Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mmiliki wa gari lililokamatwa na dhahabu adai hakujua gari yake iko Kahama

Muktasari:

  • Mmiliki wa gari lililokamatwa kwa kusafirisha dhahabu kupitia njia ya magendo amekiri kuwa hakujua gari lake lilikuwa Kahama, baada ya kuachwa na ndugu yake.

Geita. Mmiliki wa gari iliyokamatwa na polisi ikidaiwa kusafirisha dhahabu kupitia njia ya magendo, amekiri kuwa hakujua gari lake lilikuwa Kahama, mkoani Shinyanga.

Gari hiyo aina ya Toyota Premio, lilikamatwa na polisi Machi 24, 2025, likidaiwa kusafirisha dhahabu kupitia njia ya magendo.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro, wanawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha kwa njia ya magendo gramu 3263.72 za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh749 milioni.

Maro alisema watu hao walikamatwa saa tano usiku katika mtaa wa Kapera, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Yohana Idama (34), mkazi wa Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela, Mwanza; Moshi Manzili (26), mkazi wa Bariadi, mkoani Simiyu; na Hamidu Salum (25), mkazi wa Nyasubi, wilayani Kahama.

Hata hivyo, mmiliki wa gari hilo, akizungumza na gazeti hili leo, Machi 27, 2025 amekiri hakujua gari lake lilikuwa Kahama, kwani aliiacha jijini Dar es Salaam kwa ndugu yake.

Mmiliki huyo, Emanuel Kidenya, mkazi wa Kahama, amesema hakuwa na taarifa kama gari yake iko kwa watu tofauti na kwamba licha ya ndugu yake kutoa gari hiyo, hakumpa taarifa.

“Nilimwambia ndugu yangu nataka kuuza gari ninunue Harrier, sasa baada ya gari yangu kuonekana Kahama, nikamuuliza, akasema amepata wateja, lakini alikuwa hajaniambia,” amesema.

Amedai ndugu yake huyo, ambaye hakumtaja kwa jina, aliuza kwa watu hao bila kumshirikisha.

Kidenya alipoulizwa gharama za mauzo ya gari hilo na lini liliuzwa, amesema ndugu yake huyo hakumpa taarifa yoyote ya mauzo ya gari.


Chama cha Wachimbaji

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu Mkoa wa Geita (Gerema), Titus Kabuo, akizungumzia utoroshwaji wa madini, amesema ili kukomesha tabia hiyo, Serikali inapaswa kuongeza adhabu na kuweka kali zaidi kwa wale watakaokamatwa ili iwe fundisho kwa wengine.

Kwa mujibu wa sheria ya madini, wale wanaokutwa na hatia ya kutorosha madini hupewa adhabu ya mali kutaifishwa, kifungo, faini, au vyote kwa pamoja.

Amesema adhabu ndogo inayotolewa pindi wanapokamatwa wanaotorosha madini imechangia utoroshaji kuendelea.

"Mara nyingi wakikamatwa mali waliyobeba inataifishwa, lakini adhabu hii ni ndogo. Aliyetorosha inawezekana mzigo sio wake, kuna tajiri nyuma yake, lakini akipewa adhabu, mtu aliyekamatwa hii itawafanya wawe na hofu na itasaidia kumaliza utoroshwaji," amesema Kabuo.

Aidha, ameiomba Serikali kuwachunguza wanaokamatwa wakisafirisha madini kwa njia za magendo ili kujua mtandao mzima unaohusika na biashara hiyo haramu.

"Hakuna anayetorosha bila kujua anakopeleka. Masoko ya madini yapo na mtu yeyote anaruhusiwa kuja kuuza. Ukiona hawa wanaotorosha, ujue wanamtandao nje ya nchi, na ndio maana naishauri Serikali wakikamata mtu wahakikishe wanachunguza kupata mtandao mzima wa utoroshaji,” amesema Kabuo.

Akizungumzia waliokamatwa na polisi, Kabuo amesema hajui kama ni wachimbaji wa Geita au nje ya mkoa huo kwa kuwa hawana taarifa  kamili ya wachimbaji na kwamba sasa wapo kwenye mchakato wa kuorodhesha majina ili kupata idadi kamili ya wachimbaji waliopo kwenye mkoa huo.