Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu chafu magari ya wanafunzi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), imebainisha mchezo ambao umekuwa ukifanywa na wamiliki wa shule kupata leseni za magari ya kubeba wanafunzi zaidi ya uwezo wa gari husika.


Mtwara/Dar. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), imebainisha mchezo ambao umekuwa ukifanywa na wamiliki wa shule kupata leseni za magari ya kubeba wanafunzi zaidi ya uwezo wa gari husika.

Imesema wamiliki hao wamekuwa wakiongeza siti za magari kuliko zilizokuja na gari husika, kabla ya kwenda kuomba leseni ya usafirishaji, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi.

Latra imeeleza mchezo huo ikiwa ni siku moja imepita tangu gari la Shule ya Msingi ya King David aina ya hiace iliyokuwa imebeba wanafunzi zaidi ya 25 kupata ajali na kusababisha vifo 13, ikiwemo wanafunzi 11.

Ajali hiyo ilitokea juzi asubuhi eneo la Mjimwema, Kata ya Mikindani, Mtwara Mjini wakati gari hiyo ikitoka kuwachukua wanafunzi hao majumbani kuwapeleka shule. Baadhi ya waliofariki ni Johari na Emanuel Simon, ambao ni mtu na mdogo wake. Wengine ni Humaira Changu, Hajra Chibwana, Precious Benjamin, Warda False, Frida Richard Magoma na William Gideon Mrope wa Shule ya Msingi Singing aliyepewa lifti.

Waliojeruhiwa ni Mary Msigwa, Meghan Msigwa, Anifa Chibwaya, Basam Roberty, Loretta Ruzane, Mary Tarimo, Beanka Abdallah, Haisam Hintu, Hanson Evance, Yosophina Thobias, Nailance Juma na Said Ramadhan.

Baada ya ajali hiyo kutokea, kumekuwa na mjadala maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni juu ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaobebwa kwenye magari ya shule, ikiwamo baadhi yao kupakatana na wengine kusimama.

Wametolea mfano gari hiyo ya Shule ya King David ambayo ni hiace yenye uwezo wa kubeba wanafunzi si zaidi ya 15, lakini ilibeba zaidi ya 25 na ile ya Shule ya Luck Vicent iliyotokea mwaka 2017 na kuua wanafunzi 32 wakiwemo walimu.

Mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam, Andrew John alisema, “baadhi ya magari ya wanafunzi ni mabovu lakini yanajaza sana. Unaweza kuona watoto wamerundikana kwenye gari, hili limekuwa kawaida, sasa sijajua Serikali inachukua hatua gani, kwani ni hatari.”

Jana, gazeti hili lilizungumza kwa simu na Mkurugenzi wa Udhibiti na usafiri wa huduma za barabara wa Latra, Johansen Kahatano aliyesema kuwa kanuni zinawataka kubeba abiria kulingana na idadi ya viti vilivyopo. Ni kosa kubeba zaidi ya viti vilivyopo ambavyo ndio kipimo cha uwezo wa gari.

Alipoulizwa kuwepo kwa baadhi ya magari kubeba wanafunzi wengi kuliko idadi ya viti, Kahatano alisema, “Ni kweli tumekutana na kesi za mabasi, yakiwamo ya shule.”

Wakati Kahatano akieleza hayo, Mwenyekiti wa Dawati la Sera la Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Konya alisema leseni inaeleza kila mwanafunzi anapaswa kukaa kwenye kiti afike shule na nyumbani akiwa hajachoka. Alisema kama ni gari ndogo hiace inapaswa kubeba watoto 12 ni hao hao tu, “kwa sasa hali imekuwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Sababu ni gharama za uendeshaji zimekuwa kubwa. Kodi zimekuwa kubwa mno, wakati kazi tunayoifanya ni sehemu ya jamii ya Watanzania.”

Konya alitolea mfano wa agizo walilopewa la kila gari la shule kuweka namba za gari zenye rangi nyeupe. “Hali hii inatufanya kulipia kama gari la biashara daladalada, lakini unajua mwanafunzi kwenye daladala analipa Sh200.

“Kutokana na makodi kuwa mengi, ndio utaona bora warundikwe, kwani ukisema uongeze ada wazazi hawatalipa na ndio hao hao watumishi wa umma ambao nyongeza ya mishahara ndio hiyo tumeona ni Sh20,000,” alisema.

Konya, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho alilitaja jambo lingine linalosababisha ajali hizo ni gharama kuwa kubwa za uendeshaji wa shule zikiwamo za kodi, hivyo kushindwa kufanyia magari matengenezo ya mara kwa mara.


Waagwa, wasafirishwa

Miili mingine miwili ya Johari (7) na Emmanuel Simon (5) ambao ni mtu na mdogo wake jana iliagwa katika Kanisa Anglikana mjini Mtwara na kusafirishwa kwenda Mvumi, mkoani Dodoma kwa mazishi.

Juzi, Stella Yohanna ambaye ni mama wa watoto hao alisema kauli ya mwisho ya watoto wake kabla ya kwenda shule walisema “Bye dady, bye mamy” (kwa heri baba, kwa heri mama) ambayo walikuwa wanawaaga wazazi wakati wakiondoka kwenda shuleni. Kwa upande wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Clemence alisema wanafunzi saba kati ya 17 waliojeruhiwa katika ajali hiyo wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam na Hospitali ya Rufaa Ndanda, wilayani Masasi kwa matibabu zaidi na majeruhi 10 wanaendelea vizuri hospitalini hapo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema: “Nimetembelea majeruhi na kuwajulia hali, wapo wanaoendelea vizuri na matibabu na wengine wameenda kwenye uchunguzi zaidi katika hospitali nyingine za rufaa, tuendelee kuwaombea ili warejee katika maisha yao ya kawaida”.

Kwa upande wake, mmiliki wa Shule ya King David, Alex Chibunu alisema ameendesha shule hiyo kwa miaka 19 magari yake hayajawahi kupata ajali.

“Huu kwetu ni msiba mkubwa, sisi hatuna uwezo wa kufanya lolote zaidi ya Mwenyezi Mungu kumuomba atutie nguvu katika kipindi hiki kigumu, kwa sasa vyombo vya usalama vinamshikilia mkurugenzi wa fedha na utawala ambaye pia ni meneja wa shule yetu, David Chibunu kwa upelelezi zaidi,” alisema.