Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgogoro wa shamba Mbarali waua wawili, watatu mbaroni kwa mauaji

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mbeya,  linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili yanayodaiwa kufaywa na kundi la watu takribani 15

Mbeya. Wakazi wa Igurusi wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya, Wilbroad Mjengwa (38) na Maige Jirafu (44) wamedaiwa kuuawa katika mgogoro wa kugombea shamba huku watu watano wakijeruhiwa.

Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji hayo yanayodaiwa kufaywa na kundi la watu takribani 15.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ameiambia Mwananchi leo Jumanne Januari 14,2025 kuwa tukio hilo limetokea Januari 10, 2025 saa 10.00 jioni katika Kijiji cha  Shitanda Kata ya Luhanga wilayani humo.

 “Familia ya watu waliouawa walikuwa kwenye maandalizi ya kulima shamba hilo lenye mgogoro, ambalo wanamiliki kihalali kwa hati iliyotolewa mwaka 1987,” amedai kamanda huyo.

Amedai kuwa, mgogoro huo ulikuwa baina ya familia ya Raphael Mjengwa, mmiliki wa shamba la  hekari 1,050 na familia ya Mzee Malewa, waliodai kuwa walikuwa wakilitumia eneo hilo kwa kilimo na malisho ya mifugo.

“Wakati familia ya Raphael Mjengwa ikiendelea na maandalizi ya kilimo, walivamiwa na kundi hilo na shambulio hilo limesababisha vifo na majeruhi,” amedai Kuzaga.

Hata hivyo, anasema tayari Jeshi la Polisi limeshawatia mbaroni watu watatu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo baada ya msako uliofanyika Januari 13, 2025, usiku Kata ya Luhanga, Tarafa ya Ilongo.

Kamanda Kuzaga amesisitiza umuhimu wa jamii kujiepusha na tabia ya kujichukulia sheria mkononi, badala yake wafuate taratibu za kisheria.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia na Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi aliyehudhuria msibani hapo leo Jumanne, Januari 14, 2025, amelaani tukio hilo na kuhimiza uchunguzi wa kina na wahusika wakibainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.

David Mwampashe, mkazi wa eneo hilo ameiomba Serikali kutatua migogoro ya ardhi ili kuepusha matukio kama hayo yanayohatarisha usalama wa raia na mali zao.