Mbakaji ajitafutia balaa, sasa kufia jela

Muktasari:
Desemba 11, 2014, Eliah ambaye ni fundi magari, mkazi wa Kijiji cha Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka minane.
Moshi. Siku ya kufa nyani miti yote huteleza, hii ndiyo hali iliyomkuta mfungwa aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 kwa ubakaji, Eliah Bariki (22) baada ya rufaa yake kugonga mwamba na kufungwa jela maisha.
Desemba 11, 2014, Eliah ambaye ni fundi magari, mkazi wa Kijiji cha Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka minane.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Wilaya ya Rombo baada ya kupatikana na hatia ya kutenda kosa hilo Agosti 7, 2013, wakati akijua ni la jinai.
Hata hivyo, Eliah hakuridhika na kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, akipinga kutiwa hatiani na kuhukumiwa miaka 30 jela akisema Hakimu alikosea.