Michezo ya kubahatisha inavyotafuna fedha, fikra za vijana

Michezo ya kubahatisha imekua mtindo mpya wa maisha hususani kwa kundi kubwa la vijana hapa nchini.
Uzoefu unaonyesha vijana wengi wanaojihusisha na michezo hiyo ni lazima ‘abeti’ angalau mara moja kila siku ili kujiongezea nafasi ya kuibuka kuwa mshindi.
Ingawa michezo hiyo mengine imesajiliwa kisheria, lakini ni uraibu unaotafuna muda, kipato na fikra za vijana.
Michezo ya bahati nasibu ipo ya aina mbalimbali ambayo maarufu zaidi kwa hapa nchini ni ubashiri wa matokeo ya mpira wa miguu, lakini pia ipo kamari za mashine maarufu kama “gudugudu” na bahati nasibu za utumaji fedha ili kushinda zawadi fulani mfano gari, nyumba, bajaji na mengine.
Michezo hii inaendeshwa na kampuni za biashara, taasisi za kimichezo, lakini pia kwa sasa hata vyombo vya habari vimefuata mkondo huo kama njia mbadala ya kujitengenezea mapato.
Kwa mfano vituo vya televisheni na idhaa za redio zimekuwa na matangazo lukuki kila siku asubuhi hadi jioni kuhamasisha uchezaji bahati nasibu.
Hapa nchini jambo hili tayari limeteka kundi kubwa la vijana katika jamii, mfano wanafunzi wa vyuo vikuu, bodaboda, madereva na maelfu ya vijana washabiki wa mpira wa miguu ambao ni wanashiriki wakubwa katika michezo hiyo.
Uhalisia unaonyesha kwa wastani kila siku kijana ni lazima apate muda wa kutosha ili kuweza kutandika “mkeka wake” wa ushindi lakini pia apate muda wa ziada wa kufuatilia taarifa.
Ni lazima afuatilie vipindi vya redio, kujua ratiba za mechi, kufuatilia ligi mbalimbali duniani na kujua muundo wa ubashiri wake mfano “odds” ngapi zinatolewa ili aweze kujua thamani anayoweza kupata kabla ya kuamua kuweka fedha yake. Mtu mmoja anaweza kushiriki zaidi ya michezo mitano kwa siku.
Jambo hili linatafuna muda mwingi wa vijana na ikiwa endelevu mbeleni inaweza kutengeneza kundi la vijana ambao watakosa hamasa ya kufuatilia mambo muhimu ya kujifunza, au kuweka bidii katika kufanya shughuli za kiuzalishaji.
Athari yake ni kuwa inaweza kubadilisha mtindo wa maisha katika kundi la vijana kwa kufanya ubashiri kuwa kipaumbele chao na kuona kuwa ni mbadala wa changamoto zinazowakabili kimaisha mfano ukosefu wa ajira wakati si kweli.
Mwenendo huo pia umeingiza vijana katika uraibu wa kifikra kwa kudhani kuwa mafanikio ya kimaisha ikiwemo kumiliki mali yanaweza kuja kirahisi kwa njia ya michezo ya kubahatisha na kupata zawadi.
Uhalisia ulivyo ni kinyume chake, wanaoshiriki ndio wanatajirisha kampuni za ubashiri kwa kuzichangia mamilioni ya fedha kila uchwao na wao wanadokoa kiduchu katika hizo na kurejesha kwao kama kifuta jasho. Waendesha shughuli hizo hawana fedha za kutajirisha kila mtu.
Katika ukweli mwingine ambao pia hauzingatiwi ni kuwa jambo hilo linatafuna sehemu ya kipato cha vijana, mathalani kwa kiwango cha chini kijana anahitaji angalau Sh500 kwa siku ili kufanya ubashiri mzuri na kujiweka katika uwezekano wa kushinda ni lazima pia acheze kwa kurudiarudia.
Kiasi hicho kinaweza kuzidi ikiwa anashiriki katika michezo ya aina tofauti ya ubashiri.
Ingawa kuna faida za kiuchumi kwa nchi kutokana na michezo ya ubashiri kwa mfano zinazokusanywa kutoka katika michezo hiyo, au pia kampuni za michezo hiyo zimewekeza katika udhamini wa michezo na uendeshaji wa vilabu hususani katika mchezo wa mpira wa miguu.
Pia tujikumbushe kuwa matokeo yake upande wa pili si mazuri, kuna umuhimu wa kufikiria namna nzuri ya kuweza kudhibiti athari za jambo hilo kijamii.