Mfumo wa kisasa wa kusimamia uwazi wa mawasiliano waipatia Serikali mabilioni

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba
Muktasari:
- Serikali yakusanya Sh93.66 bilioni kupitia mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu katika kipindi cha miaka mitano
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba amesema Sh93.66 bilioni ziliwasilishwa serikalini tangu mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) uanze kufanya kazi Oktoba 2013 hadi Septemba 2018.
Kupatikana kwa fedha hizo kunatokana na kubainika kwa chanzo kipya cha mapato yatokanayo na simu zinazoingia kutoka nje ya nchi kuja nchini.
Kilaba ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 18, 2019 katika hafla ya makabidhiano ya Mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) inayofanyika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA)
Amesema kabla ya kuwepo kwa mfumo huo, watoa huduma walikuwa wanalipwa na kampuni za nje senti ya dola 8 hadi 9 za Kimarekani kwa kila dakika ya maongezi ya simu zilizokuwa zinapigwa nchini lakini baada ya kusimikwa kwa TTMS sasa wanapata dola senti 10 za Kimarekani.
Amesema mfumo huo unatoa mauzo ya simu katika data, ujumbe mfupi wa maandishi pamoja na matumizi ya simu za sauti.
Amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewawezesha wao kufanya makadirio ya kodi stahiki kwa watoa huduma ili kuhakikisha mapato kwa Serikali yanaongezeka.
Alizitaja faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na kugundua simu za ulaghai na kuwezesha upatikanaji wa takwimu za mawasiliano ya simu yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
"Tutaweza kutambua mapato na takwimu za miamala ya fedha mtandaoni inayofanywa kila siku na kusimamia kwa ufanisi ubora wa huduma za mawasiliano na hivyo kuboresha viwango vya huduma hizo," alisema Kilaba.
Amesema pia mtambo huo utasaidia kutambua taarifa za laini ya simu na namba tambulishi za kifaa cha mawasiliano, kubaini na kufungia simu zenye namba tambulishi zilizonakiliwa.
"Namba moja ya laini ya simu haifanani na nyingine sasa zipo zile ambazo huwa zina kaririwa na wengine na kusababisha usumbufu hivyo tutaweza kuzibaini na kuzifungia," amesema Kilaba.
Amesema mapato yote ya watoa huduma za mawasiliano pamoja na kutoa takwimu zinazohusiana na matumizi ya huduma za mawasiliano ikiwemo simu za sauti, matumizi ya data, na jumbe fupi yataratibiwa na mfumo huo.
"Mfumo huu ulianza kufanya kazi rasmi tarehe 01 Oktoba 2013, unaweza pia kusimamia shughuli nyingi zaidi kutokana na mazingira na mabadiliko ya teknolojia mpya zinapotokeza," amesema Kilaba.