Meli yenye watalii 1,500 yatia nanga bandari ya Dar

Muktasari:
- Meli yenye watalii zaidi ya 1,500 kutoka Marekani imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na itakuwepo kwa kwa siku mbili kisha kuelekea Zanzibar.
Dar es Salaam. Meli ya kitalii ya Zaandam inayomilikiwa na Kampuni ya Holland America Line imewasili nchini asubuhi ya leo ikiwa na watalii 1060 ikiwa ni sehemu za safari za kitalii za meli hiyo.
Meli hiyo yenye wafanyakazi na wahudumu zaidi ya 500 ilianza safari yake siku 71 nchini Marekani katika jimbo la Florida na baada ya kuwasili Tanzania itaelekea Shelisheli.
Akizungumzia ujio wa meli hiyo leo Novemba 10, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Amos Nnko amesema itakuwepo nchini kwa siku nne ambapo Tanzania bara itakaa siku mbili katika bandari ya Dar es Salaam na visiwani Zanzibar itakaa siku mbili.
Nnko ameeleza kuwa ujio wa meli hiyo unachochea jitihada za kukuza utalii nchini na ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa katika kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania.
Amesema watalii hao kutoka Marekani wametembea katika nchi kadhaa na sasa ni zamu ya Tanzania ambapo pamoja na kwenda katika hifadhi ya Selous, watatembelea mji wa kihistoria Bagamoyo na kuzunguka jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mathew Antony amesema ni mafanikio kwa bandari hiyo kuendelea kupokea meli kubwa ikiwa ni matokeo ya uboreshaji wa miundombinu.
“Ilizoeleka bandari ya Dar tunahudumia meli za mizigo pekee, hata hizi za watalii tunahudumia na tunawata wadau wengine walete meli zao miundombinu ni mizuri na tunazidi kuboresha,” amesema Antony.
Mmoja wa watalii hao Roseline Richard ameeleza kuwa ilikuwa ndoto yake kubwa kutembelea barani Afrika na hatimaye amefika Tanzania nchi inayosifiwa kwa ukarimu.