Prime
Mganga aliyeshtakiwa kwa kusababisha vifo vya pacha aachiwa huru

Muktasari:
- Alishtakiwa kwa kuwapa dawa yenye sumu, hata hivyo, mawakili wa Jamhuri wameshindwa kuthibitisha bila kuacha shaka.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imemwachia huru mganga wa jadi, Zuwena Runigangwe aliyeshtakiwa kwa kusababisha vifo vya pacha, aliodaiwa kuwapa dawa yenye sumu, baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha shitaka.
Katika hukumu yake, Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, amesema kuna mkanganyiko wa ushahidi iwapo sumu hiyo iliingia mwilini kwa kumezwa kupitia mdomoni au kwa kuvuta pumzi.
Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 30, 2025 na nakala yake kuwekwa katika tovuti ya Mahakama ya TanzLii Jumamosi ya Aprili 3, 2025.
Upande wa mashtaka ulidai Julai 16,2022 katika eneo la Yombo Vituka wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alisababisha vifo vya pacha hao, Khalifa Ally “Doto” na Alif Ally “Kulwa” bila kukusudia kutokana na dawa aliyowapa.
Ushahidi wa Jamhuri ulikuwa unadai kuwa siku hiyo, pacha hao walikwenda kwa mshtakiwa ambaye alikuwa ni mganga wa jadi kwa ajili ya matibabu na baada ya kufika hapo aliwapa dawa fulani za tiba asili, ambazo walizinywa muda huo huo.
Baada ya kunywa, pacha hao walianza kujisikia vibaya na kuanza kutapika na kuharisha na baada ya kuona hali yao inakuwa mbaya, mmojawao (Alif), alimpigia simu rafiki yake aitwaye Malik Bahati na ndugu yao aitwaye Ally Athman Dilunga.
Waliwajulisha mahali walipo ambapo rafiki na ndugu yao huyo waliwafuata hadi nyumbani kwa mganga, ambapo walimkuta Khalifa akiwa katika hali mbaya ya kiafya na kuamua kuwawahisha Hospitali ya Aga Khan iliyopo eneo la Buza.
Aga Khan waliwapa rufaa kwenda hospitali ya Temeke na huko wakiwa kitengo cha wagonjwa wa dharura, madaktari waliwajulisha kuwa Khalifa alikuwa ameshapoteza maisha, Alif alilazwa lakini baadaye naye akapoteza maisha.
Shahidi wa tano, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Moses Mpongo aalieleza alivyomkamata mshitakiwa na kuwa uchunguzi wa sababu za kifo kwa pacha hao ulifanywa na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Ripoti ya madaktari hao wa Muhimbili ilieleza kifo cha pacha hao kilitokana na kukosa hewa kutokana sumu.
Vikasha vyenye sampuli za damu, mkojo, matapishi na unga wa dawa ambao marehemu walikunywa wakiwa kwa mshitakiwa, zilichukuliwa na kupelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
Ripoti ya uchambuzi ilionyesha kulikuwa na sumu katika dawa iliyokuwa katika mfumo wa poda na sumu hiyo kwa mujibu wa Mkemia mkuu ni “Aflatoxin G2” na “Citrinin_M-H”.
Mshitakiwa aliposomewa shitaka la mauaji ya kukusudia wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, alikanusha mashtaka hayo na kuulazimisha upande wa mashitaka kuita mashahidi saba na kuwasilisha vielelezo vitatu kuthibitisha shitaka hilo.
Jaji alisema ili Jamhuri ifanikishe kumtia hatiani mshitakiwa, kwanza ni lazima ithibitishe alitenda jambo au aliacha kutenda jambo kinyume na sheria na kwamba ni kitendo hicho kilisababisha kifo cha pacha hao.
Katika kufikia huko, Jaji alisema ataongozwa na hoja tatu, ya kwanza ni kama marehemu walikufa kifo cha kawaida, kama mshitakiwa ndiye alisababisha vifo hivyo na kama kulikuwa na dhamira ovu.
Uchambuzi wa Jaji
Katika uchambuzi wake, Jaji alisema hakuna ubishi kuwa pacha hao walifariki na kwamba ripoti ya shahidi wa 4, Braxeda Ogweyo ambaye ni mpatholojia, inaonyesha marehemu hao walikufa kutokana na kukosa oksijeni kulikosababishwa na kuvuta sumu.
Kwa ushahidi huo, Jaji alisema hiyo inaonyesha marehemu hawakufa kifo cha asili.
Kuhusu hoja ya pili kama ni mshitakiwa ndiye alisababisha vifo hivyo, Jaji alisema hakuna shahidi wa Jamhuri aliyeshuhudia mshtakiwa akiwapa dawa hiyo, bali ushahidi ni wa mazingira na pia uliegemea maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa.
Maelezo ya onyo ya mshtakiwa yaliyoandikwa na shahidi wa saba, stesheni Sajini Moses, yalikataliwa na mshtakiwa katika usikilizwaji wa kesi, akisema hakuwahi kuandika maelezo lakini ubishi ukaamuliwakuwa aliandika, baada ya kesi ndani ya kesi.
Jaji alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili katika kesi ndani ya kesi alibaini kuwa pingamizi la mshtakiwa halikuwa na msingi kwani katika maelezo hayo anaeleza hatua kwa hatua tukio lilivyotokea na kuna taarifa binafsi za familia.
Maelezo ya mshitakiwa
Katika maelezo hayo, ambayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo cha upande wa mashitaka, mshitakiwa anaeleza kuwa siku ya tukio, walifika kwake vijana wawili ambao ni pacha na kumweleza kuwa alienda kupata tiba.
“Wote wawili waliniambia kuwa wanabanwa na kifua na kuwa wanakandamizwa usiku na wanaona vitu vya ajabu, hivyo nilianza kuwatibu kwa kuwapa dawa inaitwa mkarakata, ambayo inatibu maradhi mbalimbali,”alieleza.
“Dawa hiyo ni mizizi iliyosagwa niliwawekea kwenye maji na kabla sijawapa, mimi nilionja ndipo niliwapa wote wawili wanywe. Walipokunywa dawa hiyo baada ya dakika kumi wakataka kwenda chooni kujisaidia.
“Wakarudi na kunieleza kuwa wanajisaidia kinyesi cha njano, kitu ambacho si cha kawaida. Nilipoona hali hiyo nilikoroga sukari na kuwapa wanywe. Baada ya nusu saa walianza kutapika wakasema wamekabwa na kitu kooni hakitaki kutoka.”
“Mimi nikawapa maji ya kawaida lakini hawakupata nafuu. Mmojawapo yule mkubwa akatoa macho huku akitetemeka na mwisho akadondoka na kuzimia. Baada ya kuona hivyo mmoja akapiga simu kwao,”anasema na kuongeza:-
“Hivyo ndugu zao walikuja tulishirikiana kuwapeleka hospitali... Tulipoenda hadi Temeke hospitali ndipo tuligundua kuwa yule mkubwa aliyeangukia kwangu amefariki,” anaeleza na Jaji akasema mshitakiwa alieleza nini kilitokea.
“Ninakubali kuwa katika maelezo hayo ya kukiri kutenda kosa, mshitakiwa alikiri mwenyewe kuwapokea pacha hao, kuwatibu na kwamba baadae walikufa. Kiukweli maelezo hayo yamebeba si kitu kingine zaidi ya ukweli,” alisema Jaji.
Jaji alisema ushahidi huo unaungwa mkono na ushahidi wa shahidi wa kwanza, Maliki Bahati ambaye ni rafiki na marehemu na pia ushahidi wa shahidi wa pili, Ally Dilunga ambaye ni ndugu wa marehemu ambao wote walieleza nini kilitokea.
Ni dawa ndiyo iliyowaua?
Jaji alisema baada ya kuthibitisha kuwa siku ya tukio, mshitakiwa aliwapa pacha dawa, hoja inayopaswa kupatiwa majibu na mahakama ni kama ni dawa hiyo aliyowapa ndio iliyosababisha vifo vya hao wawili?
Kulingana na Mpatholojia Ogweyo, wakati anachunguza sampuli za damu za marehemu hazikuonyesha chochote lakini sampuli nyingine kutoka polisi ambazo ni makasha ya dawa zilionyesha kulikuwa na sumu.
“Ilihitimishwa kuwa marehemu walikufa kutokana na kukosa hewa ya oksijeni kutokana na kula kitu chenye sumu, lakini shahidi wa sita, Rukia Hassan kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali alisema makasha matatu yalikuwa sumu.
Shahidi huyo kwa mujibu wa Jaji, alisema sumu hiyo aina ya Aflatoxin na Citrine ambazo zinapatikana katika mimea ya asili na huwa haina fungus, isipokuwa isipohifadhiwa vizuri inaweza kutengeneza sumu.
“Alisema sumu hizo zinaweza kusababisha kifo kwa kuimeza au kuivua. Zinaweza kuathiri mapafu na viungo vingine vya mwili kutegemea na kiwango cha sumu kilichomezwa,”alisema Jaji katika hukumu yake na kuongeza kuwa:-
“Ukitizama simulizi za wataalamu hao wawili, ninaona haijathibitishwa kwa viwango vinavyokubalika kuwa dawa ambayo marehemu walipewa ndio ilisababisha vifo vyao na nina sababu tatu katika kufikia hitimisho hilo.”
Sababu ya kwanza ni ushahidi wa shahidi wa saba kuwa walipokuwa wanachukua makasha ya dawa, mshitakiwa aliwaonyesha kasha moja kuwa ndio ilikuwa na dawa aliyowapa marehemu, lakini yeye akaamua kuchukua na mengine.
“Kwa hiyo hakuna uhakika ni dawa ipi walipewa marehemu. Lakini pili ni hati ya ukamataji wa makasha hayo haikupokelewa mahakamani kama kielelezo.”
Jaji akaongeza: “Hata kama inaaminika makasha yenye sumu ndio dawa zile ambazo walipewa marehemu huwa ni za asili na hazina fungus, labda zinaweza kutengeneza fungus na kuwa sumu kama hazitahifadhiwa vizuri.”
“Sumu hizo zinaweza kusababisha kifo kama zitavutwa kwa pumzi au kumezwa kulingana na kiwango ambacho mtu ametumia. Lakini bado hakuna ushahidi kama ukitumia sumu hizo unaweza kufa ghafla kama ilivyotokea kwa pacha hao.”
Lakini Jaji akasema kulingana na maelezo ya kukiri kosa ya mshitakiwa na ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili ambao wana unasaba na marehemu, pacha hao walitumia dawa za mganga huyo kwa kumeza kupitia kinywani.
“Kinyume chake, ripoti ya daktari inasema sumu hiyo ilivutwa kwa pumzi. Hizi ni njia mbili tofauti, na hii inaashiria si dawa ambayo marehemu walipewa na mshitakiwa iliyowasababishia kifo,”alisema Jaji.
Ni kutokana na uchambuzi huo, Jaji alisema mahakama inafikia hitimisho kuwa si mshitakiwa aliyesababisha vifo vya pacha hao, hivyo anaachiwa huru kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia kutokana na kukosekana kwa ushahidi.