Mikononi mwa polisi akituhumiwa kumuua mama yake mzazi

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia Patrick Mmasi (24) mkazi wa Njiro Kontena kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi, Ruth Mmasi (40) ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini.
Limeeleza kuwa baada ya kufanya mauaji aliutumbukiza mwili katika shimo la choo.
Tukio hilo limebainika juzi baada ya raia wema kutoa taarifa za siri polisi ambao walikwenda na kubaini mwili huo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema taarifa rasmi zitatolewa lakini polisi wanamshikilia Patrick kwa tuhuma za mauaji.
"Tunamshikilia kijana huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani," amesema.
Taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake kutajwa, amesema tukio limetokea juzi Desemba 24,2021.
Kwa mujibu wa ndugu huyo, mtoto mwingine wa marehemu Patricia Mmasi (19) anayesoma nchini China alipata mashaka akiwa China wakati alipojaribu kumpigia simu mama yake lakini haikupokelewa.
Amesema aliamua kuja Tanzania kwa ajili ya sherehe za Krisimasi na alimuuliza Patrick kuhusu kutoonekaa kwa mama yake na kutopatikana kwenye simu ambapo ndugu yake huyo alimjibu kuwa mama yake akitoka huwa hamuagi na ndipo walipoamua kutoa taarifa polisi.
Amesema polisi walipofika walifanya upekuzi sehemu mbalimbali za nyumba hiyo ya kisasa ya ghorofa moja na ndipo wakabaini mwili huo ukiwa ndani ya chemba la choo nyuma ya nyumba hiyo na mwili huo umegundulika baada ya siku 14.
Ndugu huyo amedai marehemu alikuwa akiishi na kijana wake huyo ambaye ndiye Mmoto wake wa kwanza na mara nyingi walikuwa wakitofautiana .
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamedai mwili huo ulikuwa umeanza kuharibika na umehifadhiwa katika hospital ya Mkoa ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa ndugu marehemu, mwili wa Ruth utazikwa nyumbani kwao kesho alasiri katika eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.