Mbunge alia michezo ya kamari kuathiri vijana

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 52 cha mkutano wa bunge la bajeti, jijini Dodoma leo Juni 24, 2024. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Ahoji mpango wa Serikali wa kuweka sheria kali zaidi ili kuwabana wachezaji na kuzuia athari wanazozipata vijana.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asia Halamga amesema kuna changamoto kubwa ya uchezaji wa kamari katika makazi ya watu na imekuwa ikiathiri zaidi vijana.
“Ni upi mpango wa Serikali wa kuweka sheria kali zaidi, ili kuwabana wachezaji na kuweza kuzuia athari ambazo wanapata vijana, lakini pia na wananchi wengine kwenye makazi na kulijenga Taifa letu?” amehoji Asia katika swali lake la nyongeza aliloliuliza leo Juni 24,2024 bungeni jijini Dodoma.
Pia Asia amesema kuna changamoto ya uraibu imekuwa ikiendana na afya ya akili na kuhoji ni kiasi gani cha fedha kinatumika kusaidia huduma ya afya ya akili kwa Watanzania.
Baada ya maswali hilo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema michezo hiyo iko mitaani mwa wabunge na kuzitaka kamati za ulinzi na usalama mitaani kwao, wabunge, madiwani na vyombo vya dola kusaidia Serikali katika kupambana na changamoto hiyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema Serikali inapitia sheria yake mara kwa mara, ili kama kuna upungufu kufanyike marekebisho.
“Niwahakikishe mheshimiwa mbunge, hili linafanyiwa kazi siku hadi siku. Ni kweli baadhi ya vijana wanaweza kuingia katika uraibu na kupata changamoto ya afya ya akili, lakini Serikali imesimamia hilo na inaweka mafungu maalumu ya kutoa elimu kwa jamii, lakini hata kuongezea kipato katika sekta ya afya,” amesema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Ng’wasi Kamani amehoji Serikali ina mkakati gani wa kupambana na uraibu wa mchezo wa kamari unaoongezeka kwa kasi kwa vijana.
Akijibu swali hilo, Chande amesema pamoja na faida za kiuchumi zinazotokana na michezo ya kubahatisha, Serikali inatambua athari hasi katika jamii endapo haitaendeshwa kwa weledi.
Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 7(2) (i) cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha sura 41, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ina jukumu la kuhakikisha kuwa jamii inalindwa ipasavyo dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha.
Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, bodi imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia na kudhibiti athari hasi zitokanazo na michezo ya kubahatisha.
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuimarisha udhibiti na uratibu wa sekta kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa waendeshaji.
“Kuendelea kutoa elimu kwa jamii na wadau kuhusu athari hasi za michezo ya kubahatisha. Kutoa maelekezo na kusimamia utekelezaji wake kwa waendeshaji wa michezo ya kubahatisha kuhusu kuchukua hatua mbalimbali za kulinda jamii, ikiwemo kuwazuia wachezaji wanaobainika kuelekea katika uraibu,” amesema.
“Kusimamia utekelezaji wa sera ya watoa habari yenye lengo la kuishirikisha jamii kutoa taarifa kuhusiana na michezo ya kubahatisha, ikiwemo waendeshaji haramu, ushiriki wa watoto chini ya umri wa miaka 18, na ushiriki uliopitiliza,” amesema.