Wanaodaiwa kumuua mteja kwa kipigo Mwanza, wapandishwa kizimbani
Watuhumiwa wa kifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela iliyopo Jijini Mwanza kwa ajili ya kusomewa shtaka la mauaji. Picha na Polisi
Muktasari:
- Ikumbukwe kuwa Mei 11, 2026 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa Yunusu aliuawa kwa kushambuliwa kwa ngumi, mateke na vipande vya mbao na bomba la chuma katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani mlinzi (baunsa) pamoja na mfanyakazi wa usafi waliokuwa wakifanya kazi katika baa ya Las Vegas, wakituhumiwa kwa mauaji ya mkazi wa Mwanza, Mzafuru Yunusu.
Ikumbukwe kuwa Mei 11, 2026 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa Yunusu aliuawa kwa kushambuliwa kwa ngumi, mateke na vipande vya mbao na bomba la chuma katika sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kushindwa kulipa bili ya vinywaji ya Sh8,000 baada ya kunywa kwenye baa hiyo
Washtakiwa hao ni Yohana Peter (22), ambaye ni mlinzi wa eneo lilipotokea tukio hilo na Hamis Mussa (27), mfanyakazi wa usafi.
Wawili hao wamepandishwa kizimbani leo Alhamisi Mei 14, 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela na kusomewa shtaka la mauaji.
Akisoma shauri hilo la jinai namba 10492 la mwaka 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Christian Mwalimu, Wakili wa Serikali Clara Muhando, akisaidiana na Evance Kaiza, aliieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo mnamo Februari 05, 2026 katika baa ya Las Vegas iliyopo eneo la Kona ya Bwiru, mtaa wa Nyamanoro, Wilaya ya Ilemela.
Washtakiwa wote wawili, wakiwa katika baa hiyo ya Las Vegas, wanadaiwa kumshambulia na kumuua Mzafuru Yunusu (26) kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Hata hivyo, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza mashauri ya mauaji.
"Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili, kwa hiyo hamtatakiwa kujibu chochote juu ya tuhuma zenu. Vilevile, kesi inayowakabili haina dhamana, hivyo mtaendelea kuwa mahabusu hadi pale upelelezi utakapokamilika," amesema Hakimu Mwalimu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 28, 2026, na washtakiwa wamerejeshwa rumande.