Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miundombinu ya barabara yaibua hofu Hospitali ya Rufaa Mara

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wakitembea kwa miguu kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara maarufu kama Kwangwa kutokana na kukosekana kwa usafiri wa umma wa kwenda na kurudi hospitali hiyo. Picha na Beldina Nyakeke.

Muktasari:

Kutokana na kutokuwepo usafiri wa umma kwenda na kurudi hospitali hiyo, wananchi hulazimika kutumia gharama kati ya Sh3, 000 hadi Sh4, 000 kukodisha pikipiki.

Musoma. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inaanza kutoa huduma kuanzia Julai Mosi, 2023, huku ubovu wa miundombinu ya barabara ikiibua hofu miongoni mwa wananchi.

Ubovu wa miundombinu ya barabara ya kwenda na kurudi kutoka hospitali hiyo maarufu kama Hospitali ya Kwangwa imesababisha kukosekana kwa usafiri wa umma, hali inayowalazimisha wananchi kutegemea pikipiki za miguu miwili au zile za miguu mitatu maarufu kama bajaji.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma iliko hospitali hiyo waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti Juni 30, 2023 wameiomba Serikali kutenga bajeti ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa ulio nje kidogo ya Manispaa ya Musoma umekamilika baada ya takriban miaka 45 tangu ulipoanza kutekelezwa mwaka 1975 baada ya Serikali kutumia zaidi ya Sh39 bilioni.

Magige James, mkazi wa mtaa wa Mkendo Manispaa ya Musoma ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara ya inayoenda na kutoka hospitali hiyo ili isiwe kikwazo cha wananchi kupata huduma.

“Hii moja ya hospitali yenye hadhi kubwa Kanda ya Ziwa, miundombinu ya barabara zake lazima iakisi umuhimu na hadhi hiyo,’’ amesema Magige

Hoja hiyo imeungwa mkono na Nyamagwana Kulwa, mkazi mwingine wa Manispaa ya Musoma akisema ubovu wa barabara ya kwenda na kurudi hospitali hiyo inawalazimisha wananchi wengi kutumia usafiri wa pikipiki kutokana na magari mengi, yakiwemo ya kukodi kukataa safari za kwenda huko.

Kutokana na kutokuwepo usafiri wa umma kwenda na kurudi hospitali hiyo, wananchi hulazimika kutumia gharama kati ya Sh3, 000 hadi Sh4, 000 kukodisha pikipiki.

“Hii ni gharama kubwa kwa wananchi wenye kipato cha kawaida, hasa wenye wagonjwa waliolazwa wanaolazimika kufanya angalau safari mbili hadi tatu kuwapelekea huduma ya chakula ndugu zao waliolazwa,’’ amesema Nyamagwana

Amesema miundombinu ya barabara ikiboreshwa utawavutia wamiliki wa daladala kuanzisha safari za Hospitali ya Kwangwa, tofauti na hali ilivyo sasa.

‘’Serikali ijenge barabara hii, ikiwezekana kwa kiwango cha lami kuvutia wamiliki wa daladala kuanzisha safari za kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa,” amesema mkazi mwingine wa Manispaa ya Musoma, Nurdin Ibrahim

Huku akipongeza uamuzi wa Serikali wa kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo baada ya kukwama tangu mradi huo ulipoanza kutekelezwa mwaka 1975, Masanja Fabian amesema uamuzi huo unapaswa kwenda sambamba na maboresho ya miundombinu ikiwemo barabara zinazoenda na kutoka hospitali hiyo ambayo ni kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius kambarage Nyerere.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Musoma, Joseph Mkwizu amesema Serikali imepanga kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu ya barabara za kutoka na kwenda Hospitali ya Kwangwa.

‘’Serikali imepanga kuboresha miundombinu ya barabara zote kutoka maeneo tofauti ya Manispaa ya Musoma kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara,” amesema Mkwizu

Amesema mikakati ni kuhakikisha barabara hizo zenye urefu wa kilometa sita zinajengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2023/24.

Kwa kuanzia, meneja huyo amesema Tanroads itafanya matengenezo ya haraka kwa kuchonga na kushindilia udongo huku mchakato wa zabuni za kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami ikikamilishwa.