Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mila feki za wahenga zilivyojenga jamii, kulinda maadili

Muktasari:

  • Hivi umeshawahi kusikia makatazo kama vile kutokata kucha usiku, watoto kukatazwa kula aina fulani ya vyakula, kutosimama mlangoni wakati wa mchana? 

Wazee wa zamani walijaaliwa hekima za hali ya juu, licha ya kwamba maagizo yao ya kimila hivi leo yanaonekana kukosa nafasi kwa jamii.

Zamani jamii mbalimbali ziliishi kwenye mafundisho na makatazo mbalimbali yaliyolenga kujenga umoja wa jamii, kulinda maadili, kutunza usafi na kulinda mazingira. Hii ni mifano tu ya maeneo mengi ya ujenzi wa jamii ambapo wazee walifikia hatua ya kutunga mila za uongo ili kufanikisha dhamira yao.

Hivi umeshawahi kusikia makatazo kama vile kutokata kucha usiku, watoto kukatazwa kula aina fulani ya vyakula, kutosimama mlangoni wakati wa mchana? 

Hii ni mifano ya makatazo au mila nyingi za zamani ambazo zilitumiwa na wazee kwa sababu fulanifulani, hata kama hazikuwa na mantiki yoyote ndani yake zaidi ya kuwa ni sehemu ya vitisho dhidi ya tabia zisizokubalika.

Makala haya kwa kurejea baadhi ya makabila ya kanda ya ziwa, inaangazia baadhi ya mila hizo na namna zilivyotumika kujenga jamii.


Titi la mama kukatika

Miongoni mwa miiko waliyofundishwa watoto ni pamoja na kutojisaidia haja kubwa pembeni mwa njia na kuchunguliana wakati wa kujisaidia,  wakiaminishwa kwamba anayekaidi katazo hilo basi ziwa au titi la mama yake litakatika na yeye mwenyewe kuandamwa na moshi awapo jikoni au eneo la kuota moto nyakati za usiku.

“Tulivyokuwa wadogo tulionywa hatari ya kuchunguliana wakati wa kujisaidia tukiaminishwa kwamba yeyote anayemchungulia mwenzake akijisaidia ziwa la mama yake litakatika. Tulizingatia sana maonyo hayo ili maziwa ya mama zetu yasikatike," anasema John Okech, mkazi wa Jiji la Mwanza anayetoka jamii ya Waluo, moja ya jamii inayopatikana Mkoa wa Mara.

Akifafanua, Okech anasema; "Tulipokuwa wakubwa, tuligundua yale madai ya maziwa ya mama kukatika yalilenga kuhakikisha watoto hawajisaidii haja kubwa pembeni mwa njia siyo tu kulinda afya, bali pia usafi wa mazingira na kuwaepusha wapita njia na kero ya kukanyaga au kuona kinyesi cha binadamu,"


Binti aliyeolewa kutorejea kwao

Sarah Opiyo anasema jamii ya Waluo walikataza binti aliyeolewa na watoto wake kutorejea nyumbani kwao alikozaliwa nyakati za kilimo, palizi na mavuno kwa madai kuwa wanaweza kutumika kwa ajili  matambiko ya kimila ya kilimo, palizi au mavuno.

Lakini haikuwa kweli, lengo lilikuwa kuhakikisha binti aliyeolewa pamoja na watoto wake wanakaa nyumbani kwao (kwa mumewe) nyakati za kilimo, palizi na mavuno ili washiriki kazi hizo muhimu za uzalishaji kuwezesha familia kuwa na uhakika wa chakula.


Binti kukosa mchumba

“Zamani sisi kukiwa na harusi mtoto ukaondoka nyumbani kwenda kukesha ilikuwa ni marufuku…kwanza kabla haujaenda unakuwa unajua kabisa ni mwiko, kwa binti wa kike tuliaminisha kukosa wachumba lakini kwa wanaume waliaminishwa kupata mikosi,

“Lakini ikitokea umeenda licha ya makatazo hayo ukirudi ni kipigo sana..Na walikuwa wanazuia ili mtoto asiharibike maana yake usiku kule atakutana na mambo mengi hususani mtoto wa kike wanaweza kumbaka au wanaweza kumuingiza kwenye makundi mabaya,”anasema Zainabu Swed (66), mkazi wa Kaliua mkoani Tabora.

 Anasema kitisho cha wasichana kukosa wachumba kilitumika hata kuwakataza kurudi nyumbani usiku, hawakutakiwa kurudi nyumbani baada ya jua kuzama hata kama walienda kutembelea ndugu na taarifa za kwenda huko baba na mama zao wanazijua.

Anasema katazo hilo siyo tu ziliwajengea maadili ya kuacha kutembea hadi usiku lakini pia ziliwafanya kuwa salama dhidi ya madhila yanayoweza kutokea njiani usiku ikiwemo kukabwa, kuliwa na wanyama wakali au kuumwa na wadudu na wakati mwingine hata kubakwa.


Watoto kutokula viazi viazi vikubwa

Kulwa Samsoni, mkazi wa Mabuki wilayani Misungwi anasema wakati anakua kulikuwa na mwiko wa watoto kutotakiwa kula kiazi (kiazi kitamu) kikubwa kwa madai ya kuwa akifanya hivyo wakati wa kutembea ataangukia kwenye uzio wa nyumba ya mtu (kipindi hicho nyumba zilikuwa na uzio wa  za miti, maua au minyaa).

Anasema baadaye alivyokua mkubwa, alibaini kuwa siyo kweli bali alikuwa anafundishwa maadili ya kula kulingana na uwezo wa tumbo lake lakini bila kuchagua kwenye sahani.

“Nani aliyetaka kuanguka? hakuna hata mmoja hivyo tulikuwa tunakula viazi vidogo hadi tunashiba, hakuna mtu aliyekuwa anawahi kiazi kikubwa kama ikitokea kwenye sahani kipo basi tunamuachia mkubwa,”anasimulia.

Anasema ili wazee wathibitishe mtoto wao ana maadili mgeni akija anaambiwa akale naye, pale atakula kistaarabu hakuna kuongea wala kula haraka haraka kana kwamba anashindana.

“Lakini watoto wa siku hizi ikitengwa sahani mara aongee mara awahi nyama aseme hii yangu yaani hakuna kabisa maadili ya kula. Sisi zamani mtoto, kijana au binti alikuwa hawezi kunawa mikono muda wa kula au baada ya kula kabla wakubwa wake hawajanawa maana tuliaminishwa ni dhambi…hivyo tulisubiri wakubwa wanawe ndio na sisi tunawe. Lakini niambie wewe hali sasa ikoje? anaeleza.


Wanawake kutokula mayai, nyama

Miongoni mwa miiko au mila iliyotajwa kuwa ya kibaguzi, potofu na iliyonyima haki wanawake ni ile ya wajawazito kuzuiliwa kula vyakula vyenye protini nyingi yakiwemo mayai na hata kunywa maziwa  wakiaminishwa sio salama kwa mtoto na huenda mtoto akazaliwa akiwa hana nywele kichwani.

Hata hivyo, Michael Masanja anasema mila hiyo ilikuwa sahihi kwa wakati huo kwakuwa iliwekwa kuepusha uwezekano wa mjamzito kupata shida wakati wa kujifungua kutokana na mtoto kuwa mkubwa na hakukuwa na huduma bora za afya na upasuaji  kama ilivyo leo hii.

 “Hata kliniki za hospitalini wanazohudhuria wajawazito  hawakuwa nazo.. lakini waliwekaa miiko ambayo mama mjamzito alitakiwa asiifanye kwa usalama wake. Mfano mjamzito alikatazwa kukunja miguu akiaminishwa wakati wa kujifungua ukifika mtoto atatoka akiwa amekunja miguu au kushika tama, lakini haikuwa kweli, lengo lao lilikuwa wasiwabane watoto tumboni maana ukikunja miguu unabana tumbo,”anasema