Prime
Mikakati ya bosi mpya wa Tanroads hii hapa

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Mohamed Besta akifanya mahojiano na waandishi wa gazeti hili
Dar es Salaam. Ni miezi mitatu imepita tangu Rais Samia Suluhu Hassan amteue Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Mohamed Besta, Julai 13 mwaka huu.
Mhandisi Besta kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Tanroads alikuwa Mkurugenzi wa ufundi wa Wakala wa Usimamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (CASSOA).
Mtendaji mkuu huyo hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na Mwananchi na kuelezea, hali ya mtandao wa barabara nchini, miradi inayotekeleza, udhibiti wa rushwa kweneye mizani pamoja gharama za matengenezo ya barabara kila mwaka.
Swali: Mtandao wa barabara za Tanroads sasa ni mrefu kiasi gani? Katika mtandao huo, ni barabara zenye urefu gani zimewekwa lami na ngapi bado?
Jibu: Mtandao wa barabara unaosimamiwa na Tanroads una jumla ya kilomita 36,760 kati ya hizo 12,223 ni barabara kuu na kati ya hizo 24,000 km ni barabara za mikoa.
Kati ya hizo kilomita 12,223, kilomita 11,918 zimeweka lami tumebakiza kilomita chache sana, kati ya 28,841 za barabara za mikoa ni kiasi kidogo tumeweka lami ambapo tuna kazi kubwa ya kuhakikisha barabara zote zinafikiwa na lami.
Swali: Miradi gani mikubwa ya Tanroads ambayo inaendelea hivi sasa?
Jibu: Hivi sasa tuna miradi mingi na zimeendelea kukua mwaka hadi mwaka,
Mwaka wa fedha tumesaini miradi 25 mipya, lakini miradi ninayoweza kusema ni miradi ya kimkakati ambayo inahitaji kusimamiwa kwa karibu sana ni miradi tuliosaini Juni 2023 ambayo itasimamiwa kwa aina mpya ya usimamiaji wa miradi EPC+F
Hiyo miradi ipo saba na inatandaa nchi nzima na ipo Km 2,035 itatandaa nchi nzima.
Miradi hiyo ni kilomita 435 kutoka Kidatu Ifakara Rupilo, Malinyi Kilosa Mpepo Londo Lumecha, mradi wa pili Barabara ya Arusha –Kibaya- Kongwa 453
Barabara ya Handeni- Kiberashi-Kijingu-Kibaya- Njoro Olboroto hadi Singida barabara hii imeanza Arusha-Dodoma hadi Singida Km 60.
Pia kutakuwa na baraabra kati ya Igawa na Songwe mpaka Tunduma ambayo ni Km 218.
Mradi wa tano ni Masasi-Nachingwea hadi Liwale Km 175, Barabara ya Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiri River,Lalago, Maswa nayo ni kwa kiwango cha lawi na Barabara na Mafingo –Mtwango kwa kiwango cha lami, kwahiyo miradi hii yote saba itatuchukua muda hasa miaka mitano kuunganisha nchi nzima kama miradi ya muhimu sana.
Swali: Kuna kesi ngapi za makandarasi wanaoidai Tanroads kwa tofauti za kimikataba?
Jibu: Katika mazingira yeyote ya mkataba lazima migogoro tukutane nayo, ndio maana kwenye mikataba yote kuna sehemu ya utatuzi wa migogoro.
Kiwango cha kwanza ikitokea kutokuelewana kati ya taasisi na mkandarasi au mshauri mnaingia kwenye utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani ‘amicable settlement of disputes’ hatua hii tunaposhindwa kuafikiana ndio tunafikia hatua ya kushitakiana.
Mpaka sasa kuna kesi sita zinaendelea kati ya Tanroads na wakandarasi, kati ya kesi hizo mbili tumeshitakiwa sisi na tumewashitaki wakandarasi wanne,
Wale waliotushitaki wanatudai takribani Sh2 bilioni, kwa wale tuliowashitaki kutokana na sisi kutoridhika na kazi yao tunawadai Sh92 bilioni na kitengo chetu cha sheria kinafuatilia na wakandarasi wote ni kutoka nje ya nchi.
Swali: Miongoni mwa changamoto zinazotajwa katika ujenzi wa barabara ni ucheleweshaji wa fedha za miradi kwa makandarasi kiasi cha kuongeza riba na hatimaye gharama za ujenzi wa barabara. Je, hali hiyo imewaathiri kiasi na mnaitatua vipi?
Jibu: Ni kweli tunategemea sana Serikali katika utoaji wa fedha na ucheleweshaji wa malipo unatokana na uwezo wetu wa ndani kulipa wakandarasi,
Kupitia ushirikiano uliopo baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya fedha tunatafuta kila aina ya mbinu kuhakikisha madeni hayo hayaendelei kukua,
Ni kweli kiasi cha madai husababisha riba ambayo si kitu kizuri kwa Taifa na mategemeo ya wananchi kupata huduma ya barabara, kwa hiyo hatua tunachukua,
Leo hii tumechukua hatua kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhakikisha madeni haya tunalipa kimkakati na kuweka mbinu mbadala kuhakikisha madeni haya hayaendelei kukua na pengine huko mbele tutafute namna bora zaidi kuhakikisha hali hii haitojitokeza tena.
Swali: Kiasi gani kinatumika kwa ajili ya ukarabati wa barabara kila mwaka?
Jibu: Kwa wastani miaka mitatu iliyopita hadi sasa bajeti ya ujenzi wa barabara haijabadilika na hii ni kutokana na upatikanaji wa fedha kuwa mgumu, kwa mwaka huu wa fedha mpya bajeti iliyotengwa kukarabati barabara katika mikoa 26 nchini ni Sh534 bilioni.
Kati ya hizo Sh416 ni kwa ajili ya matengenezo ya barabara na Sh118 kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi za mikoa, nipende kusema kwamba kazi ya matengenezo ya barabara inafanywa na ofisi za mikoa na shughuli zote hizi zinafanywa kwenye ofisi hizo,.
Swali: Chanzo cha uharibifu wa barabara hizo ni nini?
Unaposanifu barabara huwa tunasanifu iishi miaka 20 na kitu kinachosababisha uharibifu ni matumizi ya vitu vizito zaidi, kutumiwa kupita kiasi, pia lami ni kitu kinachozeeka mabadiliko ya hali ya hewa huifanya kuzeeka.
Kubeba mzigo kupita kiasi kunaweza kuifanya barabara ya kuka miaka 20 ikakaa miaka miwili,
Swali: Kwa kuwa sasa umeingia kwenye uongozi wa Tanroads, ni mambo gani unayotarajia kuanza nayo na una mikakati gani kuleta mageuzi katika sekta ya barabara?
Jibu: Cha msingi kabisa ni kuhakikisha tunatumia teknolojia mpya kuhakikisha tunapunguza matumizi ya fedha na kuongeza uhai wa barabara kwa kutumia teknolojia.
Jambo lingine tutahakikisha taasisi yetu inajenga uwezo wa ndani kwa wataalamu wetu, kama unavyojua mtandao wetu ni mkubwa sana kwa hiyo mtandao wetu unahitajika wengi zaidi katika maeneo mbalimbali bila kuwa na wataalamu wa barabara wanaoaminika na kusimamia barabara vizuri hatutaweza kwenda vizuri,
Jambo la tatu inabidi tuondokane na utegemezi uliopitiliza wa fedha za Serikali tutafute fedha na mbinu mpya ili Serikali itafute fedha ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja kwenye sekta ya afya na maji.
Sisi wataalamu tushirikiane wizara ya fedha kutafuta fedha kutoka kwa wadau wengine, wananchi wanataka kuona tunajenga barabara kwa kasi bila kupata hasara inayotokana na riba hiyo ni moja ya vitu ambavyo tunatazama kuvifanya kupunguza mzigo wa Serikali na iwe malengo ya Tanroads, tufikirie barabara ni amana ambayo tunaisimamia lakini kuwepo wadau wengine wanaoshiriki kuzijenga na kuzitunza.
Pia kwenye mradi wa PPP tupo hatua za mwisho kwenye mradi huo kutoka Kibaha hadi Morogoro tunakwenda vizuri, tumefikia pazuri tutakuwa kama mradi wa Uganda wa kutoka Entebe hadi Kampala na huu mradi kutoka Kibaha hadi Chalinze tunaukamilisha hivi karibuni kwa hiyo ni mapinduzi katika utoaji wa kandarasi ya barabara na ujenzi.