Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkongo wa baharini wa 2Afrika waanza kutumika Tanzania

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imeanza kutumia rasmi mkongo wa mawasiliano unaopita baharini wa 2Africa wenye urefu wa kilomita 45,000 ukiunganisha mabara matatu, ili kutoa huduma za intaneti ya kasi zaidi.

Jambo hilo linaelezwa kuwa litaleta maendeleo makubwa katika kupanua na kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini Tanzania.

Mkongo huo wa kisasa wa 2Africa unaopita chini ya Bahari na kusimamiwa na Airtel Tanzania, unatarajiwa kuiweka Tanzania katika viwango vya juu vya mabadiliko ya kukua kwa huduma za kidijitali na kukidhi mahitaji ya uchumi wa nchi unaoendeshwa na huduma za mtandao (data).

Mkongo huo ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kituo cha mkongo wa mawasiliano baharini - Airtel Cable Landing Station kilichopo maeneo ya Mbezy Meach, jijini Dar es Salaam.

"Kuzindua Kituo cha 2Africa Cable landing Station kunaashiria hatua muhimu na mustakabali wa nchi yetu kupaa kidijitali. Miundombinu hii si tu italeta mapinduzi katika huduma za mawasiliano, pia itaharakisha ukuaji wa uchumi kwa kuimarisha muungano na mataifa mengine,” alisema Rais Samia wakati wa uzinduzi huo.

Mkongo wa 2Africa sasa umeanza kuhudumia kampuni za teknolojia ambazo zinapokea masafa ya uwezo wanaohitaji kupitia kituo cha Airtel Cable Landing Station   kilichopo Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Mkongo mpya wa Airtel 2Africa unatarajia kuwa suluhisho na ulinzi wa mikongo au kebo nyingine za mawasiliano zinazopita chini ya bahari nchini.

Uzinduzi huu wa Airtel Tanzania umekuja kutokana na kukatika kwa nyaya za mkongo wa mawasiliano unaopita chini ya bahari hivi karibuni ambazo ziliathiri baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki, ikiwemo  Tanzania.

Inaelezwa kuwa mkongo wa mawasiliano wa 2Africa una uwezo wa kusafirisha masafa mara 10 zaidi ya ile iliyopo na inalenga kusaidia kuanzishwa kwa vituo vya kuhifadhi kumbukumbu kielektroniki (Data centres),  ili kukidhi ongezeko la shughuli za kidijitali nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, amesema mazingira wezeshi ya Serikali katika kupatikana kwa leseni pamoja na uwepo wa mfumo bora wa udhibiti ndio sababu zilizowezesha Airtel Tanzania kuzindua kituo chao cha Airtel 2Africa kabla ya nchi nyingine.

Ameeleza kuwa Tanzania inashuhudia kuwashwa kwa mkongo wa 2Africa na kuanza kugawa masafa yenye uwezo wa juu moja kwa moja sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari amesema mkongo huo mpya wa mawasiliano unaopita baharini, utachochea na kuboresha zaidi huduma bora za intaneti nchini.

“Mkongo huu mpya utakuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na mahitaji ya huduma za mtandao wa intaneti nchini, ambapo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka maradufu kila baada ya miaka miwili,” amesema Dk Jabir.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema uwepo wa mkongo huo utasaidia kuunganisha nchi kimataifa na kuwepo kwa mifumo ya kibunifu kidijitali, ikiwemo kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali kuwa jumuishi.

“Mkongo wa 2Africa utaleta maendeleo kwa huduma za mawasiliano katika nchi yetu na kuwa kivutio na suluhisho la mawasiliano kidijitali kwa nchi za Afrika Mashariki," amesema Nape.