyopita.
Amesema miongoni mwa watoa mada kwenye midahalo hiyo ni viongozi kadhaa akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje nchini Uganda, Trasis Bazana watatoa mada lengo likiwa ni kuenzi mchango wake katika maendeleo ya Taifa, Afrika na Dunia kwa ujumla.
Pamoja na ushiriki wa viongozi hao, Profesa Matambalya amesema wanatarajia washiriki wengine zaidi ya 120 kuhudhuria midahalo hiyo ambao baadhi watatoka vijiji vya Wilaya ya Butiama.
“Tunataka kuhuisha falsafa ya Mwalimu Nyerere kwa watu wa makundi yote kutoka Tanzania, Afrika na maeneo mengine ya ulimwengu na programu hii ambayo baadaye itakuwa endelevu itashirikisha wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi,” amesema
Amesema licha ya mchango mkubwa aliotoa Mwalimu Nyerere katika ukombozi wa nchi na bara la Afrika lakini bado jitihada za kumuenzi hazijafanyika ipaswavyo na hivyo kuna kila sababu kwa wadau wote kuhakiksiha suala la kumuenzi linapewa kipaumbele.
“Kwasasa tuna tukio moja tu la siku ya kuzima mwenge ambalo pia lina mambo mengi ndani yake sisi tunadhani kumbukizi ya Nyerere inafaa kufanyika siku aliyozaliwa na liwe tukio maalum kwaajili ya Mwalimu na kwa kufanya hivyo tutawapa uelewa wa kutosha juu ya Mwalimu kizazi hiki na vijavyo ambavyo havikumshuhudia ili kuyaendeleza mazuri yake,” amesema
Profesa Matambalya amesema yapo mambo ambayo Baba wa Taifa, Mwalim Nyerere aliyapigania na yanafaa kuendelezwa kwa manufaa na ustawi wa jamii na nchi ikiwemo kukemea suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii.
“Uzalendo ni kitu ambacho mwalimu alikipigania lakini hivi sasa yapo mambo mengi yanayotokea ambayo yanaonyesha kabisa kuwa suala la uzalendo halipo tena kwa baadhi yetu mfano ukosefu wa uadilifu kwa viongozi na mambo mengine kama hayo kwahiyo suala la uelewa juu ya maisha ya mwalimu ni la muhimu sana kwa jamii,”amesema
Naye Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Francis Nyerere amesema mbali na midahalo hiyo, mashindano mbalimbali yakiwemo ya mpira wa miguu na pete yatafanyika katika wiki hiyo.
“Zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi wa michezo hiyo lengo ni kuhakikisha kuwa makundi mengi katika jamii yanapata ujumbe uliokusudiwa,” amesema