Matukio 1,100 ya ukaliti wa kijinsia yaripotiwa Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda (katikati) akizungumza jambo katika uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili mkoani Mtwara. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Zaidi ya matukio 1,100 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa kutokea mkoani Mtwara yakiwemo 648 yanayohusu watoto, katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu, huku mila na desturi zikitajwa kuchangia baadhi ya matukio.
Mtwara. Zaidi ya matukio 1,100 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa kutokea mkoani hapa katika kipindi cha Januari - Septemba mwaka huu, ambapo kati ya hayo, matukio 648 yanahusu watoto pekee.
Akizungumza Novemba 25, 2023 Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili amesema kuwa watoto 648 walifanyiwa ukatili ndani ya jamii, yaliyohusisha watoto wa kike yakiwa 400 jambo linatishia usalama wao.
Amesema kuwa kama wadau wanapaswa kupaza sauti kukemea matukio ya ukatili na pale wanapoona viashiria vya ukatili ili kuzuia yasitokee.
“Unajua kitendo cha kuwa na matukio mengi yanayohusu watoto sio ishara nzuri kwetu kama wazazi na walezi, ina maana matukio 648 yote yanahusu watoto lakini kati ya hayo matukio 400 yanahusu watoto wa kike, yaani hapo utaona wamama watarajiwa wanavyofanyiwa ukatili wa kijinsia, tujitafakari,” amesema Munkunda na kuongeza;
“Lazima tujiulize ni kwa nini ukatili wa kijinsia, unatokea ni wapi na maeneo gani ambayo ni hatarishi, na na nini washiriki wakubwa katika matukio haya hii itasaidia, na tutaweza kuisaidia jamii kuondoka na vitendo hivi vya ukatili.
Naye Mwakilishi kutoka Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Nakongo), Batazar Komba amesema kuwa jando na unyago zinahusishwa na ukatili wa kijinsia ambapo kupitia mafundisho wanayoyapata humo yamekuwa yakichangia mimba na ndoa nyingi za utotoni.
“Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Jinsia na Vijana kupitia Programu ya USAID Afya yangu, Rukia Mchika amesema kuwa ukatili wa kijinsia ni chanzo cha maambukizi ya Ukimwi na wajibu wetu ni kuhakiksha wanaotumia dawa, jamii haiwanyanyapai,”amesema.