Mmoja afariki dunia, 19 wakijeruhiwa ajali ya lori, basi

Basi la Happy Nation likiwa limepata ajali baada ya kugonga lori eneo la Pangale Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 19 wakijeruhiwa. Picha na Johnson James
Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo Jumatano Julai 17, 2024 kata ya Pangale Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora na kusababisha kifo cha mtoto mmoja na majeruhi 19.
Tabora. Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Yumwema Charles (4), amefariki dunia na wengine 19 wamejeruhiwa baada ya kutokea ajali iliyohusisha basi la Happy Nation lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Katavi.
Basi hilo lililigonga lori la Kampuni ya Dangote lililokuwa limeegeshwa kando mwa barabara katika kizuizi cha Kata ya Pangawe wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkaoni Tabora, Costantine Mbogandi, akizungumzia ajali hiyo leo Jumatano Julai 17, 2024, amesema chanzo chake ni uzembe wa dereva wa basi la Happy Nation ambaye hakuwa akifuata sheria za usalama barabarani.
"Ni kweli alfajiri ya leo maeneo ya Pangale, Wilaya ya Sikonge, ilitokea ajali iliyohusisha magari mawili; basi lenye namba za usajili T.519 DXH aina ya Higher, mali ya Kampuni ya Happy Nation, likiendeshwa na dereva Wilson Sinai, maarufu ‘Nyoma’ na lori lenye namba za usajili T.295 EBS mali ya Kampuni ya Dangote lililokuwa limepakia simenti," amesema Kamanda Mbogandi.
Amesema katika ajali hiyo, mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Yumwema Charles (4) amefariki dunia na watu watatu wamepata majeraha makubwa.
Amewataja majeruhi ni pamoja na Michael Masanja (31), Maftaha Mapunda (38) na Nathan Makungi (48).
Amesema dereva wa basi hilo anashikiliwa na Polisi na dereva wa lori amekimbia kusikojulikana.
"Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi kwa kuwa ajali ilipotokea kulikuwa na kizuizi cha barabarani. Dereva wa basi alikuwa na mwendo mkali, gari lilimshinda, akalazimika kuligonga lori kwa nyuma. Tunatoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za barabarani, kuangalia sheria zinasema nini na eneo la kupunguza mwendo,” amesema kamanda huyo.

Lori la Kampuni ya Dangote likiwa limepinduka baada ya kugongwa na basi la Happy Nation katika kata ya Pangale Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora. Picha na Johnson James
Ametoa wito pia kwa wamiliki wa mabasi kuhakikisha madereva wa magari wanaosafiri usiku wapatiwe muda wa kutosha wa kupumzika mchana ili anapoanza safari awe na utimamu wa kutosha.
Mwananchi imezungumza na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Patrick Bilikundi ambaye amesema wamepokea majeruhi 20 lakini mmoja amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
"Saa 11 alfajiri leo Julai 17 tulipokea taarifa za uwepo wa ajali iliyohusisha basi la Happy Nation lililokuwa likitokea Dar kwenda Katavi kupitia Tabora, lililogongana na lori lililokuwa limebeba simenti. Tulipokea majeruhi 20 na kati ya hao mmoja alifariki dunia," amesema Dk Bilikundi. Amesema majeruhi wa ajali hiyo waliowapokea miongoni mwa wanawake wanane na wanaume 12 na kati ya hao watoto ni watatu,” amesema mganga huyo.
Amesema majeruhi 15 wamepata majeraha ya kawaida wametibiwa na kuruhusiwa na wanne wana hali mbaya.
“Mmoja tayari tumemuingiza kwenye chumba cha upasuaji kutokana na mivunjiko aliyoipata na wawili wamepewa rufaa kwenda Hospitali Kuu ya Kanda ya Bugando wakapate huduma za kibingwa,” amesema Dk Bilikundi.
Mashuhuda wasimulia
Wakisimulia namna ajali hiyo ilivyotokea, mashuhuda akiwamo Ayoub Lyanga mkazi wa Pangawe amesema alisikia kishindo kikubwa na baada ya muda mfupi, akasikia tangazo kutokea msikiti likiwaomba wananchi kwenda kutoa msaada kuna ajali ya basi imetokea.
“Tukatoka kuelekea eneo ilipotokea ajali tulipofika tukaanza kuwaokoa watu, majeruhi walikuwa wengi. Ajali ilivyotokea ni kwamba basi ndilo lililogonga lori lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara,” amesema Lyanga.
Naftali Bakumda, majeruhi aliyekuwa kwenye basi akitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Katavi, amesema walianza safari vizuri mpaka Tabora na wakati ajali inatokea alikuwa anachungulia nje ghafla akajihisi yupo ndotoni. "Tumeanza safari vizuri tu ghafla nikasikia kama tairi inatoa upepo, sio muda mrefu nikajikuta nagalagala chini kama niko ndotoni kumbe ndio ilikuwa hali halisi, mguu mmoja wa kushoto umevunjika na gari halikuwa na mwendo mkubwa. Kwa sasa ninaendelea vizuri kwa kuwa nimeshapewa huduma ya kwanza," amesema Bakumda.
Kondakta wa basi, Julius Pantaleo amesema wakati ajali inatokea alikuwa anakagua abiria wake ghafla akamsikia dereva akilalamika kwa nini lori la Dangote limeziba njia.
"Mimi nilikuwa naongea na abiria ambaye alikuwa na changamoto, kabla hatujamaliza mazungumzo dereva wetu alisema mbona lori la Dangote limeziba njia. Kwa kuwa alikuwa na mwendo kasi kidogo na alishalifikia na pembeni kulikuwa na uzio, basi akaamua kuligonga lori hilo lililokuwa limeegeshwa kwa kuwa hakuwa na sehemu nyingine ya kupeleka gari. Baada ya hapo nilipoteza fahamu, sikujua kilichoendelea," amesema Pantaleo.