Mbunge Kafulila ‘awasafisha’ maaskofu

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
Muktasari:
Katika sakata hilo Sh306 zilichotwa katika akaunti ya Escrow
Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ‘amewasafisha’ viongozi wa dini waliotajwa kupokea mgawo wa fedha za escrow, akisema kuwa hapakuwa na namna viongozi hao wangesaidia upatikanaji wa fedha hizo kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza jijini humo jana, Kafulila ambaye amelikomalia suala hilo, alisema kila akifikiria haoni sababu ya kuwatia hatiani viongozi watatu wa dini waliotajwa kwenye Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta escrow kuwa walipokea fedha hizo kwa nia mbaya.
Akiwasilisha ripoti hiyo bungeni hivi karibu, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini alipokea Sh80.5 milioni, Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimanye Simon Sh40.4 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi hao walikiri kupokea fedha hizo wakieleza kwamba haikuwa mara ya kwanza kupewa msaada na Rugemalira.
Kafulila alisema kwa kuwa sifa ya rushwa ni kulenga kufanikisha jambo fulani na anaamini majaji na viongozi wengine serikalini, wana nafasi ya kutumia nyadhifa zao kufanikisha uchotaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu.
“Kuna baadhi ya vigogo walihusika, mahakama, mawaziri, wabunge kwa namna moja au nyingine kwa mamlaka zao wanaweza kusaidia kupatikana kwa fedha hizo. Askofu anasaidiaje hela itoke?” alihoji na kufafanua kuwa anaamini walipewa fedha kwa sababu binafsi.
Aliongeza: “Hoja yangu kubwa ni hela imetokaje Benki Kuu?”
Kafulila alisema hata kama Benki ya Mkombozi inamilikiwa na Kanisa Katoliki, bado haoni sababu ya kuwa na shaka nao kwa kuwa wao kama wafanyabiashara wasingeweza kukataa kupokea fedha.
“Benki inaona faida mtu akienda kuweka fedha kwake kwa hiyo isingeweza kukataa fedha hizo vinginevyo sheria iwe imevunjwa,” alisema.
Alisema hivi karibuni, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP), Harbinder Singh Sethi Singht alikwenda katika makanisa kadhaa jijini Dar es Salaam kutoka mchango kwa kutumia fedha zinazolalamikiwa kuchotwa kwenye akaunti ya escrow.
“Lakini hatusemi fedha hizo ni haramu. Akimpa Kafulika ni ishu, akienda akatoa KKKT (Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania) au msikitini siyo ishu kwa sababu hakuna namna unaweza ukamwezesha Sethi katika madili yake,” alisema.