Kijana auawa Arusha kisa hajasalimia
Muktasari:
- Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo Mei 18, 2026, inaelezwa Emmanuel alikuwa akitokea kazini na kupitia kwenye kijiwe kilichokuwa jirani na nyumbani kwao, ambapo alikuta vijana watano wakiwa wamekaa.
Arusha. Kijana Emmanuel Thomas (36), mkazi wa eneo la Sinoni jijini Arusha, ameuawa kwa kuchomwa visu na ndugu zake kufuatia ugomvi uliodaiwa kusababishwa na salamu.
Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo Mei 18, 2026, linadaiwa kutokea wakati Emmanuel akitoka kazini na kupitia kwenye kijiwe kilichokuwa jirani na nyumbani kwao, ambapo alikuta vijana watano wakiwa wamekaa.
Inadaiwa aliwasalimia vijana watatu kwa kuwapa mkono kwa ishara ya ‘tano’ huku akiwaacha wawili ambao ni watoto wa ndugu yake bila kuwapa salamu hiyo.
Hali hiyo ilidaiwa kuwakasirisha vijana hao, ambao walimtaka awasalimie kwa nguvu kabla ya kuzuka kwa ugomvi.
Katika purukushani hizo, mmoja wa vijana hao anadaiwa kutoa kisu mfukoni na kumchoma Emmanuel shingoni, kifuani upande wa kushoto na kwenye mbavu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru.
“Katika tukio hilo, tunawahoji watu kadhaa na upelelezi ukikamilika tutachukua hatua nyingine za kisheria,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu idadi ya watuhumiwa waliokamatwa, amesema: “Subirini taarifa rasmi zitatolewa.”
Mama wa marehemu, Hellena Lomayani amesema akiwa nyumbani alisikia ukunga ukitokea barabarani karibu na nyumba yao, ndipo alipokimbilia eneo la tukio.
“Kama watu wengine walivyokuwa wanakimbia, na mimi nilielekea huko bila kujua ni tukio gani lililosababisha vilio.
“Nilipofika nilimkuta mwanangu kipenzi amelala chini nikajua labda amezimia.”
“Niliogopa kuona hali ile, nikarudi nyumbani na kumpigia simu kaka yake mkubwa aje amuangalie.”
“Niliporudi eneo la tukio ndipo nikapewa maelezo kuwa mwanangu amelala pale baada ya wadogo zake wa boma kulazimisha awasalimie na alipokataa walimchoma visu hadi kufa.
“Niliumia sana lakini sikuwa na cha kufanya. Nililia kama mtoto mdogo kuona mwanangu anakufa kifo cha ghafla kwa kudhulumiwa na watoto wa boma letu wenyewe,” amesema.
Mama huyo amesema mwanaye alikuwa kijana mwenye upendo, heshima na usikivu mkubwa kwa jamii tofauti na vijana wengi wa sasa.
“Alikuwa kijana msikivu na mwenye upendo sana lakini ndio nimeshapoteza, naomba jamii ihamasishe watoto wamrudie Mungu, mimi tayari nimeshapoteza mwanangu kwa vitendo visivyo vya kimaadili kama hivi,” amesema.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, baba wa marehemu, Thomas Mollel amesema mwanaye alikuwa akitokea kazini saa 4 usiku na alipitia madukani ambapo aliwasalimia baadhi ya vijana kwa kuwapa ‘tano’ huku wawili wakidaiwa kuachwa bila salamu.
“Inadaiwa wale vijana waliuliza kwa nini hajawasalimia, ndipo marehemu akawaambia kwani lazima? Ndipo ugomvi ukaanza na wakamchoma visu,” amesema.
“Hii imeniuma sana, afadhali mwanangu angeugua nikampeleka hospitalini nikajua Mungu amemchukua, lakini amedhulumiwa haki yake ya kuishi na wanadamu wengine tena vijana wadogo,” amesema.
Amesema matumizi ya bangi na pombe miongoni mwa vijana, pamoja na tabia ya kutembea na silaha hasa mapanga na visu, ni miongoni mwa sababu zinazochochea vitendo vya uhalifu katika jamii yao.
“Hawa watoto walipaswa wao ndio wawasalimie wakubwa, si kudai kusalimiwa, hizi ni bangi na pombe wanazotumia kila kukicha zimechangia dharau na uchokozi wa namna hii,” amesema.
Kaka wa marehemu, Nicholas Thomas, amesema baada ya kupata taarifa alifika eneo la tukio na kumuwahisha mdogo wake hospitalini lakini hakuweza kuokoa maisha yake.
Shuhuda wa tukio hilo, Rehema Lebayo amesema baada ya ugomvi kuzuka baadhi ya wananchi waliwazuia vijana hao na kupiga simu polisi kabla ya gari lao kufika eneo la tukio na kuwachukua watuhumiwa.
“Gari la polisi lilifika kwa wakati na kuwachukua watuhumiwa wawili, mmoja akitajwa kuwa na umri wa miaka 20 na mwingine miaka 16,” amesema.
Dada wa marehemu, Elizabeth Thomas, amesema kaka yake alikuwa mtu mpole na asiye na ugomvi.
“Eti kisa hajawasalimia ndio wamemuua, kama hujasalimiwa si uendelee na shughuli zako.”
“Bangi na pombe za mitaani wanazokunywa na kuvuta zinasababisha watoto wadogo kutembea na visu na mapanga kana kwamba ni jambo la kawaida, wakati ni ushamba,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Jeshi la Polisi kushirikiana na viongozi wa mtaa na kata kufanya operesheni na doria za mara mara kukamata vijana wanaojishughulisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo kuuza na kutumia bangi na pombe haramu, lakini pia wizi wa mara kwa mara.
Wakutwa na dawa za kulevya
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 64 baada ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi na kujihusisha na utengenezaji wa pombe haramu ya moshi.
Kati yao watuhumiwa 19 walikutwa na kilogramu 90 za mirungi na 12 waliokutwa na misokoto 177 ya bangi huku watuhumiwa 33 wakikutwa wakijihusisha na utengenezaji na usambazaji wa pombe haramu ya moshi.
Mbali na watuhumiwa hao, pia, jeshi hilo limefanikiwa kukamata mitambo tisa ya kutengeneza pombe ya moshi na lita 434 za pombe hiyo.
Kamanda Masejo amesema watuhumiwa hao wamepatikana katika operesheni mbalimbali zilizofanyika katika kipindi cha kuanzia Aprili 18, 2026 hadi sasa.