Prime
Kauli ya mwisho bodaboda aliyechinjwa Tanga 'Ninawapakia ngoja niombe Mungu'
Muktasari:
- Wenzake waeleza walivyomuonya asiwapakie abiria wale, akasema ngoja niombe Mungu
Tanga. Wakati familia ya Abdallah Chambo, mwendesha bodaboda aliyeuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana wilayani Handeni, Tanga ikiendelea kuomboleza kifo chake, simulizi kutoka kwa baba yake na wenzake vinaeleza namna tukio hilo lilivyotokea na maisha aliyokuwa akiishi kabla ya mauti kumkuta.
Baba mzazi wa marehemu, Andrea George Chambo, mkazi wa Mtaa wa Kilole wilayani Handeni, amesema mwanawe alikuwa tegemeo kubwa kwa familia licha ya kujishughulisha na biashara ya kawaida ya bodaboda.
Amesema Abdallah alikuwa akijituma kutafuta maisha kwa njia halali huku akiwa na ndoto nyingi za kuboresha maisha yake na ya familia yake.
Kwa mujibu wa Chambo, taarifa za kutoweka kwa mwanawe zilianza kusikika majira ya saa moja na dakika 45 usiku, lakini yeye hakuelezwa mara moja kutokana na hofu ya namna angepokea habari hizo.
“Majira ya saa nne ndipo taarifa zilifika kwa familia, lakini kwangu zilicheleweshwa kwa sababu waliamua kunificha kwanza,” amesema kwa huzuni.
Baba huyo amesema bado anapokea taarifa mbalimbali kuhusu mazingira ya mauaji ya mwanawe, lakini haoni ni sahihi kuzungumzia kila jambo hadharani kabla ya uchunguzi kukamilika.
“Msiba huu ni mzito sana. Naomba vyombo vya uchunguzi viendelee kufanya kazi yake ili siku moja familia iweze kusikia waliohusika wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.
Chambo amesema maneno ya mwisho anayoyakumbuka kutoka kwa mwanawe yalihusu mipango ya maisha na mustakabali wa familia yake.
Amesema Abdallah alikuwa tayari ana watoto wawili, mmoja nje ya ndoa na mwingine kwa mwanamke aliyekuwa akiishi naye, huku akiwa na mpango wa kufunga ndoa rasmi na kuanzisha maisha mapya.
“Alikuwa na ndoto ya kununua pikipiki yake mwenyewe kwa ajili ya biashara ya bodaboda. Hilo lilikuwa lengo lake kubwa,” amesema baba huyo.
Mbali na hilo, amesema mwanawe alikuwa na maono ya kujenga nyumba yake kwa kuwa alikuwa akiishi kwa baba yake mkubwa, na tayari alikuwa ameanza kutafuta kiwanja kwa ajili ya kutimiza ndoto hiyo.
Akizungumzia mazingira ya tukio, Chambo amesema maelezo anayoyapata yanaonyesha kuwa watu waliotekeleza mauaji hayo walikuwa wamefika muda mrefu kwenye kituo cha bodaboda kabla ya mwanawe kuwasili.
“Wenzake walikuwa tayari wamewatilia shaka na wakakataa kuwabeba. Mwanangu alipofika hakujua yaliyokuwa yameendelea, akawachukua ndipo yaliyotokea yakatokea,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amezungumzia tukio hilo na kusema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku likiomba ushirikiano kutoka kwa wananchi.
Wakati huo huo, baadhi ya waendesha bodaboda waliokuwa wakifanya kazi pamoja na marehemu wameeleza jinsi walivyoanza kupata mashaka kabla ya tukio hilo kutokea.
Khalifa Ally amesema wakati wao wanaanza kazi ya bodaboda, Abdallah alikuwa bado anaendelea na masomo, lakini baadaye aliingia kwenye biashara hiyo huku pia akiwa na kipaji cha muziki.
“Akipenda sana kazi za DJ. Kuna kipindi aliacha kidogo bodaboda akaenda kujifunza kazi hiyo ya muziki ambayo pia ilikuwa ikimwingizia kipato,” amesema Ally.
Amesema marehemu alikuwa mtu mwenye bidii ambaye hakuchagua kazi mradi iwe halali na imsaidie kujikimu.
“Wakati mwingine anafanya bodaboda, wakati mwingine anaitwa kwenye shughuli za muziki kufanya kazi yake ya DJ,” amesema.
Akieleza kuhusu siku ya tukio, Ally amesema yeye na wenzake waliingiwa na mashaka kutokana na mwenendo wa watu waliokuwa wanatafuta usafiri usiku huo.
Amesema watu hao walikaa kwa muda mrefu karibu na kibanda cha chipsi kilichokuwa kimefungwa katika eneo la giza huku wakizungumza kwa sauti za chini, jambo lililowafanya baadhi ya madereva wa bodaboda kuwakataa.
“Tulishawatilia shaka na tukawakataa. Mwenzetu alipofika alisema, ‘ngoja niombe Mungu,’ kisha akaondoka nao,” amesema.
Amesema baada ya Abdallah kuchelewa kurejea, walianza kupata hofu na kujaribu kumpigia simu, lakini simu moja haikupatikana huku nyingine ikiita bila kupokewa.
Hali hiyo iliwalazimu kuanza msako wa kumtafuta kwa kujigawa katika makundi na kupitia maeneo mbalimbali waliyoelekezwa.
“Ndipo tulimkuta akiwa amechinjwa na watu hao wameondoka na pikipiki yake,” amesema.
Kwa upande wake, Abdallah Andrea amesema siku hiyo marehemu alikuwa ametumia pikipiki ya ndugu yake baada ya kupewa kwa ajili ya kupeleka watu msibani.
Alisema baada ya kunyeshewa mvua, alirudi nyumbani kubadilisha nguo kabla ya kurejea tena kituoni, ambako aliwakuta watu hao na kuondoka nao.
Katibu wa Umoja wa waendesha bodaboda Wilaya ya Handeni, Khamis Kidunda maarufu Sakatonge, amesema tukio hilo limewashtua sana waendesha bodaboda wilayani humo.
Amesema kuna haja ya kutoa elimu zaidi kwa madereva wa bodaboda kuhusu namna ya kutambua abiria wenye nia ovu, hasa nyakati za usiku.
“Changamoto kubwa kwa bodaboda ni matukio ya uporaji, kujeruhiwa na kuuawa. Tukitoa elimu vizuri tunaweza kupunguza matukio haya,” amesema.