Prime
Mbu 'Steve' janga jipya kwa malaria

Dar es Salaam. Uwekezaji wa miongo kadhaa katika sekta ya afya wa kupambana na malaria, unatajwa huenda ukaathiriwa na mbu aina ya Anopheles Stephensi ‘Steve’ anayeeneza ugonjwa huo kwa kasi barani Afrika.
Tanzania imeshaweka mikakati kadhaa ya kukabiliana na mbu huyo anayeeneza kwa kasi vimelea vya malaria.
‘Steve’ anatajwa kusababisha kuongezeka kwa maambukizi ya malaria Afrika, hivyo kuongeza wasiwasi kuhusu afya za watu.
Mbu huyo mwenye asili ya Asia Kusini, alitambuliwa kwa mara ya kwanza Djibouti mwaka 2012.
Tangu agunduliwe, Bara la Afrika limepata ongezeko kubwa la viwango vya malaria.
Machi mwaka jana, alitajwa kuonekana katika kaunti ndogo za Laisamis na Saku lakini hivi sasa ameenea katika nchi saba za Afrika ambazo ni Djibouti, Ethiopia, Sudan, Somalia, Kenya, Nigeria na Ghana.
Miezi kadhaa Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na aina hiyo ya mbu iwapo ataingia, huku ikiendelea na udhibiti kwa matumizi ya vyandarua, upuliziaji wa dawa na viuatilifu.
Kaimu Meneja, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria wa Wizara ya Afya, Dk Samwel Lazaro alisema bado hawajambaini mbu huyo kuingia nchini lakini wameongeza vituo vya ufuatiliaji.
“Wizara tuna tabia ya kufuatilia aina ya mbu tulionao, kuna vituo huwa tunafanya kazi kutengeneza aina ya mbu na tabia zake ili tuweze kutengeneza afua zetu kutokana na aina na tabia zake,” alisema Dk Lazaro.
Alisema baada ya kupata taarifa za uwepo wa mbu huyo kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka jana, wameendelea kukusanya mbu kwenye vituo vya zamani na kuongeza vingine vichache kwenye maeneo ambayo ni rahisi kupita ikiwamo kwenye ndege, meli na mipakani.
Mbali ya hilo, Dk Lazaro alisema Wizara ya Afya imeendesha mafunzo kwa waratibu wa wadudu dhurifu wa mikoa na halmashauri.
“Kuwafundisha kuhusu huyo mbu umbo lake na tabia zake ili katika kazi zao za kila siku kama yupo waweze kumbaini, lakini bado hatujambaini kuingia nchini. Djibouti, Ethiopia, Sudan, Somalia, Kenya, Nigeria na Ghana.” alisema Dk Lazaro.
Wakati kukiwa na tishio hilo mwaka 2023 WHO iligawa takribani dozi milioni 18 za chanjo kukinga watoto dhidi ya malaria Afrika, hata hivyo Tanzania si miongoni, ingawa watoto walitumika kufanikisha upatikanaji wa chanjo hiyo.
Mei 2023 Shirika la Uzalishaji Chanjo Duniani la Gavi Alliance lilitangaza kupatikana kwa chanjo dhidi ya malaria baada ya zaidi ya miaka 50 kuitafuta kwa majaribio.
Kwa mujibu wa mtafiti kiongozi kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk Ally Olotu, mwaka 2021 taasisi hiyo ilianza utafiti wa mwisho wa chanjo ya majaribio R21 kwa kuhusisha watoto 600 wa Kitanzania na wengine 4400 kutoka Kenya, Mali na Burkina Faso.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alipotafutwa na gazeti hili kufahamu ni lini Tanzania itaridhia chanjo hiyo ili kuwakinga watoto dhidi ya malaria alisema wanaendelea na mawasiliano na watengenezaji wa chanjo hiyo ili waweze kutuma taarifa zao, nchi iweze kuzisajili ili utaratibu huo ukishakamilika iweze kuendelea kuitumia pale panapohitajika.
“Chanjo yoyote kuingia nchini kuna utaratibu, kwanza ni lazima isajiliwe na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) baada ya kujiridhisha na usalama wake. Mpaka wiki mbili zilizopita watengenezaji wa chanjo hii bado walikuwa hawajazisajili,” alisema Profesa Nagu.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu katika sekta ya afya Januari 10, mwaka huu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema, “vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kufikia 1,340 mwaka 2023 kutoka vifo 1,533 mwaka 2022.”
WHO yatoa angalizo
Juzi, WHO kupitia mratibu wa magonjwa ya kitropiki Afrika, Dk Dorothy Achu ilisisitiza tishio linaloletwa na ‘Steve’ katika mazingira ya mijini, akipinga mikakati ya sasa ambayo kimsingi ilizingatia afua za ndani.
Alibainisha ugumu wa kugundua na kumuondoa mbu huyu mwenye uwezo wa kustahimili hali ya hewa, hivyo kutatiza juhudi za kupunguza athari zake kwa afya ya umma.
“Wakati mbu huyo akiendelea kuenea, maofisa wa afya wanakabiliana na hitaji la dharura la mikakati ya kibunifu kukabiliana na tishio hili linalojitokeza la kudhibiti malaria barani Afrika,” alisema Dk Achu.

Alisema Afrika inabeba sehemu kubwa isiyo na uwiano ya mzigo wa malaria duniani; kwa mwaka 2022 ilikuwa na asilimia 94 ya wagonjwa ulimwenguni na asilimia 95 ya vifo vilitoka Afrika.
“Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano walichangia asilimia 80 ya vifo hivi,” alisema Dk Achu.
Alisema mataifa kadhaa ya Afrika yanaendelea kutekeleza mipango ya kina ya kudhibiti malaria, kwa kutumia mchanganyiko wa hatua za kuzuia, zana za uchunguzi na afua za matibabu.
Kwa mujibu wa tafiti, mbu huyo hueneza vimelea kwa kasi na anazaliana kwa wingi ukilinganisha na mwingine.
Iwapo mtu ataugua anaweza kutibiwa lakini bado vimelea vikabaki kwenye ini, hivyo ugonjwa unaweza kuibuka wakati mwingine hata kama hakung’atwa na mbu.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Afya ya Mazingira na Ikolojia kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk Emmanuel Kaindoa alisema mbu huyo anapenda kuzaliana maeneo ya mijini zaidi ikilinganishwa na vijijini.
Alisema huzaliana katika mabaki ya vitu kama makontena, vifuu vya nazi, maji yalituama na kwenye mazingira machafu.
Pia, alimtaja kuwa ni mbu anayependa tabia za mbu wale wasioeneza malaria na tabia za mbu anayeeneza Dengue.
“Inaleta shida namna ya kuvitibu (vimelea), ni hatari sana na malaria yake ina tabia ya kujificha na kuwa ile ya ghafla,” alisema Dk Kaindoa.
“Tabia nyingine aliyonayo anaweza akala kwa binadamu na kwa viumbe vingine ambavyo si binadamu tabia inayomfanya awe tofauti lakini kwa tafiti zilizofanyika Misri na Djibout anaweza kueneza malaria kwa kiwango kikubwa.”
Kwa mujibu wa WHO, ‘Steve’ akichukua damu kwa binadamu hukaa siku tatu kisha hutaga mayai na siku ya nne hurudi tena kutafuta damu nyingine, hapo atamwambukiza mwingine na huishi kwa siku 30; na huenda na mzunguko huo mpaka anapokufa na hutaga mayai 300 kwa wakati mmoja.
‘Steve’ ni aina ya mbu ambaye hawezi kuuliwa na aina yoyote ya dawa ya viatilifu, kwa maana ya dawa ziwekwazo kwenye neti, za kupuliza na aina nyinginezo na hadhibitiwi na chanjo.
Novemba 2015, kikundi cha utafiti cha Marekani kiligundua mbu huyo aliye na mabadiliko ya kijeni kuwa, anaweza kupunguza uwezo wa kusambaza malaria.
Anopheles ambao ni mbu wanaoeneza malaria, wanapenda kutaga mayai kwenye maeneo yenye majimaji au karibu na kingo za mito na vijito.
Mbu jike hutaga yai moja baada ya jingine moja kwa moja kwenye maji. Mayai huelea juu ya uso wa maji; kwa mbu jike aliyekomaa hutaga mayai 50 hadi 200 kwa wakati mmoja.
Mbu jike aina ya Anopheles huwauma watu na wanyama; na hufanya hivyo jioni au usiku. Mbu jike huhitaji damu ili kuzalisha mayai.
Mbu jike aina ya Anopheles hupendelea kupata chakula kutoka kwa binadamu au wanyama kama vile ng’ombe.
Baadhi ya mbu dume aina ya Anopheles huruka katika makundi makubwa, kwa kawaida karibu na jioni, majike huruka katika makundi hayo ili kujamiiana.
Baada ya kunyonya damu, mbu jike hupumzika kwa siku chache huku damu ikiyeyushwa na mayai kukua. Baada ya mayai kukua, jike hutaga kwenye vyanzo vya maji.
Mbu aina ya Anopheles kwa jumla hawaruki zaidi ya maili 1.2 (kilomita mbili) kutoka kwenye makazi yao ya mabuu.
Mbu aina ya Anopheles huvutiwa na maeneo yenye giza na yenye vivuli wakati wa mchana kwa ajili ya kupumzika.