Masoud Kipanya kumdai Mwijaku fidia ya Sh5 bilioni

Muktasari:

  • Wakili wa Masoud adai mteja wake amekashifiwa, kushushiwa heshima

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kusambaa taarifa zinazomuhusu Ali Masoud 'Masoud Kipanya' kwenye mitandao ya kijamii, Wakili Mwandamizi Alloyce Komba amesema wanakusudia kwenda mahakamani kudai fidia ya Sh5 bilioni.

Taarifa inayodaiwa kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na Burton Mwemba maarufu 'Mwijaku' inaelezwa kuwa imemkashfu na kumshushia heshima Masoud.

Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi Juni 15, 2024 Komba anayemwakilisha Masoud amesema maneno yaliyosambazwa na Mwijaku ni ya uongo na ya kashfa dhidi ya mteja wake.

Amesema maneno hayo pia yana nia ovu kwa kuwa hadi sasa hakuna ushahidi wowote uliowekwa hadharani.

"Maneno hayo ambayo yalichapishwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii yanaendelea kusambaa kwa watu, yamemuathiri mteja wetu, anaona aibu hata kupita mbele za watu," amesema.

Komba, wakili kutoka kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza amesema baada ya kuona ujumbe huo Juni 4, 2024 alishauriana na mteja wake na kukubaliana kumuandikia barua Mwijaku.

Amesema Juni 7, 2024 alimuandikia barua ikimtaka kuomba radhi kupitia mitandao yote aliyotumia kusambaza ujumbe huo, na kukubali kuwa amesema uongo akiwa na nia ovu.

"Kwa kuwa alikuwa amesafiri tulimtumia barua kwa njia ya mtandao, lakini Juni 10, nilimpelekea barua hadi leo hajafanya tuliyotarajia, sasa tumejipanga kwenda mahakamani kumfungulia kesi ya madai tukidai Sh5 bilioni kwa kumchafua," amesema.

"Madhara aliyoyapata mteja wangu ni makubwa kuliko maelezo atakayoyatoa, watu na taasisi mbalimbali wameendelea kumpigia simu na kampuni mbili anazofanya nazo kazi zimeshasitisha   mkataba naye," amesema.


Mambo anayolalamikia

Komba amedai chapisho hilo linaeleza Masod anafanya biashara haramu ambayo inasababisha vijana kuharibu maisha yao.

Kashfa nyingine anadai ni kuizodoa na kuwasema vibaya viongozi wa Serikali na kukubali kutumika na kuhongwa ili kuisema vibaya.

Hata hivyo, Mwijaku jana Juni 14, 2024 alimuomba radhi Masoud Kipanya kwa kile alichokiongea wakati akizungumza na wanahabari.

Mwijaku hakupatikana kuzungumzia madai hayo baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana.