Mfanyabiashara wa madini, mwanaye wauawa kwa kupigwa na kitu kizito

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Marco Chilyaakati
Muktasari:
- Mfanyabiashara wa madini aliyetambuliwa kwa jina la Festo Marwa (55) na mtoto wake John Marwa wameuawa kikatili kwa kupigwa kichwani na kitu kizito chenye ncha kali.
Songea. Mfanyabiashara wa madini aliyetambuliwa kwa jina la Festo Marwa (55) na mtoto wake John Marwa wameuawa kikatili kwa kupigwa kichwani na kitu kizito chenye ncha kali.
Marwa na mwanawe ambao ni wakazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, wamekutwa na umauti wakiwa katika kitongoji cha Mkerema Kijiji cha Lilondo, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mauaji hayo jana Jumatano Agosti 30, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Marco Chilyaakati amesema John (mtoto) amekutwa na jeraha kubwa kichwani na uchunguzi wa awali unaonyesha kapigwa na kitu kizito chenye ncha kali kilichosababisha ubongo kutoka nje.
“Baada ya mauaji hayo, wauaji hao waliichukua miili yao na kuiweka kwenye gari la Marwa ambalo ni Jeep lenye namba za usajili T241 DSX kisha wakalisukuma gari hilo hadi kwenye korongo,” alidai kamanda huyo.
Amedai lengo la kulisukumia gari hilo korongoni ni kutaka ionekane kuwa walipata ajali.
Hata hivyo, Kamanda Chilyaakati amesema makachelo walipolikagua gari hilo halikuwa limepata ajali.
“Baada ya kufanya utafiti tumefanikiwa kumkamata dereva aliyekuwa akiliendesha lile gari aliyetuambia kuwa baada ya tukio wenzake walimsindikiza hadi kituo cha mafuta kusudi aende polisi akatoe taarifa kwamba kapata ajali,” alidai kamanda Chilyaakati.
Amedai ili kupoteza ushahidi, dereva huyo alipigwa na kitu chenye ncha kali mguuni ili naye aonekana kapata majeraha kwenye ajali hiyo ya kutengeneza.
Anadai baada ya kumhoji alimtaja mtuhumiwa mwingine ambaye naye ametiwa mbaroni akihusishwa na tukio hilo.
“Lakini tumebaini watuhumiwa hawa wote ni wakazi wa Kunduchi Dar es Salaam na wanafahamiana vizuri na marehemu Marwa na walisafiri naye Agosti 17, 2023 kuja Songea wakaenda mpaka Kijiji cha Amani Makolo kulikokuwa na machimbo ya Marwa,” amedai kamanda huyo.
Anasema Marwa alikuwa akimiliki vitalu 10 vya madini aina ya Safaya alivyoviwekeza kwa mwekezaji.
“Na huyu muuaji tumeambiwa ndiye aliyefanikisha kupatikana kwa mwekezaji huyo na ilitakiwa apatiwe asilimia 30 ya hisa katika mradi huo,” alidai kamanda huyo.
Amesema kwa kuwa kila kitu kilikuwa kinaratibiwa na huyo anayedaiwa kuwa muuaji, alimshauri Marwa waende Mbeya ambako kulikuwa na mazungumzo kuhusiana na madini na jana wangerejea.
“Walianza safari ya kurejea mgodini na walipofika Makambako, dereva aliyekuwa anawaendesha Marwa na mwanawe aliwaambia amechoka anahitaji kupumzika.”
“Lakini huyu aliyekuwa anamsadia Marwa shughuli zake za madini alimwambia yeye anashukia hapo na angekuja (Songea) na gari nyingine ambayo ni Toyota –IST,”amedai.
Hata hivyo, anadai walipomuhoji dereva huyo baada ya kuachana na mwenzao huyo kipi kilifuata, alisema kabla hajaondoka alimfuata tena dereva huyo na kumtaka waondoke kuelekea Songea na walipofika kitongoji cha Mkerema kata ya Wino Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, aliwasimamisha kisha akawafuta ndani ya gari ambako aliwabonda Marwa na mwanawe.
“Alituambia watu hao walikuwa tayari wameleweshwa dawa baada ya kudungwa sindano. Aliposema hivyo tulikagua gari na kweli tuligundua ndani ya gari waliyokuwamo kina Marwa kulikuwa na sindano ya dawa za kulevya iliyotumika kuwadunga walipokuwa wamepumzika Makambako,” alidai kamanda Chilyaakati.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwashikilia watu hao na linawasaka wengine huku akitoa wito kwa ndugu wa marehemu hao kufika Songea kwa ajili ya kutambua miili ambayo imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Songea.
Aidha, Kamanda Chilyaakati ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na uhalifu wa aina yoyote kuwa hawako salama watanaswa muda wowote.