Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mila, umaskini vyatajwa kikwazo kwenye malezi

Muktasari:

  • Changamoto za malezi kwa jamii zinahitaji mshikamano kati ya serikali, jamii, na wadau wa maendeleo ili kufanikisha malezi bora.

Arusha. Pamoja na jitihada kubwa za Serikali na wadau mbalimbali kuimarisha malezi ya awali ya mtoto, jamii ya Watanzania bado inakumbwa na changamoto kadhaa zinazohitaji uingiliaji wa haraka na wa pamoja ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira bora ya kimalezi.

Ripoti kutoka Mkoa wa Arusha inaonyesha kuwa, licha ya mafanikio ya mpango wa Mzazi Hodari, bado kuna maeneo ambayo mila na desturi zimeendelea kuwa kikwazo kwa baadhi ya wazazi, hususan wanaume, kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao.

“Watu wengine walikuwa wakicheka wanapoona baba anambeba mtoto au anahudhuria kliniki na mkewe, lakini sasa hali imeanza kubadilika,” amesema Denis Mguye, Ofisa Ustawi wa Jamii wa mkoa huo.

Hata hivyo, mabadiliko hayo bado hayajaenea kwa kasi inayohitajika na familia nyingi, hasa vijijini, bado zinakabiliwa na upungufu wa elimu kuhusu umuhimu wa malezi jumuishi, hali inayosababisha watoto kukua katika mazingira yasiyo rafiki kwa maendeleo yao ya kimwili, kiakili na kihisia.

Pia, ukosefu wa miundombinu rafiki kwa malezi, kama vituo vya kulelea watoto wachanga (daycare), na huduma rafiki za afya ya uzazi kwa wazazi wapya, ni changamoto inayoathiri uwezo wa familia nyingi kutoa malezi bora.

 “Wazazi wengi hawana taarifa sahihi, wala nafasi ya kupata msaada wa kitaalamu wanapokumbwa na changamoto za kimalezi,” amesema Violet Chahe, Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Wilaya ya Arusha.

Changamoto nyingine inajitokeza katika mfumo wa elimu na utekelezaji wa sera, ingawa Mwongozo wa Uendeshaji na Uwasilishaji wa Mipango ya Ustawi wa Jamii (CCSWOPG) umewekwa tangu 2022, utekelezaji wake umekuwa hafifu katika baadhi ya halmashauri, ambapo mipango ya malezi ya awali bado haijapewa kipaumbele cha bajeti.

Katika baadhi ya jamii, umaskini pia umeendelea kuwa kikwazo kikubwa ambapo wazazi hulazimika kutumia muda mwingi kutafuta riziki na kukosa muda wa kushughulikia mahitaji ya kihisia na maendeleo ya watoto wao. Hali hii imechangia kuongezeka kwa matatizo ya tabia, msongo wa mawazo kwa watoto, na hata ukatili wa majumbani.

Hata hivyo, kuna matumaini kupitia programu kama Mzazi Hodari, jamii imeanza kuamka. Majukwaa ya redio, makundi ya WhatsApp, na hata michezo ya soka sasa vinatumika kama majukwaa ya elimu ya malezi.

“Wazazi wameshika hatamu, wakishirikiana kama jamii, kuleta mabadiliko ya kweli,” anasema Mguye.

Changamoto zilizopo zinahitaji mshikamano kati ya serikali, jamii, na wadau wa maendeleo ambapo kufanikisha malezi bora si suala la mtu mmoja ni jukumu la wote.