Mganga Mkuu Moshi akutwa amekufa ‘gesti’
Moshi. Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (DMO) Kilimanjaro, Dk Alex Kazula amekutwa amefariki dunia kwenye nyumba ya kulala wageni iliyopo Manispaa ya Moshi.
Mwili wake ulikutwa kwenye nyumba hiyo usiku wa kuamkia Oktoba 9, mwaka huu.
Chanzo cha habari kimesema awali Dk Kazula alionekana akiwa na wageni katika nyumba hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori pasipo kutaja nyumba hiyo ya wageni alisema mwili wa Dk Kazula, polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wanachunguza mazingira ya kifo hicho kujua kimesababishwa na nini.
Kamanda wa Polisi Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema wanawashikilia wanawake wawili kwa tuhuma za kukutwa na simu za daktari huyo.
"Ni kweli DMO amefariki dunia kwenye nyumba ya kulala wageni, lakini tunawashikilia wanawake wawili," alisema Kamanda Maigwa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi, Shadrack Mhagama alisema lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 9.
"...mambo mengine bado yanashughulikiwa na vyombo vya dola, tusubiri wamalize mtapata taarifa," alisema Mhagama.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jairy Khanga alisema kifo cha daktari huyo kimetokea ghafla akiwa usingizini.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais –Tamisemi, Nteghenjwa Hosseah imeeleza wizara kusikitishwa na kifo cha daktari huyo, ikitoa pole kwa halmashauri, ndugu, jamaa, marafiki na watumishi wa halmashauri hiyo.
Mwananchi ilifika katika nyumba ya wageni iliyopo eneo la Soweto inayoelezwa kuwa ndiko alikofia daktari huyo.
Licha ya msimamizi wa nyumba hiyo kuwapo eneo hilo, hakuwa tayari kujibu maswali aliyoulizwa na mwandishi; badala yake aliondoka eneo hilo.
Mwananchi ilifika nyumbani alikokuwa akiishi daktari huyo eneo la KDC jirani na ofisi za halmashauri na kumkuta kijana aliyejitambulisha kama mmoja wa wanafamilia akisema hawako tayari kutoa taarifa yoyote na kuzuia wanahabari kupiga picha.
Katika eneo hilo, walionekana watu wakiwa katika makundi ambao nao hawakuwa tayari kuzungumza chochote kwa wanahabari.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi, Mhagama aliyekuwa eneo hilo alisema, "namna kifo kimetokea siwezi kusema maana ni mambo ambayo yapo kwenye vyombo vya dola kwa uchunguzi. Kwa sababu inaonekana alikuwa mahali fulani wikiendi na kuna watu alikuwa nao. Inasemekana watu aliokuwa nao walikuwa wanne na watu hao walimchukua mpaka maeneo hayo ambayo alikutwa amekufa,” alisema Mhagama.
“Mwingine aliweza kuondoka na simu yake, siwezi kusema sana maana liko kwenye uchunguzi na ukikamilika taarifa itatolewa.”
Alisema mwili wa daktari huyo utaagwa leo katika ofisi za halmashauri na baadaye kusafirishwa kwenda Iringa kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii.