Prime
Mganga wa jadi alivyomuua ofisa ardhi baada ya kumuuzia rupia feki kwa Sh20 milioni

Sumbawanga. Hivi ni kweli ukipata Rupia unatajirika au ni utapeli? Ni swali linaloibuka baada ya mganga wa jadi mjini Sumbawanga, Severino Choma kumuuzia ofisa ardhi Manispaa ya Mpanda, sarafu ya Rupia kwa Sh20 milioni kisha kumuua.
Maelezo ya mganga akisimulia namna yeye na mshirika walivyomuuzia ofisa huyo wa ardhi Rupia feki na kukodi pikipiki kwa Sh30, 000 na kwenda naye hadi mlimani kuifanyia tambiko rupia hiyo kabla ya kumuua, yatakuacha kinywa wazi.
Rupia au Rupee ni sarafu iliyotumika Tanganyika, sasa Tanzania, wakati wa ukoloni wa Wajerumani, kutoka mwaka 1890 hadi 1916 na kuendelea kuzunguka hadi 1920 na sasa inadaiwa kutumika kughilibu watu hutumika kumpa mtu utajiri.
Simulizi ya mauaji ya Hishim Muyinga, aliyekuwa Ofisa Ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, aliyeuawa Desemba 22, 2017 katika Kijiji cha Ujiji Manispaa ya Sumbawanga, inaanzia kwa mganga wa jadi aliyekuwa akimuagua.
Mganga huyo, sasa anasubiria kunyongwa baada ya rufaa yake kupinga hukumu ya kifo aliyohukumiwa Desemba 30, 2022 kutupwa na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani, Augustine Mwarija, Lilian Mashaka na Dk Eliezer Feleshi.
Katika hukumu yao waliyoitoa Machi 28, 2025, majaji hao walisema wameridhika kuwa mlolongo wa matukio unaoonekana katika maelezo ya mganga huyo ya kukiri kosa, yalithibitisha shitaka la Jamhuri dhidi yake pasipo kuacha mashaka.
Shitaka hilo lilithibitishwa kupia ushahidi wa mashahidi nane wa Jamhuri na vielelezo saba ambavyo ni pamoja na maelezo ya ungamo kwa mlinzi wa amani, kitabu cha wageni na maelezo yake ya onyo na vielelezo halisi vilivyokamatwa.
Ofisa ardhi alivyokutana na mganga
Mrufani ambaye alikuwa ni mshitakiwa katika kesi hiyo ya mauaji, Severino Choma, alikuwa akiishi eneo la Malangali katika Mainispaa ya Sumbawanga na walikutana na Ofisa Ardhi aitwaye Hishim kwa mara ya kwanza Julai mwaka 2017.
Hii ni baada ya ofisa ardhi huyo kufika kwa mganga huyo akihitaji huduma ya tiba na kuanzia hapo ofisa huyo akawa mteja wa mara kwa mara wa mganga na wakati mwingine akifika kwa mganga kupata matibabu, alikuwa akilala kwa mganga.
Mwanzoni mwa Desemba 2017 kulingana na ushahidi, ofisa huyo wa Serikali alimuomba mganga amtafutie sarafu ya zamani ya Mjerumani (Rupia) ambapo alimtafutia ila ilikuwa ni feki na walipokutana akamwambia inauzwa Sh20 milioni.
Siku hiyo walipokutana ambayo ni Desemba 15, 2007 nyumbani kwa mganga kwenye saa 5:00 usiku, ofisa ardhi huyo hakuwa na fedha hiyo hivyo akarudi Mpanda siku hiyo hiyo na kurudi tena kwa mganga huyo Julai 22, 2017.
Kulingana na ushahidi, siku hiyo alilipa Sh20 milioni, lakini baada ya kupita siku kadhaa, watoto waliokuwa wanachunga ng’ombe karibu na mlima Ulinji, waliona mwili wa mtu aliyekufa na kutoa taarifa kwa mwenyekiti na baadaye polisi.
Mwili ulipelekwa hospitali na kufanyiwa uchunguzi na kubainika kiini cha kifo chake ni majeraha mabaya aliyoyapata kichwani ambapo mganga alikamatwa na inadaiwa walipohojiwa polisi na kwa mlinzi wa amani, alikiri kutenda kosa hilo.
Huu ndio utetezi wake kortini
Lakini, baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi, mahakama ilimuona mganga ana kesi ya kujibu hivyo kutakiwa kujitetea ambapo alijiweka kando na mauaji hayo na kumrushia mpira mshirika wake kuwa ndiye aliyeua mbele yake.
Alijitetea kuwa yeye ni mfanyabiashara aliyekuwa anamiliki mgahawa, mashine ya kuchomea pikipiki na pia alikuwa ni mganga wa jadi na marehemu aliuawa ili kuficha kutokujulikana kwa ‘deal’ (mauziano) ya rupia bandia.
Katika kujitetea huko, alieleza kuwa mmiliki wa hiyo Rupia alilipwa Sh10 milioni wakati yeye na mshirika wake waligawana sawa Sh10 milioni na kwamba aliandika maelezo yake ya onyo polisi na baadaye aliomba kupelekwa kwa mlinzi wa amani.
Baada ya kusikiliza na kupima uzito wa ushahidi wa Jamhuri na utetezi wa mshitakiwa, mahakama ilimtia hatiani mganga huyo na kumhukumu adhabu ya kifo, lakini hakuridhishwa na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa.
Wakili wake, Deogratious Sanga alishikilia hoja kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa umeshindwa kuthibitisha shitaka dhidi ya mteja wake na mahakama ilikosea kumtia hatiani kwa kuegemea maelezo ya onyo ambayo yalipokelewa kimakosa.
Lakini, mjibu rufaa ambaye ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiwakilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Calistus Kapinga, akisaidiana na wakili wa Serikali, Joseph Mwakasege, walisisitiza Jamhuri ilithibitisha shitaka bila kuacha mashaka.
Mawakili hao walieleza kuwa kilichozaa mauaji hayo ni biashara ya Rupia feki na kwamba matendo ya mrufani ikiwamo kushindwa kutoa taarifa ya kitendo kilichokwenda kuzaa mauaji, kinadhihirisha dhamira ovu aliyokuwa nayo.
Hukumu ya majaji
Majaji katika hukumu yao, walisema Mahakama Kuu iliyosikiliza shauri hilo, iliridhika kuwa maelezo ya onyo ambayo mrufani aliyatoa polisi akikiri kutenda kosa la mauaji na yale yaliyotolewa kwa mlinzi wa amani, yalitolewa kwa hiyari.
Katika hitimisho lao, majaji hao walisema watachambua maelezo ya onyo ya kukiri kosa ambayo mrufani aliyatoa polisi na maelezo ya ungamo aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani ambayo kwa mujibu wa majaji hao yalikuwa yakijieleza yenyewe.
Maelezo ya onyo yanasomeka “Mwaka 2016 nikiwa naendelea na shughuli zangu za uganga nilifahamiana na (mshirika wake). Alianza kujifunza shughuli za uganga na kuwa msaidizi wangu. Aliweza kumpatia Hisim Zuberi namba yangu”
“Mwezi wa 07/2017 alifika nyumbani kwangu na kunieleza kuwa ana matatizo ya miguu na macho. Niliweza kumpatia dawa na alinipatia Sh200,000 na alilala siku moja. Tuliendelea kuwasiliana na mwezi wa tisa alikuja tena kuchukua dawa.”
“...mwezi wa 12/2017 mwanzoni akiwa Mpanda alinipigia simu na kunieleza kuwa anatafuta Rupia. Niliendelea kuitafuta nikiwa nimemshirikisha (mshirika wake) hivyo aliweza kuipata ambayo ilikuwa ni tarehe 15.12.2017,” anaeleza.
“Tarehe hiyo hiyo niliweza kumpigia simu Hisim Zuberi na kumweleza ambapo tarehe hiyo hiyo alianza safari na kufika saa 5:00 usiku ambapo alifikia nyumbani kwangu na nilimuonyesha Rupia na baada ya kuiona aliridhika….”
Kulingana na maelezo hayo, mrufani huyo anasema baada ya mteja wake kuridhika, alisema ana Sh15 milioni, lakini yeye akamkatalia na kumtaka akaongeze zifike Sh20 milioni, aliondoka na kurudi tena Desemba 22, 2017.
“Saa 5:00 usiku alifika nyumbani kwangu na baada ya kumpokea tulimuonyesha Rupia na aliiona ni yenyewe na ndipo alipotupa Sh20 milioni ambayo ilikuwa ndani ya kibegi cha mgongoni chekundu zikiwa zimewekwa kwenye bahasha…”
“Tayari tulikuwa tumekubaliana na mwenzangu kuwa Rupia tuliyompatia sio yenyewe na kwa kuwa sisi tulikuwa tunatafuta fedha na tumeshaipata tumdanganye ili aweze kuichukua inabidi kwenye kufanya matambiko porini,” amesema.
Katika maelezo hayo anaeleza kuwa walikodi pikipiki kwa Sh30,000 ambapo yeye ndio aliendesha akiwa na mshirika wake pamoja na marehemu ambapo walipofika mlimani, mshirika wake alimpiga marehemu kwa nondo kichwani.
“Kitendo hicho kilipelekea Hisim Zuberi kuanguka kifudi fudi ambapo mimi nilikimbia kuelekea tulipoacha pikipiki nikimsubiri mwenzangu ambapo alifika bila nondo na alinieleza kuwa mwili wa marehemu ameuvuta hadi kwenye kichaka,” amesema.
Maelezo hayo ya onyo, hayatofautiani sana na yale aliyoyaandika kwa mlinzi wa amani, ambapo majaji wakasema kwa maelezo hayo ni wazi mganga huyo pamoja na marehemu ni watu waliofahamiana vizuri tangu Desemba 2017.
“Mrufani ndiye aliyekuwa masterminder (kinara) wa kupatikana kwa Rupia feki na kumwita marehemu kutoka Mpanda tarehe 22.12.2017. Baada ya kufika ndio alimuongoza kwenda mlima wa Uliniji ambapo alimuuua,” walisema majaji.
“Baadae kama walivyopanga, waligawana mazao ya uhalifu huo wa Rupia feki baina yao. Kwa mazingira hayo tunakubaliana na mahakama iliyosikiliza kesi hii na kuukataa utetezi wa mshitakiwa kuwa hauna mashiko,”walisisitiza majaji.
Ni kwa msingi huo, majaji hao walisema wameridhishwa kuwa mnyororo wa matukio yanayoonekana kwenye ushahidi na vielelezo yakiwamo maelezo hayo yanathibitisha kuwa Jamhuri ilithibitisha shitaka hilo pasipokuacha mashaka.