Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tabia hatari za kifedha zinazokufanya uendelee kuwa masikini

Watu wengi hujiuliza kwa nini hawawezi kupiga hatua kifedha hata kama kipato chao kinaonekana kutosha. Mara nyingi, tatizo si ukosefu wa kipato, bali ni kuwepo kwa tabia za kifedha hatarishi ambazo hujificha na kuharibu hali ya kifedha polepole.

Dalili hizi za hatari huweza kuharibu utajiri taratibu na kumwacha mtu katika mzunguko wa madeni, msongo wa mawazo, na hali ya kukata tamaa. Kuelewa na kushughulikia tabia hizi ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea maisha ya kifedha yaliyo imara na yenye mafanikio.

Moja ya mitego mikubwa ni kuishi zaidi ya uwezo wako. Hii hutokea unapokuwa unatumia zaidi ya kile unachokipata, mara nyingi ukichochewa na shinikizo la kijamii au tamaa ya kuboresha maisha kila unapopata nyongeza ya kipato.

Suluhisho ni kutengeneza bajeti halisi ya kila mwezi na kujitahidi kuifuata. Toa kipaumbele kwa mahitaji muhimu kama chakula, makazi, usafiri, na huduma za umeme kabla ya kutumia kwenye anasa. Kuishi chini ya kipato chako ni msingi wa uhuru wa kifedha.

Dalili nyingine ya hatari ni kukosa mfuko wa dharura. Watu wengi hutegemea mikopo au kadi za mkopo pindi gharama zisizotarajiwa zinapojitokeza. Kujenga mfuko wa dharura, hata kwa kuweka Sh5,000 tu kwa wiki, kunaweza kutoa kinga dhidi ya kukopa kila mara matatizo yanapotokea. Lengo la muda mrefu ni kuwa na akiba inayoweza kugharimia angalau miezi mitatu ya mahitaji muhimu.

Matumizi ya ghafla au ya kihisia pia ni tabia inayosababisha upotevu wa pesa bila kujitambua. Iwe ni kwa sababu ya ofa au kuchoka tu, ununuzi usiopangwa hujilimbikiza. Njia bora ya kukabiliana na hili ni kutumia kanuni ya “subiri saa 24” kabla ya kufanya ununuzi wowote usio wa lazima. Mara nyingi, hamu ya kununua hupotea na fedha huokolewa.

Kuepuka deni hakumaanishi kupuuza madeni. Wengine hulipa kiwango cha chini kabisa au hujitia hamnazo kuhusu madeni yao. Hii husababisha salio la deni kukua na riba kuongezeka. Ni vyema kuorodhesha madeni yako yote na kuanza kuyalipa kwa kutumia mbinu ya “snowball” (anza na deni dogo zaidi) au “avalanche” (anza na deni lenye riba kubwa zaidi). Njia yoyote utakayochagua, jambo muhimu ni kuwa na mkakati na kuendelea kuwa thabiti.

Kutokuwa na malengo ya kifedha ni kikwazo kingine kikubwa cha mafanikio. Bila mwelekeo maalumu, fedha hutumika ovyo kwa starehe za muda mfupi.

Weka malengo ya kifedha yaliyo wazi na yenye muda maalumu—iwe ni kununua nyumba, kuanzisha uwekezaji, au kustaafu mapema. Malengo haya huwa dira ya kila uamuzi wa kifedha unaofanya kila siku.

Kutoandika au kufuatilia matumizi ni adui kimya wa utajiri. Kama hujui pesa yako inaenda wapi, huwezi kufanya uamuzi sahihi. Tumia daftari, jedwali la Excel au programu ya bajeti kufuatilia mapato na matumizi yako. Fuatilia mara kwa mara ili kubaini mianya ya matumizi yasiyo na ulazima. Uwazi wa kifedha huleta amani na udhibiti.

Kutegemea chanzo kimoja cha kipato ni hatari kubwa zaidi katika dunia ya leo isiyotabirika. Kupoteza kazi au kipato cha ghafla kinaweza kusababisha mshtuko mkubwa wa kifedha. Kuongeza vyanzo vya kipato chako kupitia biashara ndogo, kazi za muda, au kipato pasipo kuhusisha nguvu nyingi kama kodi ya nyumba au gawio la hisa huongeza utulivu wa kifedha na nafasi ya mafanikio.

Tabia nyingine hatari ni kuhifadhi fedha tu bila kuwekeza. Ingawa kuweka pesa benki ni salama, hakui utajiri wako. Anza kujifunza kuhusu uwekezaji wa msingi kama hati fungani, mifuko ya pamoja (mutual funds), au hisa zinazouzwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Uwekezaji wa aina hii, ukifanywa kwa maarifa, ni njia nzuri ya kukuza utajiri kwa muda mrefu.

Kuchelewesha uamuzi wa kifedha ni kikwazo kingine kikubwa. Kila mara kusema “nitaanza kuokoa mwezi ujao” husababisha kupoteza muda na fursa. Hata kama ni kiasi kidogo, kuanza sasa ni bora kuliko kusubiri wakati mzuri. Weka mpango wa kuokoa kiotomatiki ili iwe tabia ya kawaida na sio chaguo la kila mwezi.

Hatimaye, kupuuza elimu ya kifedha ni moja ya dalili kubwa zaidi za hatari. Watu wengi hufuata ushauri wa bahati nasibu au hukisia kwa sababu hawajachukua muda kujifunza. Elimu ya kifedha si hiyari—ni hitaji.

Jenga tabia ya kusoma vitabu, makala, au kusikiliza vipindi vya kifedha kutoka kwa wataalamu. Hudhuria semina au warsha. Maarifa hutoa uwezo wa kufanya uamuzi bora na huzidisha thamani ya utajiri wako.

Kujenga utajiri si suala la kupata pesa nyingi pekee, bali ni kuendesha pesa zako kwa ufanisi. Kwa kutambua na kurekebisha dalili hizi za kifedha hatari, mtu yeyote anaweza kutoka kwenye hali ya uhaba na kufikia utulivu wa kifedha—na hatimaye mafanikio.

Anza kwa kubadilisha tabia moja leo. Mabadiliko madogo ya mara kwa mara hujenga mafanikio makubwa. Na “wewe wa baadaye” atakushukuru kwa uamuzi unayofanya leo.