Meli iliyobeba watalii 715 yatinga Dar

Meli ya kitalii ya Seabourn Sojourn iliyowasili jana Jumatatu Aprili 17, 2023 katika Bandari ya Dar es Salaam ikitokea Zanzibar ikiwa na watalii 715.
Dar es Salaam. Meli ya kitalii ya Seabourn Sojourn imewasili nchini asubuhi ya leo ikiwa na watalii 715 ikiwa ni mkakati maalum wa kuhakikisha Tanzania inavuka lengo la idadi ya watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni jitihada zilizofanywa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini kupitia filamu ya The Royal Tour.
Akizungumzia ujio wa meli hiyo leo Aprili 17, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Lily Fungamtama amesema ujio wa meli hiyo ni ushahidi tosha kuwa Filamu ya Royal Tour imeitangaza Tanzania Kimataifa huku akisizitiza kuwa Meli nyingi zaidi za watalii zinatarajiwa kuja nchini kwa siku za usoni.
" Tunajivunia ujio wa meli hii ikiwa ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza vivutio vilivyopo nchini kupitia Filamu ya The Royal Tour tunaahidi sisi kama Bodi ya Utalii Tanzania tutaendelea kufanya kazi usiku na mchana kutangaza nchi yetu" amesema Fungamtama
Amesema watalii hao mara baada ya kuwasili katika Bandari ya Dar es salaam wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Jiji ikiwemo Makumbusho ya Taifa, Kijiji cha Makumbusho, Soko la vinyago lililoko Mwenge na viwanja vya Mnazi Mmoja na kuitaja Tanzania kama nchi yenye fursa nyingi za utalii.
Aidha, watalii wengine mara baada ya kuwasili nchini wamepata fursa ya kwenda kutembelea Hifadhi za Taifa ya Serengeti na Ngorongoro

Amebainisha kuwa meli hiyo ilianza safari yake kutoka nchini Marekani ikiwa na raia wa mataifa mbalimbali ya Ulaya imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam ikitokea Zanzibar baada ya hapo itaelekea nchini Afrika Kusini.
Kwa upande wake muongoza watalii katika Kijiji cha Makumbusho, Zakia Kawambwa amesema kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii wanaotembelea kijiji hicho cha Makumbusho kwa lengo la kujifunza mila na utamaduni wa makabila mbalimbali yaliyoko hapa nchini
Mmoja wa watalii hao Burton Nadiolado ameeleza kuwa ilikuwa ndoto yake kubwa kutembelea barani Afrika na hatimaye amefika Tanzania nchi inayosifiwa kwa ukarimu.