Mganga wa jadi auawa, azikwa akiwa amekalishwa

Muktasari:
- Ester Juma, aliyeshuhudia mauaji asimulia wauaji walivyoingia chumbani kwake na kumuua mganga huyo na mkewe.
Dar/Kahama. Mganga wa tiba asili, Ngusa Jilumba (58) na mkewe Bugumba Mahola (54), wameuawa kwa kukatwa kwa panga na shoka, baada ya kuvamiwa nyumbani kwao na watu wasiojulikana.
Mauaji hayo yamefanyika katika Kijiji cha Sungamile kilichopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Wanandoa hao walipoteza maisha kwa kujeruhiwa kichwani na shingoni na wamezikwa kijijini Sungamile. Jilumba alizikwa kimila akiwa amekalishwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha mauaji hayo yaliyotokea katika Halmashauri ya Msalala.
Amesema wanandoa hao walituhumiwa kujihusisha na upigaji ramli chonganishi.
Amesema wanaendelea kufanya uchunguzi kubaini kiini cha mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina.
Kamanda Magomi pasipo kutaja idadi, amesema polisi inawashikilia watu kadhaa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Amesema bado kuna changamoto ya kuwapo waganga wa tiba asili wasiozingatia maadili, ambao wanapiga ramli chonganishi.
Katika msako uliofanyika ndani ya mwezi mmoja, amesema wamekamata vifaa kadhaa vinavyotumika kupigia ramli.
Kamanda Magomi amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, badala yake wafuate sheria ili kukomesha matukio hayo.
Akizungumza eneo la tukio, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sungamile, Charles Tungu amesema Januari 20, 2024 alipata taarifa za tukio hilo saa nane usiku.
Amesema kwa kushirikiana na kikundi cha ulinzi shirikikishi (Sungusungu) na polisi walilipata shoka lililotelekezwa shambani baada ya mauaji hayo.
Vileviloe, naye ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, huku akiomba wataalamu wa saikolojia kuwasaidia watoto walioachwa na marehemu, akiwamo mwenye ulemavu wa macho.
Mtoto huyo alikatisha ndoto zake za kuendelea na elimu katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo baada ya kupofuka alipomaliza kidato cha nne.
Ester Juma, aliyeshuhudia baba na mama yake mkubwa wakiuawa, amesema alikuwa amelala chumba kingine akasikia mlango ukipigwa na kitu kizito kisha ukafunguliwa.
“Nilisikia mlangoni paa, mama na baba mkubwa wakapiga kelele, mara nikasikia baba analia na kuanguka chini, mama aliyekuwa amejificha akajitokeza akasema tuna laki saba (Shilingi) tunaomba tuwape, sauti ikasikika hiyo laki saba tunaweza kununua ng’ombe sisi? Nikasikia tu mguu unakanyagwa paa, akaacha na kuongea, sasa wakatoka.”
“Chumbani kwangu aliingia baba mmoja hivi na panga akanisonda, walikuja saa saba. Nikasikia nyumba ya pili kaka asiyeona anapiga kelele na lilitumika shoka la hapa nyumbani walilitelekeza shambani, sasa tunaogopa, sijui tunaishije?” amesema.
Watoto wa marehemu, akiwamo Lukala Jilumba wameeleza kusikitishwa kwa tukio hilo, wakiomba vyombo vya dola kuendelea kuchunguza zaidi ili kuwabaini waliofanya mauaji hayo.
“Nasikitika wazazi wangu wawili kufariki dunia siku moja kwa ajali mbaya ya namna hii ya kukatwakatwa mapanga. Nina changamoto, sioni, naomba Serikali ilifuatilie hili tukio maana mimi ni mlemavu wa macho tangu mwaka 2018, wazazi wangu ndio nilikuwa nawategemea kwa kila kitu, kama kuna uwezekano nisaidiwe matibabu,” amesema.
Seni Jilumba, kaka wa marehemu amesema hajawahi kusikia mgogoro wowote, huku jirani Masumbuko Doto akisema saa 7:45 usiku alitumiwa ujumbe wa maandishi (sms) kwenye simu, ndipo alipopiga filimbi na mayowe kuita Sungusungu.
Mtemi wa Sungusungu katika halmashauri hiyo, Bundu Kahanya ameiomba Serikali kuimarisha ulinzi shirikishi.
“Tunashirikiana na Serikali ila tunaiomba iongeze nguvu hasa vyombo vya dola kushirikiana na sisi, mfano kupata vifaa vinavyoweza kunasa mapema watu wanaofanya vitendo kama hivi, tuunganishe nguvu maana wakati mwingine wahalifu wanakuwa na silaha nzito, sisi hatuna namna,” amesema.
Onesmo Daud, ambaye ni mwanasheria amesema watu waliopoteza maisha wamekoseshwa haki ya msingi ya kuishi.