Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchungaji Mpambichile ‘awachorea ramani’ waumini kufikia mafanikio 2025

Waumini wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Gabriel Kibaha mkoani Pwani wakiwa kwenye mkesha Wa Mwaka Mpya, Picha na Sanjito.Msafiri

Muktasari:

  • Mchungaji Mpambichile amesema mafanikio yanahitaji juhudi za makusudi huku akibainisha kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha ni msingi muhimu wa kufikia malengo aliyojiwekea kila mtu.

Kibaha. Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Gabriel, Kibaha Pwani, Exavia Mpambichile amewahamasisha waumini wake kuanza mwaka mpya wakiwa na malengo thabiti ya maendeleo, hasa katika sekta ya uchumi.

Akizungumza katika ibada ya mkesha wa mwaka mpya iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Januari Mosi, 2025 kwenye kanisa hilo, Mpambichile alisisitiza umuhimu wa kuwa na malengo ya kununua viwanja na kujenga nyumba za kuishi kama njia ya kujijengea mustakabali bora wa maisha.

Katika mahubiri yake, mchungaji huyo amesema mafanikio yanahitaji juhudi za makusudi huku

akibainisha kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha ni msingi muhimu wa kufikia malengo.

"Mafanikio hayaji kwa njia ya miujiza, bali hupatikana kupitia bidii na malengo madhubuti. Lazima pia tuwe na nidhamu katika matumizi ya fedha tunazozipata," alisisitiza.

Aidha, aliwahimiza waumini kuwekeza katika biashara halali na kutumia muda wao katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kupoteza muda katika mambo yasiyo na tija.

"Anza mwaka mpya kwa kuweka malengo. Usikubali kukaa kwenye nyumba za kupanga miaka yote, nunua hata kipande kidogo cha ardhi na uanze ujenzi hatua kwa hatua. Safari ya mafanikio ni ya hatua moja baada ya nyingine," alisema.

Mchungaji Mpambichile pia alikazia umuhimu wa kuwa na nidhamu ya lugha na kauli njema kwa watu wengine, akisema kuwa ni msingi wa mafanikio katika maisha ya kila siku.

"Kauli njema huleta amani na mafanikio. Tukitumia lugha nzuri, tutavutia fadhila na kushirikiana vyema katika safari ya maisha," alisema.

Katika mahubiri hayo, alitoa wito pia kwa wazazi kuimarisha mshikamano na kuongeza upendo ndani ya familia zao ili kujenga msingi wa kuishi kwa kufuata maadili.

"Familia zenye mshikamano, umoja, upendo na kumcha Mungu, zina uwezo wa kutatua changamoto na kufanikisha malengo yao kwa pamoja," alisema.

Wakizungumza kanisani hapo, baadhi ya waamini wamekiri kuwa mahubiri yaliyotolewa yanatoa mwanga wa namna ya kukabiliana na changamoto za maisha kwa mtazamo wa maendeleo.

"Mahubiri ya Mchungaji yametufundisha umuhimu wa kuweka malengo na kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha yetu," alisema Samuel Mwegoha, mmoja wa waumini hao.

Naye Neema Masawe alisema mahubiri hayo yanafungua njia ya namna mtu anavyoweza  kukabiliana na changamoto za kila siku.

"Ibada hii imenifunza kuweka malengo na kuwa na nidhamu katika kila hatua ya maisha yangu hapa duniani,” alisema Masawe.