Mgombea ubunge ‘atoweka’, wazazi watumiwa ujumbe wa vitisho

Mgombea ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo katika Jimbo la Bariadi Magharibi, Masunga  Nghezo. Picha na Mpigapicha wa ACT-Wazalendo.

Muktasari:

Mbali na kutoonekana kwa Nghezo, simu yake aliyokuwa akiitumia, ndiyo inatumika kutuma ujumbe wa vitisho kwenda kwa mzazi wa mgombea huyo ikimtaka amkanye mwanae kuachana na siasa vinginevyo familia nzima itadhurika.

Bariadi. Mgombea ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo katika Jimbo la Bariadi Magharibi, Masunga  Nghezo ametoweka kusikojulikana na hajapatikana hadi sasa akiwa katika harakati za kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo hilo.

Mbali na kutoonekana kwa Nghezo, simu yake aliyokuwa akiitumia, ndiyo inatumika kutuma ujumbe wa vitisho kwenda kwa mzazi wa mgombea huyo ikimtaka amkanye mwanae kuachana na siasa vinginevyo familia nzima itadhurika.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Afisa Habari wake, Abdallah Khamis, imesema kuwa Nghezo alitoweka siku ya Jumatatu ya wiki hii akijiandaa kwenda katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Baneni.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kabla ya kutoweka kwake, Nghezo, alienda kumtafuta dereva mwingine wa kumuendesha baada ya yule wa siku zote kwenda msibani na kwamba aliporudi na dereva mwingine aliliacha gari likiwa katika maandalizi ya kufungwa vipaza sauti.

Taarifa imeongeza kuwa baada ya dereva na viongozi wengine wa chama kumaliza kazi ya kufunga vipaza sauti walianza kumtafuta mgombea wao bila mafanikio huku simu yake ikiwa haipatikani hadi jana mzee wake alipopokea ujumbe mfupi wa simu kupitia simu ya mwanae ikimtaka kumkanya mwanae aachane na siasa za Bariadi.

Pia taarifa ya Khamis inaeleza kuwa mzazi wa mgombea, Mzee Nghezo, anazidi kutumiwa ujumbe wenye masharti wakimpa muda wa saa sita kutekeleza masharti yao vinginevyo watamdhuru kijana wake na kisha kuitafuta familia nzima,

Hata hivyo Mwananchi Digital imezungumza na mzazi wa mgombea huyo, Joseph Nghezo ambaye amethibitisha kupotea kwa mtoto wake tangu siku ya Jumatatu.

Mzee Nghezo amesema kuwa siku ya Jumatatu viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo walimpigia simu wakitaka kujua kama mtoto wake yupo nyumbani, ndipo alishtuka kwakuwa alijua mwanawe yuko kwenye kampeni.

Ameongeza kuwa baada ya kuulizwa sana juu ya mtoto wake, majirani walimshauri aende akatoe taarifa katika kituo cha polisi.

‘’Tumeenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi hapa mjini Bariadi na polisi wamechukua maelezo hivyo wanafanya kazi’’ aliongeza Nghezo.

Mwananchi Digital imemtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi ili kuthibtisha tukio hilo lakini hakuweza kuzungumza lolote kwakuwa alipopokea simu alisema yuko kwenye kikao.