Anayedaiwa kumuua muongoza filamu, kuendelea kusota rumande
Muktasari:
- Rehema anadaiwa kumuua muongoza filamu nchini, Athuman Nyanza tukio analodaiwa kulitenda Februari 10, 2026 eneo la Mwapemba, Kigamboni
Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Kigamboni Mwapemba, Rehema Hassan(42) anayekabiliwa na kesi ya mauaji, ataendelea kusalia mahabusu hadi Mei 26, 2026 kesi yake itakapotajwa tena, kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Rehema anadaiwa kumuua muongozaji na msimamizi wa sauti za filamu nchini, Athuman Nyanza.
Wakili wa Serikali, Titus Aron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Mei 13, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa njia ya video, huku mshtakiwa akiwa mahabusu.
Aron amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, anayesikiliza kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake haujakamilika.
“Hivyo, Jamhuri inaomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa," amesema Wakili Aron.
Hakimu Mwankuga, baada ya kusikiliza maelezo ya Jamhuri amekubaliana nayo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 26, 2026 itakapotajwa kwa njia ya video.
Kesi ya msingi
Rehema anadaiwa Februari 10, 2026 eneo la Mwapemba lililopo Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam, ulimuua Athuman Nyanza.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, kinyume na kifungu 196 na kifungu 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo Aprili 29, 2026 na kusomewa shtaka hilo.
Hata hivyo, kesi ya mauaji ni miongoni mwa mashtaka ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria na ndio sababu ya Rehema kuendelea kusalia rumande.