Mhasibu asimulia walivyoukuta mwili wa miliki wa kiwanda mtaroni
Muktasari:
- Simanzi imetanda kiwandani, Mabibo Sokoni baada ya mmiliki wa kiwanda cha plastiki, kuuwawa kisha mwili wake kuokotwa mtaroni ndani ya kiwanda, huku Jeshi la Polisi likiendelea kuchunguza tukio hilo.
Dar es Salaam. Simanzi imetawala ndani ya kiwanda cha XIL LI kilichopo Mabibo Sokoni, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, baada ya mmiliki wa kiwanda hicho kuuwawa na mwili wake kutupwa kwenye mtaro wa kiwandani.
Mmiliki wa kiwanda hicho ni raia wa China, Bhaozang Ge (50), alikuwa anaishi ndani ya kiwanda hicho akiwa na mfanyakazi mwingine wa Kichina pamoja na walinzi.
Kiwanda hicho kinajihusisha na uchakataji wa plastiki na uzalishaji wa malighafi zinazotumika kutengenezea bidhaa mbalimbali za plastiki, huku kikiajiri mamia ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Mei 19, 2026 Mhasibu wa kampuni hiyo, Eversophy Michael, amesema hakuna mfanyakazi aliyedhani siku hiyo ingeishia kwa kuuona mwili wa mwajiri wao ukiwa umetupwa mtaroni ndani ya kiwanda hicho.
“Tulifika asubuhi ya Jumamosi kama kawaida tukitegemea walinzi watufungulie geti, lakini tuligonga sana hakuna aliyekuwa anajibu, hapo ndipo hofu ilianza,” amesema Eversophy.
Amesema walijaribu kumpigia simu Bhaozang Ge mara kadhaa lakini simu yake haikupokewa jambo lililozidi kuwapa wasiwasi wafanyakazi waliokuwa wamekusanyika nje ya geti.
Eversophy amesema walimuita mfanyakazi mwingine wa Kichina aliyekuwa ndani ambaye hajui lugha ya Kiswahili vizuri ili awafungulie geti na walipoingia ndani walikuta hali ya ukimya mzito.
“Tulipoingia ndani tulikuta walinzi waliokuwa zamu usiku hawapo, lakini simu ya bosi ilikuwa ikiita ndani ya chumba chake hivyo tukapata wasiwasi na kuhisi kutakuwa na tatizo limejitokeza usiku,” amesema.
Amesema walipofungua chumba hicho walikuta simu ya Bhaozang Ge ikiwa ndani huku mwenyewe hayupo, hivyo walitoka nje ya kiwanda kwa ajili ya kuuliza walinzi wa geti lingine kama walimuona bosi wao akitoka.
“Hapo kila mtu alichanganyikiwa ndipo tulianza kuhisi kuna jambo baya limetokea usiku,” amesema Eversophy.
Kutokana na hali hiyo, amesema walianza kupiga simu katika vituo mbalimbali vya polisi wakidhani huenda kulikuwa na ugomvi uliosababisha baadhi ya watu kupelekwa kituoni, lakini hakuna taarifa iliyokuwa imepokelewa.
Katika hali ya sintofahamu, amesema walimuuliza mlinzi aliyekuwa kwenye geti kubwa ambaye aliwaeleza saa tisa usiku aliwaona walinzi wawili wa Kimasai wakiondoka, huku mmoja wao akiwa amebeba begi mgongoni.
“Walidai wanapelekana hospitali kwa sababu mmoja wao alikuwa anaumwa, kwa kuwa walikuwa walinzi wetu, hakuna aliyewashuku,” amesema.
Baada ya maelezo hayo, wafanyakazi walianza kuzunguka kila kona ya kiwanda hicho wakimtafuta mwajiri wao huku hofu ikizidi kuongezeka, kwani mmiliki huyo hakuwahi kutoka nje ya geti peke yake na bila sababu za msingi.
Amesema walikuwa wanatembea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho wakiwa na wasiwasi mkubwa, kila mmoja akiwa anaomba moyoni asikute jambo baya.
Lakini amesema safari yao iliishia kwenye simanzi kubwa baada ya kuufikia mtaro uliopo karibu na mashine za kusaga ndani ya kiwanda hicho.
“Tulipofika eneo la kuwashia mashine za kusaga malighafi ndipo tulikuta damu na mwili wa bosi wetu ukiwa kwenye mtaro, kila mtu alipigwa na butwaa watu walianza kulia, wengine wakashindwa hata kuzungumza,” amesema mhasibu huku machozi yakimlenga.
Eversophy amesema kilichowapa mashaka zaidi ni kutoweka kwa walinzi waliokuwa zamu usiku pamoja na begi lililokuwa na fedha za matumizi ya kiwanda.
Amesema kilichowauma zaidi ni kuona mtu ambaye kabla ya mauti walimuacha akiwa mzima na siku inayofuata wamemkuta amekufa kikatili, ambapo wafanyakazi kwa sasa wanaishi kwa hofu na majonzi kutokana na kumpoteza mwajiri wao ambaye alikuwa tegemeo la familia nyingi.
Mhasibu huyo amesema baada ya kutokea kwa tukio hilo walipiga simu kwenye kampuni ya ulinzi waliyoingia nayo mkataba ambapo bosi wao alipofika eneo la tukio na kuelezwa jambo hilo alishangaa, kwani na yeye alipigiwa simu zaidi ya tano na walinzi waliokimbia.
Kuhusu msiba, amesema kwa sasa upo kiwandani hapo ambapo wanamsubiri mkewe afike kutoka China ili kujua kitakachoendelea.
Mfanyakazi wa kampuni hiyo, Felista Deus amesema taarifa za kifo cha mwajiri wao zimewaumiza wafanyakazi wengi kwa sababu hawakutarajia tukio hilo kutokea.
“Kiukweli taarifa za bosi wetu kuuawa katika mazingira ambayo hata sisi wafanyakazi hatuyaelewi zimetusikitisha, hapa tunashindwa hata cha kusema kwa sababu ni jambo lililotuumiza,” amesema Felista.
Amesema hadi sasa wafanyakazi wengi hawajui hatima ya kampuni hiyo wala ajira zao baada ya tukio hilo kwani kiwanda hicho kilikuwa kinawasaidia wao na familia zao.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kifo cha raia wa China, Bhaozang Ge.
Taarifa ya umma iliyotolewa leo Mei 19, 2026 na Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Mei 16, 2026 saa 2:00 usiku, ambapo marehemu alishambuliwa na walinzi binafsi wa kiwanda chake, hali iliyosababisha kifo chake.
“Upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili watuhumiwa wachukuliwe hatua zaidi kali za kisheria,”ameeleza Muliro kwenye taarifa hiyo.