MCL yazindua Kampeni ya The Citizen Rising Woman Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar"(SMZ), Mhandisi Zena Ahmed Said ambaye ndiyo mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni ya The Citizen Rising Woman Zanzibar, inayofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr.
Unguja. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imezindua kampeni ya kumuinua mwanamke ya The Citizen Rising Woman.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema baada ya kujitathimini, kampuni iliona kuna sehemu inapwaya upande wa Zanzibar na kuamua kupeleka nguvu.
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 25, 2024 katika Hotel ya Madnat huku mgeni rasmi akiwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Zena Said.

Machumu amesema kampeni hiyo imekuwa ikifanyika Tanzania bara na kutoa motisha kwa wanawake wanaofanya vitu vikubwa kwenye jamii hivyo kuamua kuipeleka Zanzibar.
Amesema lengo la kampeni hiyo ni kuchochea ushiriki wa wanawake na kuwafanya watoto wa kike washiriki katika mambi makubwa nchini.
"Tulipoanza kampeni hii mwaka 2021 tumefanya mambo mengi kwanza tumeandika hadithi mbalimbali za wanawake waliofanikiwa kimaisha hapa nchini," amesema Machumu.
Machumu amesema hadi sasa zimeshaandikwa hadithi 231 tangu kampeni hiyo ilipoanzishwa Februari 2, 2021.