Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi holela ya viuatilifu, ubovu wa masoko watishia usalama wa chakula

Mchumi Idara ya Viwanda vidogo na biashara ndogo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Denis Kagombora akizungumza wakati wa warsha ya kuwajengea uwezo madiwani na wakurugenzi wa halmashauri za Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza kuhusu usalama wa chakula. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

  • Chakula kisicho salama kinatajwa kusababisha madhara mbalimbali kwa binadamu ikiwemo uvimbe na Kansa, kuharibiwa kwa ufahamu na ubongo, kuharibika mfumo wa uzazi, viungo vya ndani kuharibika ikiwemo in kuungua, figo na mapafu kushindwa kufanya kazi.

Mwanza. Matumizi holela ya viuatilifu, masoko yenye miundombinu mibovu na uhifadhi usio salama wa chakula vimetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazohatarisha usalama wa chakula nchini, hali inayoweza kusababisha magonjwa kama saratani, matatizo ya uzazi na uharibifu wa viungo vya ndani vya mwili.

Utafiti wa tathmini ya miezi mitatu (Julai - Oktoba 2024) uliofanywa katika mikoa 10 nchini, umebaini kuwa masoko mengi hayana mpangilio mzuri, yana idadi kubwa ya watu kuliko uwezo wake, na taka hutupwa kiholela, hali inayoongeza hatari ya usalama wa chakula.

Matokeo ya tathmini hiyo, yaliyowasilishwa Machi 18, 2025, kwa madiwani na wakurugenzi wa halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela, yalitolewa na Mchumi wa Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Denis Kagombora.

"Kuna matumizi mabaya ya viuatilifu; wakulima wanapulizia dawa na ndani ya siku moja au siku hiyo hiyo bidhaa zinaingia sokoni, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu," amesema Kagombora.

Amesisitiza kuwa ni jukumu la madiwani na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha elimu ya usalama wa chakula inawafikia wananchi na kutungwa kwa sheria ndogo zitakazosaidia usimamizi wa chakula.

"Tunatarajia halmashauri, kwa kushirikiana na baraza la madiwani, zitunge sheria ndogo zitakazosaidia katika usimamizi wa chakula kwa sababu madiwani wako karibu na jamii ambayo inauza na kutumia chakula hicho," amesema Kagombora.

Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Kisera kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kuboresha Lishe (GAIN), Laetitia William, amesema kuwa miundombinu duni husababisha ulaji wa chakula kisicho salama, hali inayoweza kusababisha magonjwa yasiyoambukiza na kuathiri ukuaji wa mwili na ubongo.

"Miundombinu ikiwa duni, tunapata chakula kisicho salama. Madiwani wanapaswa kuzingatia usalama wa chakula wanapotunga kanuni ili kuwezesha maafisa lishe kufanya kazi zao kwa ufanisi na kulinda afya za wananchi," amesema Laetitia.


Siasa na changamoto ya usimamizi

Hata hivyo, baadhi ya madiwani wamesema changamoto kubwa ni mazingira ya kisiasa, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha, amesema baadhi ya madiwani wamekuwa wazito kusimamia sheria za usalama wa chakula kwa kuhofia kuwakera wananchi na kupoteza kura.

"Tuna miezi michache kuelekea uchaguzi, madiwani wanaogopa kupingana na ilani ya chama. Mimi nitakuwa upande wa wananchi kwa sababu nahitaji kura zao. Wataalamu fanyeni kazi yenu, lakini mheshimu sheria, nendeni polepole," amesema Kotecha.

Diwani wa Sangabuye, Manispaa ya Ilemela, Renatus Mlunga, amesema kuwa usimamizi wa usalama wa chakula unasuasua kutokana na upungufu wa wataalamu wa serikali, hali inayosababisha maeneo mengi kutofikiwa kwa elimu ya usalama wa chakula.

"Mbolea za viwandani zinaathiri ardhi yetu. Tuiombe Serikali itafute njia mbadala ili wakulima waachane na mbolea zenye kemikali na kurejea matumizi ya mbolea ya asili kama samadi," amesema Mlunga.

Naye Ofisa Kilimo wa Manispaa ya Ilemela, James Wembe, ameshauri kuwa chakula kibaya kitupwe badala ya kupelekwa sokoni.

"Mfanyabiashara naye hawezi kujua mtoto wake atakutana nacho wapi. Hebu tutimize wajibu wetu, tusizungumzie tu suala hili na kuliacha hapa, bali tuwape elimu sahihi," amesema Wembe.