MAWAIDHA: Misingi ya amani ya kweli katika Uislamu

Kwa mujibu wa Uislamu, amani ni dhana pana katika maisha ya mwanadamu. Amani ya kweli ya mwanadamu katika Uislamu hujengwa kupitia malengo yake makuu matano (maqasid as-shari‘ah) ambayo ni; Mosi, amani ya nafsi dhidi ya kuuawa, kushambuliwa, au kudhoofishwa na maradhi.
Pili, amani ya heshima ya mwanadamu na kila kinachohusiana na familia yake na watoto wake. Tatu, amani ya mali yake dhidi ya wizi, dhuluma na uporaji wa ardhi au haki zake.
Nne, amani ya dini yake, dhidi ya fitina, ukandamizaji au kupokwa uhuru wake wa kiimani na kiibada. Tano, amani ya akili yake, dhidi ya uvizaji, uhuru wake wa kufikiri na kutoa maoni.
Neno amani limetajwa sehemu nyingi katika Qur’an Tukufu, miongoni mwa sehemu hizo ni kauli yake Allah Mtukufu:
‘’Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua? Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma, hao ndio watakaopata amani na wao ndio walioongoka” (6:81-82).
Amani katika Uislamu imegawanyika katika aina mbili: Mosi, amani halisi. Hii ni amani ya kweli na ya kudumu, ambapo hakuna tishio lolote linalomhofisha mwanadamu. Mfano wa amani hii imeelezwa katika Qur’an: “Ewe Musa! Njoo mbele wala usiogope. Hakika wewe ni miongoni mwa waliosalimika” (28:31). Pili, amani ya dhahania (kufikirika). Hii ni amani ya bandia iliyojengwa juu ya misingi ya kiburi, udikteta, uonevu, dhuluma, uongo na kutotambua hatari halisi.
Mtu hujihisi yuko salama kwa misingi isiyo ya kweli. Amani hii bandia imeelezwa katika Qur’an: “Je, watu wa miji walijiamini kuwa adhabu yetu haitawajia usiku wakiwa wamelala?” (7: 97)
Muumini kwa mujibu wa itikadi ni yule anayemuamini Allah, mitume wake, vitabu vyake, malaika, Siku ya Mwisho na Qadari (maamuzi ya Allah) kuhusu kheri na shari.
Na Muumini kwa mujibu wa mwenendo wake katika jamii, ni mtu mwaminifu, anayehifadhi na kuheshimu damu na mali za watu wengine.
Mtume wa Allah amesema katika Hotuba ya Hijja ya Kuaga: “Je, nikujulisheni muumini ni nani? Ni yule ambaye watu wanajihisi salama (kupitia yeye) kwa mali zao na nafsi zao.” (Musnad Ahmad: 23958).
Amani ya familia inategemea mambo mengi yaliyo ndani na nje, ambayo yanatengeneza mazingira salama kwa kila mmoja katika wanafamilia. Kwa mujibu wa maandiko ya Kiislamu, kuna mihimili minne ya kimaadili inayochangia moja kwa moja katika kujenga usalama na amani ndani ya familia.
Mihimili hiyo ni; moyo wa kupendana (mawadda), huruma (rahma), upole (rifq) na maadili mema (ḥusn al-adab). Nyumba yoyote ambayo haijajengwa juu ya mojawapo ya mihimili hii, ipo hatarini kusambaratika uhusiano wake, jambo ambalo huathiri usalama na uthabiti wa familia.
Qur’an inasema: “Na miongoni mwa ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake kutoka nafsi zenu ili mpate utulivu kwao, naye ameweka baina yenu mapenzi na huruma.” (30: 21)
Amani ya ajira inajengwa juu ya nguzo mbili kuu; ambazo ni uaminifu na ufanisi katika kazi. Uaminifu wa mfanyakazi ni chanzo cha amani kwa mwajiri, na ufanisi wa kazi ni njia ya kujihakikishia uthabiti wa ajira hata nyongeza ya kipato.
Mtume wa Allah anasema: “Hakika ardhi ya Mashariki na Magharibi itafunguliwa kwenu, na hakika watendaji wake watakuwa motoni, isipokuwa mchaji Allah na mkweli katika uaminifu.” (Musnad Ahmad: 22599)
Katika Uislamu, amani ya kijamii si jukumu la Serikali pekee, bali ni la kila mtu. Kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu kwa kuwa na huruma, tabia njema, moyo wa kusaidia bila ubaguzi. Mtume wa Allah anasema:
“Hakuna yeyote miongoni mwenu atakayeingia peponi isipokuwa mwenye huruma.” Masahaba wakamuuliza: Ewe Mtume wa Allah! Sisi sote tuna huruma. Akasema: “Siyo huruma ya mtu kwa nafsi yake na familia yake, bali ni huruma kwa watu wote.”
Allah Mtukufu ameumba ardhi na kuweka alama ili kuwaongoza wasafiri. Mtume alionya vikali kuhusu kubadilisha au kuharibu alama za barabarani ambazo watu huzitumia kuelekea katika miji yao, nyumba zao na shughuli zao za kila siku.
Mtume wa Allah anasema: “Allah amemlaani mtu yeyote anayebadilisha alama za ardhi.” (Muslim: 1978). Laana hii inawahusu wote wanaoondoa na kuharibu alama hizo.
Amani ya nchi, miji, vijiji na mataifa ni mstari mwekundu katika Uislamu. Hairuhusiwi kwa mtu au kikundi chochote kuwatisha raia au kuwashambulia kwa silaha, bila kujali hali au sababu.
Mtume wa Allah alimwambia Ali (Allah Amridhie): “Kutakuwa na mtafaruku au jambo baada yangu. Ikiwa utaweza kuwa mtu wa amani basi fanya hivyo.” (Musnad Ahmad: 2/85).