Mbaroni kwa kukutwa na meno ya tembo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda akionesha meno ya Tembo aliyokutwa nayo Edson Mahmoud (44) akiyasafirisha kwa pikipiki.
Muktasari:
- Edson Mahmoud (44) mkazi wa wilaya ya Ngara anashikiliwa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali.
Kagera. Jeshi la Polisi mkoani Kagera linamshikilia mkazi wa kitongoji cha Kafua kilichopo wilaya ya Ngara, Edson Mahmoud (44) kwa tuhuma za kukutwa na meno ya tembo yanayokadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 12 aliyokuwa akiyasafirisha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Februari 25, 2024, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amesema kupitia taarifa fiche kutoka kwa wananchi, jeshi hilo liliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa pamoja na vielelezo hivyo.
“Hata hivyo watuhumiwa wenzake watatu walifanikiwa kutoroka baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa,” amesema.
Amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Februari 21, 2024 saa 4 asubuhi katika kijiji na kata ya Benako, wilaya ya Ngara akiwa na meno ya tembo vipande vitatu vinavyokadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 12.
“Nyara hizo za Serikali ambazo ni meno ya tembo alikuwa akizisafirisha kwenda kuziuza kwa kutumia usafiri wa pikipiki yenye namba za usajili MC 977 DSZ aina ya Bajaji Boxer,” amesema Kamanda Chatanda.
Ametoa onyo kwa watu wote wanaoendelea kujihusisha na njia haramu za kujipatia kipato kuacha mara moja akidai hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi watakapobainika, akiwataka wajitafutie kipato kihalali.