Prime
Mwanafunzi mwingine wa chuo hajulikani alipo kwa siku 13
Muktasari:
- Tukio hilo linajiri wakati bado jamii haijapoa mshtuko wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba, ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umetupwa katika Mto Msimbazi bila kichwa.
Dar es Salaam. Yuko wapi Mtatiro Chacha? Hilo ndilo swali linalozidi kuzungumzwa miongoni mwa wanafunzi na jamii ya elimu ya juu nchini, kufuatia taarifa za kupotea kwa mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), ambaye inadaiwa hajaonekana tangu Aprili 24, 2026.
Tukio hilo linajiri wakati bado jamii haijapoa mshtuko wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba, ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umetupwa katika Mto Msimbazi bila kichwa, na leo amezikwa mkoani Kilimanjaro.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikiliwa watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Temba.
Hilo linakuja kukiwa na taarifa nyingine za tukio la kupotea kwa Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu ‘Rahma’ (22) ambao wanadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Juni 20, 2025, mkoani Arusha, baada ya kuhudhuria sherehe ya kupongezana kufuatia kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza wa chuo.
Polisi mkoani Arusha imeomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wenye taarifa za kuhusika na kupotea kwa wasichana hao.
Hali hiyo imeibua wasiwasi kwa wanafunzi wa vyuo na wazazi kwa kile walichoeleza hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kukomesha hali hiyo inayoonekana kuota mizizi.
Taarifa za kupotea kwa Chacha, anayesoma mwaka wa nne katika Programu ya Land Management and Evaluation (LMV) zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana Jumatano, Mei 6, 2026 kufuatia tangazo lililotolewa na Serikali ya wanafunzi ya chuo hicho.
“Uongozi wa Serikali ya wanafunzi unapenda kuwataarifu mwanafunzi Mtatiro Chacha wa LMV 4 hajaonekana kwa kipindi cha siku tatu. Tunaomba yeyote mwenye taarifa za mahali alipo au aliyemuona hivi karibuni atoe taarifa haraka kupitia namba zilizopo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Viongozi wa wanafunzi wamesema juhudi za awali za kumtafuta zinaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na wenzake, familia na uongozi wa chuo, huku wito ukitolewa kwa umma kushiriki kutoa taarifa zozote zitakazoweza kusaidia kumtafuta.
Leo Alhamisi, Mei 7, 2026, Mwananchi imefika chuoni hapo na kuzungumza na Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Sinde Malagila ambaye amethibisha taarifa za kutoonekana mwanafunzi huyo.
“Ni kweli kama ambavyo umesikia Chacha ni mwanafunzi wetu na hayupo, taarifa za kutoweka kwake tumezipata kwa familia yake na kwa mujibu wa maelezo ya dada yake hajaonekana tangu asubuhi ya Aprili 24,2026.
Mtatiro chacha
“Hawa wanafunzi wa mwaka wa nne huwa hawaingii darasani katika mwaka wao wa mwisho badala yake wanautumia muda huo kufanya tafiti, hivyo vigumu kugundua hayupo kupitia chuo kwa sababu hakuna vipindi darasani vinavyowahusu,” amesema Malagila na kuongeza.
“Juzi Mei 4, 2026 ndiyo ndugu zake walikuja hapa chuoni kwa ajili ya kuwatafuta marafiki zake ndipo wakafika hadi ofisini na kuelezea kuhusu suala hilo, kuanzia hapo hadi sasa tunashirikiana nao pamoja na polisi kutafuta ni wapi anaweza kuwa amekwenda, hivyo tunaomba yeyote atakayekuwa na taarifa kumhusu atujuze.”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotafutwa kuzungumzia taarifa hiyo, simu yake iliita bila kupokewa.
Ilikuwaje
Malagila amesema kwa mujibu wa kaka wa Chacha aliyekuwa akiishi naye eneo la Tabata Mwananchi, kijana huyo aliondoka asubuhi ya Aprili 24 bila kueleza alipokuwa anaelekea.
“Kuondoka kwake hakukuwa na wasiwasi wowote kwa sababu ni mtu mzima na hata ambavyo hakurudi kwa siku za mwanzoni walijua yuko kwa wenzake au chuoni, sasa walipoona siku zinazidi ndipo walipoona si kawaida, wakaanza kumtafuta katika maeneo mbalimbali na hatimaye wakafika chuoni.
“Tulipowahoji waliwasiliana lini ili hata tujue wapi pa kuanzia labda kuna watu aliwasiliana nao, ilibainika kwamba simu ya Chacha ilipotea hivyo kwa muda mrefu hakuwa na mawasiliano,” amesema Malagila.
Mkurugenzi huyo wa huduma za wanafunzi amesema tukio hilo linaumiza vichwa si tu familia bali chuo na hata wanafunzi wenzake kwani ni mara ya kwanza kwa jambo hilo kutokea.
“Hatujawahi kukutana na jambo la aina hii, suala la usalama hapa chuoni liko vizuri na hata ingetokea amepotea akiwa hapa taarifa ingejulika muda huo huo, changamoto ni kwamba imetokea mtaani huko na zimepita siku kadhaa,” amesema.
Mwananchi ilizungumza na dada wa Chacha kwa simu ambaye alijibu kwa kifupi, “bado tunahangaika kumtafuta sijatulia, nikitulia tutazungumza.”
Kengele ya hatari
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam wameeleza hofu yao kufuatia kuongezeka kwa matukio yanayowahusisha wanafunzi katika mazingira ya kutatanisha, wakisema hali hiyo imeanza kuathiri utulivu wao wanapokuwa chuoni na nje ya vyuo.
Akizungumza na Mwananchi mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Neema Mushi amesema matukio hayo yanaongeza wasiwasi mkubwa kwa wanafunzi na familia zao.
“Kila mzazi anapompeleka mtoto chuoni anaamini yuko salama, lakini matukio haya yanaondoa amani ya akili. Tunaamini mamlaka zinapaswa kuongeza juhudi za haraka kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama,” amesema Neema.
Ramadhani Suleiman ambaye ni mwanafunzi wa IFM amesema wanafunzi wengi kwa sasa wamelazimika kuishi kwa tahadhari kubwa kutokana na hali inavyoendelea.
“Tukio la Temba lilitushtua lakini hili lingine limetushtua zaidi na kutufanya tuanze kuhoji usalama wetu hata tunapotoka kufanya shughuli za kawaida,” amesema Suleiman.
Kwa upande wake Stella Mwakyusa, mwanafunzi wa ARU, amesema ipo haja ya vyuo vikuu kuwa na mifumo madhubuti ya kufuatilia ustawi wa wanafunzi, hasa wale wa miaka ya mwisho wanaokuwa nje ya darasa kwa ajili ya tafiti.
“Wanafunzi wa mwaka wa mwisho wanatumia muda mwingi nje ya chuo, hivyo ni rahisi mtu kutokuwepo kwa muda bila kugundulika mapema,” amesema Stella.
Naye Kelvin Mrema wa ARU amesema jamii inapaswa kushiriki katika kuhakikisha usalama wa vijana, kwa kuwa karibu nao na kufuatilia mwenendo wao wa kila siku.
“Wakati mwingine vijana wanapitia changamoto mbalimbali lakini wanakosa watu wa karibu wa kuwasikiliza au kufuatilia hali zao, sasa hatujui huyu mwenzetu kimemkuta nini maana kama hata aliyekuwa anaishi naye hakumuga anakwenda wapi,” amesema.
Asha Mgema, mwanafunzi wa UDSM amesema matukio hayo yanaonesha umuhimu wa uchunguzi wa kina kufanyika na taarifa kutolewa kwa uwazi ili kuondoa hofu iliyopo kwa wananchi.
“Kwa sasa wanafunzi wengi wanajiuliza kama kweli wako salama wanapoendelea na masomo yao jijini Dar es Salaam,” amesema Mgema.
Akizungumzia hilo, Wakili Bashir Yakubu amesema matukio ya watu kutoweka ni matokeo ya utamaduni wa kujichukulia sheria mkononi, kujengeka kwenye jamii ilhali sheria zipo.
“Hakuna kitu ambacho hakijaelezwa kisheria, ila sijui kwa sababu gani utamaduni huu unaota mizizi na watu wanafikia hatua ya kujichukulia sheria mkononi. Ukweli ni kwamba matukio mengi ya watu kupotea yanahusisha watu kujichukulia sheria mkononi ndiyo haya unasikia mtu amepotea kisha anaokotwa amekufa.
“Polisi wanaweza kutusaidia kwenye suala hili kwa kuongeza nguvu, kuwabaini wanaofanya matukio haya kwa sababu wana uwezo huo na sasa kwa msaada wa teknolojia kwao inaweza kuwa rahisi zaidi kufanya uchunguzi na kupata matokeo,” amesema Yakubu
Hata hivyo, wakili huyo amewasihi vijana kuwa makini kwa kujilinda wao wenyewe na kujiepusha kushiriki katika matukio ya aina hiyo.
“Waathirika wengi ya matukio ya kupotea, kutekwa au kuuawa ni vijana sasa ni vyema wakawa makini na mienendo yao na hata watu wanaoshirikiana nao, siku hizi mambo ya uhalifu yamekuwa mengi,”amesema Yakubu.