Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbowe na wenzake wana kesi ya kujibu

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewakuta Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu na kesi ya kujibu

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewakuta Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu na kesi ya kujibu katika kesi ya ugaidi inayowakabili.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Februari 18, 2022 na Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo zikiwa zimetimia siku 202 tangu kesi hiyo ianze.


Hatua hiyo inakuja baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake kwa kuwaita mahakamani mashahidi 13 kati ya 24 iliokuwa imepanga kuwaita, huku ikitoa vielelezo 39.


Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.


Tangu kesi hiyo ianze, imesikilizwa na majaji watatu; Elinaza Luvanda, Mustapher Siyani na Joachim Tiganga.


Kwa upande wa Jamhuri, mawakili ni Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Esther Martin, Tulimanywa Majige na Ignasi Mwinuka.


Upande wa utetezi wamekuwa na jumla ya mawakili 26 wakiongozwa na Peter Kibatala, baadhi yao ni Nashon Nkungu, John Mallya, Dickson Matata, Fredrick Kihwelo, Faraji Mangula, Sisty Aloyce, Michael Mwangasa, Gaston Garubindi, Seleman Matauka, Maria Mushi, Hadija Aron, Idd Msawanga.

Jumatano, Agosti 19, 2020 Halfan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Abdallah Ling’wenya walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa saba waliyodaiwa kuyatenda kati ya Mei 1 na Agosti 1, 2020.

Pia, walidaiwa kukutwa na silaha, vifaa vya milipuko, sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na dawa za kulevya aina ya heroin.

Usiku wa kuamkia Julai 21 2021, polisi waliwakamata watu 11 kwenye Hoteli ya Kingdom mjini Mwanza na siku iliyofuata walithibitisha kuwakamata viongozi 15 wa Chadema akiwamo mwenyekiti wao, Mbowe.


Soma hapa uamuzi wa kesi hiyo ulivyotolewa

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi tayari wamefikishwa Mahakamani.


Washtakiwa hao walipofika katika viwanja vya Mahakama wamelakiwa kwa shangwe na vifijo kutoka kwa wanachama na wafuasi wa Chadema na baada ya kushushwa kwenye gari wameingizwa katika mahabusu ya Mahakama kusubiri muda wa kusikiliza uamuzi.


Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameshaingia katika ukumbi wa mahakama kwa ajili ya kutoa uamuzi imwapo washtakaiwa hao wana kesi ya kujibu ama la.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando: Mheshimiwa Jaji shauri limekuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo. Sisi tuko tayari


Jaji: Utetezi?


Wakili Peter Kibatala: Nasi tupo tayari
Uamuzi mdogo katika kesi ya Mbowe na wenzake unakuja chini ya kifungu 41(1) cha sheria ya uhujumu uchumi na mahakama inatakiwa kuona kama wana kesi ya kujibu ama la.


Kabla ya uamuzi huo, mahakama itapitia ushahidi wote kuona kama kuna chochote kilicholetwa cha kuwafanya washtakiwa watakiwe kujitetea.


Kama mahakama itaona wana kesi ya kujibu, itawaeleza haki zao namna ya kujitetea na kama itaona hawana kesi ya kujibu, wataachiwa huru.


Sasa hivi Jaji Joachim Tiganga anarejea mashtaka yanayowakabili washtakiwa.


Jaji: Washtakiwa wote walikana mashtaka yote, lakini walikubali taarifa zao binafsi. Mshtakiwa wa kwanza mpaka wa tatu walikiri walikuwa askari wa Jeshi Kikosi cha Makomando na waliachishwa kwa sababu za kinidhamu.


Mshtakiwa wa nne, Mbowe alikiri ni Mwenyekiti wa Chadema, lakini mengine yote walikana, hivyo ni jukumu la upande wa mashtaka kuleta ushahidi kuthibitisha mashtaka haya.


Katika juhudi za kuthibitisha, upande wa mashtaka kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha sheria ya ushahidi, waliita jumla ya mashahidi 13.


Jaji: Mashahidi walitoa vielelezo 39 yakiwemo maelezo ya onyo ya washtakiwa, bastola na risasi na maganda yake na ripoti za miamala ya fedha.


Pia walitoa taatifa za usajili wa namba za simu za wateja, hati za ukamataji mali, hati za makabidhiano ya mali zilizokamatwa kwa washtakiwa,  ripoti ya uchunguzi wa kisayansi ya mawasiliano ya simu (kati ya mshtakiwa wa nne, Mbowe na shahidi wa 12, Luteni Urio), simu za washtakiwa na  za shahidi wa 12.


Upande wa utetezi waliingiza vielelezo vitano yakiwemo maelezo ya mashahidi watano wa upande wa mashtaka.


Katika hatua hii, jukumu la mahakama ni kupitia ushahidi kuona kama kesi ya upande wa mashtaka imetengenezeka, ili waweze kujitetea ama la.


Jaji: Mahamama ya Rufani katikamoja ya jukumu lake kuhusu suala hilo inasema: kwa uelewa wangu katika hatua hii mahakama inatakiwa kuangalia ushahidi kwa ujumla wake na si kupima uzito na kuaminika kwa mashahidi.


Nimetumia siku mbili kupitia ushahidi wote na vielelezo vyote vya upande wa mashtaka na vya utetezi. Baada ya kupitia hayo yote haya ndio maamuzi.


Naanza na shtaka la sita kwa mshtakiwa wa kwanza, Halfani Bwire Hassan la kukutwa na mali au vifaa vya kutekelezea vitendo vya kigaidi.


Jaji: Ushahidi ulioletwa ulikuwa ni vielelezo ambavyo ni sare za jeshi na mahakama ilikataa kuvipokea kwa sababu upande wa mashtaka ulikiuka misingi ya sheria wakati waikamata vielelezo hivyo.


Hivyo mahakama inaona hawakuleta ushahidi na mahakama inatamka mshtakiwa hana kesi ya kujibu.


Kifungu namba 20 cha sheria hiyo kinaelekeza penye upungufu kurudi kwenye sheria mama, kuona nini cha kufanya.


Baada ya mahakama kurejea kifungu namba 203 cha sheria ya uendeshaji mashtaka, kinachoeleza kama washtakiwa wanakiri ya kujibu itatamka wanaachiwa huru.


Hivyo mahakama inatamka kuwa mshtakiwa wa kwanza hana kesi ya kujibu na anaachiwa huru.


Mashtaka mengine mahakama imefanya uchunguzi imeona kwamba upo ushahidi ambao umeleta tuhumua kiasi cha kufanya kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu katika shtaka la kwanza hadi la tano.


Hivyo mahakama inaelekeza kuwa wanaweza kuleta utetezi wao na hata kuleta mashahidi au kukaa kimya.


Wakijitetea kwa kiapo, upande wa mashtaka utawahoji na wakikaa kimya, basi mahakama itaweza kuamua.
Hivyo, mahamama inawaalika washtakiwa waeleze ni kwa namna gani wataleta utetezi wao.


Wakili Jeremiah Mtobesya: Mheshimiwa Jaji tumepokea uamuzi ya mahakama kwamba mshtakiwa wa kwanza ana kesi ya kujibu kwenye kosa la kwanza, la pili na la nne, amenieleza atajitetea mwenyewe chini ya kiapo na anategemea kuita mashahidi wengine watano, hivyo yeye atakuwa ni wa sita.


Pia amenieleza katika kuleta utetezi atatoa vielelezo vitano.
Wakili John Mallya; Mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa kwa makosa aliyopatikana na kesi ya kujibu matatu ataleta ushahidi wake chini ya kiapo na mashahidi wawili pamoja na vielelezo vine.


Wakili Fredrick Kihwelu: Mshtakiwa wa tatu, Mohamed Ling'wenya atajitetea chini ya kiapo, atakuwa na mashshidi watano pamoja na vielelezo vitano:
Wakili Peter Kibatala; Mshtakiwa wa nne, Mbowe atajitetea kwa kiapo, ataleta mashshidi 10 na yeye wa 11 na ataleta vielelezo 20.


Baada ya hapa nafahamu kuwa mtanitaji nakala ya proceedings
Wakili wa Serikali Kidando: Mheshimiwa Jaji tulikuwa tunapitia Rule 15 (2) za Ecomonic procedure na inatakiwa pande zote mbili zitoe majina na anuani ya mashahidi pamoja na vielelezo.


Wakati wa usikilizwaji waliorodhesha mashahidi wane, lakini wakaomba wasi-desclose majina ya mashahidi wengine, sasa wanatakiwa waweke wazi.


Wakili wa Serikali Kidando: Hivyo tunaomba wenzetu wacomply hiyo kanuni kwa kutoa idadi na majina ya mashahidi na anuani zao na vielelezo ambavyo watavitumia.

Jaji Tiganga: Baada ya kupitia jalada, tarehe 10 Septemba ndio usikilizwaji wa awali ulifanyika, utetezi ukataja mashahidi saba ukaomba wanne Kibatala usiwataje.
Baada ya hapo ukaibuka ubishi, kwamba maombi hayo yalikuwa kwa sheria sahihi au hapana na jaji akatoa uamuzi kuwa hao wanne kama mahakama itaona washtakiwa wana kesi ya kujibu utalazimika kuwataja mashahidi.
Sasa kama hamtaki kuwataja mtalazimika kufuata utaratibu, kuleta maombi ya kutokuwataja mashahidi.

Jaji Tiganga ameingia tena mahakamani kwa ajili kuendelea na kesi, kiongozi wa jopo la mawakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala amesimama kwa ajili ya kueleza mahakama walichojadiliana baada ya kuomba dakika tano wakutane na wenzao wa upande wa mashtaka.

 Kibatala: Mheshimiwa Jaji, kama tulivyojadiliana tumeona majina ya mashahidi yateletwa siku ambayo washtakiwa wataanza kujitetea.

Na kwa kuwa tumezingatia proceeding za mahakama na nakala ya uamuzi itapatika ndani ya siku 7 kuanzia leo.

Hivyo, kama itawapendeza na wenzetu (upande wa mashtaka), tunaomba washtakiwa aanze kujitetea Machi 4, mwaka 2022.

Kidando: Mheshimiwa Jaji, hatuna pingamizi ya maombi ya washtakiwa kuanza kujitetea tarehe Machi 4, mwaka 2022.

Jaji: Maombi yamezingatiwa na washtakiwa wataanza kujitetea Machi 4, 2022. Proceeding zitakuwa tayari ndani ya siku saba na mtapatiwa Ijumaa ya wiki ijayo.

Jaji Tiganga: Naahirisha kesi hii hadi Machi 4, 2022, saa 3:00 asubuhi itakapoitwa kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea. Nawaelekeza washtakiwa watakuwa mahabusu chini ya usimamizi wa magereza. Niwatakie jioni njema.