Hakimu akwamisha kesi ya kusafirisha vipande 413 ya meno ya tembo

File Photo
Muktasari:
- Washtakiwa wanne wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kukusanya, kununua, kuuza na kusafirisha vipande 413 vya meno na tembo na meno mawili ya kiboko yenye thamani ya zaidi ya Sh 4.4 bilioni
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kusafirisha vipande 413 vya meno ya tembo na meno mawili ya kiboko vyenye thamani ya zaidi ya Sh4.4bilioni, inayowakabili Hassan Shaban na wenzake watatu.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi, imeshindwa kuendelea mahakamani hapo kutokana na hakimu anayesikiliza shauri hilo, Evodia Kyaruzi kuteuliwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na kupangiwa majukumu mengine.
Mbali na Shabani, washtakiwa wengine ni Olivia Mchuwa, Haidari Sharifu na Joyce Thomas, wanaokabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge na kusafirisha nyara za Serikali bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori Nchini.
Leo Jumanne, Januari 2, 2024 Wakili wa Serikali, Winiwa Samson amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendea na usikilizwaji, lakini wakili anayeendesha kesi hiyo hayupo na pia hakimu anayesikiliza kesi hiyo naye hayupo, hivyo anaomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa huku wakisubiri kupangiwa hakimu mwingine.
Hakimu Lyamuya amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Januari 16, 2023.
Washtakiwa wapo rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo walitakiwa kwenda kuomba Mahakama Kuu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uharifu kwa kukusanya, kununua, kuuza na kusafirisha nyara za Serikali ambazo ni vipande 413 vya meno na tembo na meno mawili ya kiboko.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo Agosti 28, 2019 jijini Dar es Salaam, ambapo walikutwa na nyara hizo ambazo ni mali ya Serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh4.4 bilioni.