Prime
Mfahamu Dk Alicia Massenga Mkurugenzi mpya wa Bugando

Muktasari:
- Dk Massenga ambaye pia ni mtawa (Sister) wa Kanisa Katoliki, ana zaidi ya machapisho 19 katika majarida ya kisayansi, yanayogusa maeneo kama tiba salama ya watoto, matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea (antibiotiki), na changamoto za huduma za dharura kwa watoto wachanga.
Mwanza. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limemteua Dk Alicia Massenga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, iliyopo jijini Mwanza.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu, Juni 23, 2025 na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Bahati Wajanga imesema Dk Alicia ataanza majukumu yake leo.
"Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa amemteua Dk Sr. Alicia Massenga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kuanzia Tarehe 23/06/2025," imeeleza taarifa hiyo.
Huyu ndiye Dk Massenga
Kabla ya uteuzi huo, Dk Massenga amewahi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji katika hospitali hiyo.
Pia, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika idara ya upasuaji wa jumla katika Chuo cha Tiba cha Bugando.

Baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa huduma za upasuaji akisimamia idara zaidi ya 12 nafasi aliyoihudumu hadi uteuzi wa sasa kama Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo.
Idara hizo ni idara ya Urolojia, idara ya masikio, pua na koo (ENT), idara ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, idara ya upasuaji wa moyo na kifua, idara ya usingizi na huduma za wagonjwa mahututi, idara ya macho.
Idara nyingine ni ya upasuaji wa jumla, idara ya mifupa (Orthopedic Surgery), idara ya meno (Dental Surgery), idara ya upasuaji wa ngozi na urekebishaji maumbile (Plastic and Reconstructive Surgery), idara ya magonjwa ya wanawake na uzazi na idara ya upasuaji wa watoto.
Dk Massenga ni miongoni mwa madaktari wa kwanza wa upasuaji wa watoto waliomaliza mafunzo yao kwa msaada wa ufadhili kutoka shirika la Kids Operating Room.

Baada ya mafunzo hayo ya kimataifa Dk Massenga alipata ujuzi wa hali ya juu katika upasuaji wa watoto, jambo lililomwezesha kuanzisha kitengo cha kwanza cha upasuaji wa watoto kilichowekewa vifaa maalum katika hospitali hiyo ya rufaa kwa Kanda ya Ziwa.
Mbali na jukumu lake la kuongoza idara ya upasuaji, Dk Massenga amekuwa mstari wa mbele katika kuratibu kambi za upasuaji zinazohusisha wataalamu kutoka hospitali mbalimbali, likiwemo ya Muhimbili.
Utaalamu wake pia umechangiwa na kazi za utafiti, akiwa na zaidi ya machapisho 19 katika majarida ya kisayansi, yanayogusa maeneo kama tiba salama ya watoto, matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea (antibiotiki), na changamoto za huduma za dharura kwa watoto wachanga.
Dk Massenga alihakikisha anasimamia timu ya madaktari bingwa na wauguzi waliobobea katika idara ya upasuaji, sasa ni kiungo muhimu kati ya Serikali, Kanisa Katoliki (TEC), wafanyakazi, wagonjwa na jamii kwa ujumla.
Akitakiwa kuhakikisha kuwa hospitali hiyo inatoa huduma bora, endelevu na zenye viwango vya kimataifa.
Akizungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina, mmoja wa madaktari bingwa katika hospitali hiyo amesema Dk Massenga anazidi kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wanaojitosa katika taaluma za kitabibu, zinazochukuliwa kuwa ngumu na za wanaume.
Amesema amethibitisha kuwa taaluma ya udaktari wa upasuaji ni uwanja unaofaa kwa yeyote mwenye dhamira na moyo wa kusaidia.