Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfungwa wa bangi aachiwa kwa kushtakiwa kwa sheria isiyokuwepo

Muktasari:

  • Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Manyara imesema mfungwa huyo alishtakiwa kwa kifungu cha sheria kisicho sahihi.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Manyara, Babati imetengua hukumu ya mfungwa aliyekuwa amehukumiwa kutumia kifungo cha miaka 30 jela, Abubakari Hussein kwa kosa la kukutwa na bangi, baada ya kuridhika kuwa alishtakiwa kwa sheria isiyokuwepo kulingana na kosa lililokuwa likimkabili.

Uamuzi huo umetolewa Novemba 23, 2023 na Jaji John Kahyoza kufuatia rufaa aliyoikata Abubakari mahakamani hapo dhidi ya adhabu hiyo aliyohukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro iliyoko Orkesumet, katika kesi ya jinai namba 16 ya mwaka 2022.

Jaji Kahyoza amefikia uamuzi huo akikubaliana na hoja zilizotolewa na Wakili wa Serikali Blandina Msawa, aliyemwakilisha mjibu rufaa Jamhuri (Serikali) ambaye aliunga mkono rufaa hiyo.

Katika hukumu yake hiyo ya rufaa ya jinai namba 100/2023, Jaji Kahyoza amesema kuwa kumbukumbu (za Mwenendo wa kesi ya msingi) zinatoa ushuhuda kuwa Abubakari alishtakiwa kwa kifungu cha sheria kisicho sahihi, kama alivyoeleza kwa usahihi, Wakili wa Serikali, Blandina.

Amesema kuwa Kifungu cha 11 (1) (d) cha Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) kilichotumika kumshtaki kama kinavyotajwa katika hati ya mashtaka kinaunda kosa linalohusiana na uzuiaji wa kilimo cha baadhi ya mimea.

Amsema kuwa kifungu cha 15(1) na (2) (c) ndicho kinachounda kosa la marufuku ya usafirishaji dawa za kulevya, ikiwemo bangi ambayo Abubakari alidaiwa kukutwa nayo misokoto 103 na kwamba makosa hayo mawili si madogo wala yanayohusiana.


Hivyo amesema kwamba katika mazingira hayo mrufani (Abubakari) asingeweza kutiwa hatiani kwa kosa lililokuwa linamkabili katika kesi ya msingi.

"Katika mazingira hayo, ushahidi uliotolewa katika kesi ya msingi haukuunga mkono shtaka. Matokeo yake mrufani alitiwa hatiani na kuadhibiwa isivyo sawa," amesema Jaji Kahyoza na kuamuru:

"Natengua hatia na ninatupilia mbali adhabu. Ninaamuru Abubakari Hussein aachiliwe mara moja kutoka gerezani, isipokuwa vinginevyo kama ataendelewa kushikiliwa kihalali.”

Katika kesi ya msingi Abubakari Hussein alishtakiwa kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi chini ya kifungu cha 11 (1) (d) cha DCEA, kama ilivyorekebishwa mwaka 2019.

Hivyo Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro ilimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifingo cha miaka 30 jela, lakini hakuridhika na adhabu hiyo, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu alibainisha sababu mbili za kupinga adhabu hiyo.

Katika sababu hizo ambazo Mahakama iliziunganisha na kufanya sababu moja, akidai kuwa Mahakama ya Wilaya ilikosea kumtia hatiania hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Abubakari alijiwakisha mwenyewe, hivyo alitoa fursa kwa Wakili wa Serikali, kujibu sababu zake rufaa, kama alivyoziwasilisha kwa maandishi bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Wakili Blandina aliieleza mahakama hiyo kuwa anaunga mkono rufaa hiyo kwa kuwa kwanza hati ya mashtaka ina kasoro, alibainisha kuwa mrufani (Abubakari) alishtakiwa kwa sheria isiyokuwepo.

Alieleza kuwa kwa kosa alilokuwa anakabiliwa nalo kifungu sahihi cha sheria ambacho alipaswa kushtakiwa nacho ni kifungu cha 15 (1) na (2) (C) cha DCEA na si kifungu cha 11(1) (d) kilichotajwa kwenye hati ya mashtaka.

Alifafanua kuwa kifungu cha 11(1) (d) kinazungumzia kosa la kukutwa na mimea iliyopigwa marufuku na kwamba kifungu cha 15 (1) na (2) (c) ndicho kinachozungumzia kosa la kukutwa/kusafirisha dawa za kulevya, ambo ndilo lilikuwa likimkabili mrufani huyo.

Pia wakili Blandina alieleza kuwa mnyororo wa utunzaji vielelezo vya misokoto 103 ya bangi aliyodaiwa kukutwa nayo Abubakari haukuwa na muunganiko.

Alibainisha kuwa shahidi wa kwanza upande wa mashtaka ambaye ni ofisa wa polisi aliyemkamata hakubainisha misokoto hiyo 103.

Aliongeza kwamba hata shahidi wa pili aliyepeleka vielelezo (misokoto hiyo ya bhangi) kwa Mkemia wa Serikali ( kwa uchunguzi) hakuelezwa kama vielelezo hivyo vilivyowasilishwa mahakamani ndivyo vilivyohodhiwa ( vilivyokamatwa) na shahidi wa kwanza wala kwamba ndivyo alivyokutwa navyo mrufani.

Vilevile Wakili Blandina alidai kuwa hapakuwa na shahidi huru (asiye askari) aliyeitwa mahakamani na upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake.

Abubakari hakuwa na cha kuongeza katika hoja hizo zilizotolewa na Wakili wa Serikali.