Mkenda aweka mkazo elimu ya amali kuongeza ajira

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (aliyesimama) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa karakana ya ufundi ya Laban katika chuo kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ili kukidhi vigezo katika ushindani wa soko la ajira kwa wanafunzi wanaohitimu, elimu ya ujuzi wa utendaji (amali) inapaswa kupewa kipaumbele nchini.
Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema Tanzania haina budi kuweka nguvu katika elimu ya amali ambayo ni chanzo kikubwa cha ajira si Tanzania tu bali kote ulimwenguni.
Akiongea katika uzinduzi wa Karakana ya ufundi ya Luban leo jijini hapa katika chuo kikuu cha Ardhi, Mkenda amesema ajira nyingi ziko kwenye elimu hiyo inayohusisha ujuzi wa utendaji.
"Ajira nyingi kwa sasa zipo kwenye mafunzo ya amali ambayo ni mafunzo ya kazi yanayohusisha ujuzi wa utendaji," amesema.
Mkenda amesema ushirikiano kati taasisi tatu zilihusika katika ujenzi wa karakana hiyo hiyo ni hatua muhimu ya mashirikiano kati ya Tanzania na China.
"Napenda tuimarishe ushirikiano kati yetu na China katika elimu ya mafunzo ya amali," amesema Mkenda.
Pia amesema Tanzania imeingia makubaliano kati chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) na chuo cha China ambacho kinatoa mafunzo ya amali ya uhandisi ambapo wamepeleka wanafunzi 30.
"Hawa wanafunzi wataingia DIT, watasoma mwaka mmoja, wataenda China kusoma diploma kwa miaka miwili halafu watarudi hapa na kusoma tena mwaka mmoja huku wakiwa wanafanya kazi na baada ya hapo watatunukiwa Shahada," amesema.
Aidha amesema amemuomba balozi ya China kuongeza idadi ya wanafunzi hao wanaotarajiwa kwenda kusoma China kutoka 30 hadi 300.
"Tungependa tuwe na program za shahada za amali ambazo zinachanganya kusoma hapa na nje ya nchi kwa sababu lazima tukiri kwamba tuna mapungufu na tukubali kujifunza kwa wenzetu," amesema.
Pia amesema Serikali inapenda kuona vyuo mbambali vinatoa kipaumbele katika mafunzo hayo.
"Tuchofanya ni kuhakikisha vijana wetu wanaosoma wanapata fursa ya kwenda nje na hivi karibuni tutatambulisha ufadhili wa masomo nje ya nchi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi," ameongeza.
Kwa upande wake balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian amesema kwa miongo mingi sasa uhusiano kati ya Tanzania na China umekua wa manufaa makubwa kwa nchi hizo katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu.
Amesema uhusiano wa mataifa hayo umejikita katika kuwajenga uwezo na kuinua vipaji ili kuwa na rasilimali watu wa kutosha.
"Luban ni alama ya ushirikiano kati ya mataifa yetu. Ni chapa maarufu ya China katika kupalilia na kuinua vipaji katika uhandisi, teknolojia na kuendeleza ujuzi kwa vijana wanaosoma," amesema Mingjian.
Pia amesema mataifa hayo yana uhusiano mwingine katika elimu ikiwemo wanafunzi wa Tanzania kwenda kusoma China akisema takriban wanafunzi 6000 wa Tanzania wanasoma nchini China na kuifanya China kuwa nchi yenye idadi kubwa ya wanafunzi kutoka Tanzania.
Naye makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa, amesema wamezindua Karakana hiyo kwa lengo kuongeza ujuzi wa wanafunzi jambo ambalo ni kipaumbele cha Serikali.
"Tunataka kuondokana na utegemezi wa mafundi kutoka nje. Mfano tuna miradi mbalimbali nchini lakini hatuna wataalamu wa kutosha wazawa," amesema Liwa.
Mnamo Julai 2022, Taasisi ya Ufundi ya Chongqing ya Uhandisi na Group Six International Ltd ziliweka saini ili kujenga Msingi wa Mafunzo yatakayo tolewa na taasisi ya Luban ili kutoa mafunzo kwa zaidi ya vipaji 100,000 vya uhandisi kwa raia wa hapa nchini.
Mnamo 2023 taasisi hizo na Chuo Kikuu cha Ardhi kwa pamoja walitia saini makubaliano mapya ya ushirikiano ili kuanzisha Taasisi ya ufundi wa uhandisi ya Luban nchini Tanzania.