Mgomo Soko Kuu Mafinga waingia siku ya tatu

Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamekaa nje wa Maduka yao katika soko kuu la Mji wa Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Picha na Mary Sanyiwa
Muktasari:
- Siku tatu sasa zimepita wananchi wa Mji wa Mafinga wameendelea kukosa huduma soko kuu wakieleza adha wanayopitia ya kukosa ikiwamo kukosa mahitaji muhimu.
Mufindi. Wananchi wa Halmashauri ya Mji Mafinga pamoja na maeneo ya jirani katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wameendelea kusota kwa kukosa huduma kwa siku tatu mfululizo katika Soko Kuu la mji Mafinga, baada ya wafanyabiashara wa soko hilo kufunga maduka yao.
Mgomo huo umeingia siku ya tatu na kusababisha adha kubwa kwa wananchi kukosa huduma huku ikiwa haijulikani lini watarejesha huduma hizo.
Mwananchi Digital ilifika sokoni hapo leo Jumapili Agosti 25, 2024 na kushuhudia milango ya maduka ikiwa bado imefungwa, huku baadhi ya wananchi waliofika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali wakiduwaa wasijue cha kufanya.

Akizungumzia mgomo huo mfanyabiashara wa soko hilo Damiani Kyando amesema wanaendelea kufunga maduka yao kwa sababu halmashauri imewaelekeza kulipa kodi ya pango ya Sh80,000 wakilalamikia kiwango hicho ni kikubwa kwao.
“Kwenye kibanda changu nilikuwa nalipa kwa mita moja Sh8,000 hadi 9,000 lakini kwa sasa imekuwa kama adhabu, tumeamriwa kulipa kodi ya Sh80,000 kwa mwezi lakini tumefanya jitihada mbalimbali za mazungumzo kuhusu jambo hili, ili liwe rafiki kwa wafanyabiashara bila mafanikio,” amesema Kyando.
Aidha Kyando amesema kufungwa kwa maduka hayo kuna athari ikiwemo wananchi kukosa huduma, halmashauri kukosa mapato hivyo viongozi hao wanapaswa kuangalia saula hilo kwa jicho la kipekee.
“Leo siku ya tatu tumeendelea kufunga maduka yetu hadi pale itakapojulikana hatma ya jambo hili kwa sababu hali ya kufunga na kufungua, inaonyesha kwamba sisi hatuna maumivu lakini tunapata maumivu makubwa sana katika jambo hili,” amesema Kyando.
Ameongeza, “Hasara ambayo tunaipata ikiwa fedha ya chakula ukizingatia wengine wana wagonjwa hospitalini pamoja na familia ambazo tunazihudumia na biashara zetu ndio kama hivi zimesimama hata Serikali inakosa mapato.”
Naye Benjamin Haule, mkazi wa Mafinga amesema mgomo huo una athari kubwa kwao kutokana na kufika sokoni hapo kwa ajili ya kupata huduma bila mafanikio, hali inayosababisha kurudi kijiji akiwa amepoteza nauli na muda.
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara walioulizwa wamesema kuna uwezekano wa kulipa Sh25,000 lakini si Sh80,000 kulingana na gharama za maisha kuwa juu na faida inayopatikana nindogo.
Wameeleza kuwa utitiri wa kodi ikiwemo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pango, ushuru wa taka na ulinzi ni gharama kubwa.
Akizungumzia mgomo huo Katibu wa soko hilo, Victor Mgani amesema changamoto kubwa iliyopo ni wafanyabiashara kulalamikia kodi kubwa ya pango.
“Sisi kama viongozi tunaona jambo hilo lina changamoto, kwa sababu ya ustawi wa mtu hivyo lazima liangaliwe na kufanyiwa kazi, kwa kuwa mtu hawezi kulipa kodi akiwa ananung’unika hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisema kila kukicha mtu anatakiwa kulipa kodi anayostahili.
“Kodi hii ilipangwa na mtu mmoja haina makubaliano ya watu kukubaliana kwamba fedha hiyo inalipwa katika mikono ipi,” ameeleza Katibu huyo.
Mgani ameongeza kuwa wafanyabiashara hao wameamua kufunga maduka yao, huku wakisema hawawahitaji viongozi wa wilaya na mkoa kwa sasa na badala yake wanamhitaji Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasaidia kumaliza jambo hilo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Boma, Julias Kisoma amesema mgomo wa wafanyabiashara unaleta madhara makubwa hususan kwa wananchi, ukizingia soko hilo linahudumia wilaya yote ya Mufindi.
“Hili ndiyo Soko Kuu ambalo linahudumia halmashauri zote mbili ya Mji Mafinga pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi watu kutoka pembe zote za wilaya hii wanategemea soko hili lakini leo ni siku ya tatu vibanda 331 vimefungwa na biashara haziendi hii ni shida kubwa,” amesema Kisoma.
Diwani huyo amefafanua kuwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Mei mwaka huu miongoni mwa ajenda walizojadili ni kupokea na kubariki kodi ambazo walikubaliana na wafanyabiashara hao ikiwemo kuendelea kumiliki vibanda hivyo kwa muda wa miaka 14 kwa kushirikiana na halmashauri hiyo.
Pia walikubaliana kodi ya pango wanayopaswa kulipa ni Sh50,000 sawa Sh25,000 kwa ajili ya fidia ya majengo na Sh25, 000 mapato ya halmashauri hiyo.
Awali akizungumzia mgomo huo, Mwenyekiti wa Soko hilo, Philinus Mgaya amesema; “Kupanda kwa kodi hiyo ya pango wafanyabiashara wameshindwa kuvumilia.
Hata hivyo wafanyabiashara hao wametoa ombi kwa Serikali kurejea kwa mpango wa awali wa halmashauri wa kulipa Sh50,000 ikiwa Sh25,000 kwa ajili ya kufidia ujenzi wa vibanda hivyo 331 kwa sababu vilijengwa na watu binafsi kwa gharama zao.
Jitihada za kuwasiliana na uongozi wa halmashauri na ofisi ya mkuu wa wilaya jana na leo ili wazungumzie suala hilo hazikuzaa matunda na simu zao zimekuwa zinaita bila kupokewa.