Prime
Masoko yageuka uwanja wa kelele – 1
Muktasari:
- Si ajabu unapofika katika masoko kama ya Mchikichini ‘Karume’, Ilala, Kariakoo, Manzese au Tandika ukakaribishwa na sauti za kelele zinazotoka kwenye spika zilizorekodiwa matangazo ya bidhaa mbalimbali.
Dar es Salaam. Kelele nzito zinazotokana na spika za matangazo ya biashara, ikiwemo vipaza sauti, zimegeuka kuwa sauti rasmi katika masoko mengi ya jijini Dar es Salaam.
Ni kweli biashara ni matangazo. Lakini yanayoendelea katika baadhi ya masoko ya jijini humo si matangazo bali ni kelele zinazosababisha kero kwa wapitanjia na wateja.
Si ajabu unapofika katika masoko kama ya Mchikichini ‘Karume’, Ilala, Kariakoo, Manzese au Tandika ukakaribishwa na sauti za kelele zinazotoka kwenye spika zilizorekodiwa matangazo ya bidhaa mbalimbali.
Kutokana na kelele hizo, imekuwa vigumu kusikia kinachozungumzwa kati ya mteja na mfanyabiashara wanaouza bidhaa mbalimbali katika masoko hayo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu.
Wakati mwingine, kama mteja ana changamoto ya masikio, hulazimika kuziba masikio kwa kutumia mikono pindi anapofika katika eneo la soko husika.
Kwa mujibu wa wateja wa masoko hayo, kelele zimekuwa kero kubwa, hali inayosababisha kutosikilizana au kutokuelewana baina yao na wakati mwingine kukosekana kwa utulivu, jambo linalowaathiri pia kisaikolojia.
Mteja aliyekutwa Karume akinunua bidhaa mbalimbali, Martin Betram, anasema kero hiyo si Karume pekee bali hata kwenye masoko mengine yenye wafanyabiashara wadogo (wamachinga).
“Hizi spika zimekuwa kero, hakuna masikilizano. Huyu anatangaza viatu, yule mabegi, mara nguo. Inafika mahali mteja unatoka kwenye mwelekeo wako kutokana na mkanganyiko.
“Kuna wakati nalazimika kutumia nguvu kubwa kuzungumza na mfanyabiashara ili tuelewane kuhusu kile ninachokihitaji. Muda mwingine wanaokwenda sokoni wanaagizwa, lakini wanajikuta katika wakati mgumu kutoa mrejesho kwa simu kutokana na kelele,” anasema Betram.
Betram anasema kutokana na hali hiyo, kuna wakati analazimika kutoka nje ya soko ili kuzungumza kwa simu kwa utulivu na kutoa mrejesho kwa aliyemtuma kununua bidhaa.
Anasema kutokana na shughuli zake ana uzoefu wa jambo hilo kwa kuwa aliwahi kupata changamoto kupitia kijana wake aliyemtuma kununua bidhaa kwenye soko la Karume.
“Nilimpigia kijana zaidi ya mara sita nikafikiri ameibiwa simu baada ya kupiga kwa muda mrefu bila kupokelewa. Hata alipopokea aliniambia hakusikia kutokana na kelele za eneo hilo,” anasema Betram.
Anasema kijana wake huyo alipokea simu huku akilalamika kuwa kichwa na masikio vinamuuma kutokana na kukaa muda mrefu kwenye kelele, jambo lililomfanya arudi nyumbani akiwa amechoka na kufikia kulala.
Naye, Mariana Geofrey, anasema kelele za kwenye masoko zinaathiri. Mfano, akiingia Tandika kwa muda mrefu hadi kurudi nyumbani, ni lazima kichwa kimuume.
“Tunajua ni sehemu ya kuvutia wateja, lakini ni lazima waweke sauti kubwa hivyo? Sasa kumekuwa kama kuna mashindano ya kuweka spika kwenye biashara,” anasema Mariana.
Anasema kuna haja ya wafanyabiashara kupewa elimu maana kwa sasa imekuwa ni utaratibu wakati ni kero kwa wateja wanaofika kufanya manunuzi kwenye masoko yenye watu wengi.
“Ninachokijua, mteja anaifuata bidhaa kwa namna anavyoiona. Uzuri wenyewe sokoni kila kitu kinaonekana, hivyo sioni ulazima wa kupiga kelele,” anasema Mariana.
Kwa upande wake, Zainabu Masha anasema ni jambo la kawaida hivi sasa mtu ukienda Manzese ukakutana na kadhia ya kelele zinazotokana na spika za matangazo, huku hakuna hatua zinazochukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Sheria inasemaje
Kwa mujibu wa kifungu cha 106(5) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2025, hairuhusiwi mtu yeyote kupiga kelele au kusababisha kelele kuzidi kiwango kilichoainishwa au kitakachobainishwa kuhusiana na upigaji wa kelele.
Kulingana na vifungu namba 7 na 9 vya Kanuni ya Usimamizi wa Mazingira na Udhibiti wa Kelele na Mitetemo ya mwaka 2015, vimeweka utaratibu wa viwango vya sauti na mitetemo vinavyoruhusiwa kulingana na aina ya eneo (makazi, biashara, viwanda, shule na hospitali).
Vifungu hivyo vinafafanua kuwa hairuhusiwi mtu yeyote kutengeneza au kuruhusu kelele inayoweza kusumbua, kuumiza au kuhatarisha afya, usingizi au amani ya watu na mazingira, huku kiwango cha sauti kikiruhusiwa kuwa desibeli 55 wakati wa mchana katika maeneo ya makazi na biashara, na desibeli 45 wakati wa usiku.
Kwa mujibu wa ripoti ya tatu ya hali ya mazingira nchini iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) mwaka 2019, tatizo la uchafuzi wa kelele linaongezeka kwa kasi hasa katika maeneo ya mijini, na kwamba lina madhara ya kimwili na kisaikolojia.
Mwaka 2021, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Seleman Jafo, alisema kasi ya ukuaji wa uchumi inaenda sambamba na ongezeko la shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazoambatana na ongezeko la uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo, hali inayosababisha athari za kiafya.
Chanzo cha vispika
Mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika soko la Tandika, Juma Hamidu, anasema matumizi ya vispika yamekuja baada ya wauzaji kuona uvivu wa kupigia debe bidhaa na kujibu kila mteja anayeulizia bei.
Anasema si kwamba wanapiga kelele bali wanachofanya ni kutangaza biashara zao, ili kuvutia wateja kununua.
“Biashara ni matangazo. Ninachokifanya ni kutangaza kupitia spika hii. Hata hivyo, mimi si mwenye mali bali ni kibarua ninayetimiza majukumu yangu ili nipate fedha za kujikimu kimaisha,” anasema.
Wakati Hamidu akieleza hayo, Yassin Mussa anayefanya shughuli zake Karume anasema: “Biashara ni matangazo. Tunavyotumia spika zinasaidia kuwavuta wateja.”
“Wakati mwingine hatulazimiki kusema bei ya bidhaa bali mteja anaisikia moja kwa moja kwenye matangazo. Ingawa ni changamoto, lakini hatuna namna maana zama zimebadilika. Sasa hivi tupo miaka ya 2000, si miaka ya 90,” anasema.
Hata hivyo, wakati wafanyabiashara wakitoa sababu za kutumia spika hizo, baadhi yao wamepinga hatua hiyo wakisema si muhimu kuzitumia kwa sababu zinaathiri wateja.
Joseph Mshana anayefanya shughuli zake Karume anasema haoni umuhimu wa wafanyabiashara kutumia spika hizo kwa sababu zimekuwa kero kubwa.
“Wengine wanaona sawa, lakini mimi imefikia wakati hata sisikii vizuri hadi mteja aniongelee mara mbili. Hali si nzuri,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Mshana, kuna wakati spika hizo ziliondolewa katika soko la Karume baada ya malalamiko, lakini cha kushangaza zimerejea upya.
Kwa upande wake, Mvije Yassin anadai soko la Karume limekithiri kwa kelele za spika zinazoanzia asubuhi hadi jioni, akisema umeme ukikatika kunakuwa na ahueni kidogo kwa kuwa hubaki zinazotumia betri.
“Wateja wanalalamika wakija hapa. Hata ukimtajia bei anaweza kukuuliza zaidi ya mara tatu kwa sababu hakuna masikilizano. Kuna wateja wengine wakiingia humu sokoni wanaziba masikio yao kwa mikono,” anasema Yassin.
Yassin anaongeza: “Muda mwingine wateja wanatuuliza nyie mnaishi vipi humo sokoni kutokana na kelele hizi?”
Katibu wa wafanyabiashara wa soko la Tandika Usangi, Muhrami Simba, amesema matumizi ya spika hizo yamekuwa kero, ndiyo maana kwa nyakati tofauti amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi na wateja.
“Kuna kipindi niliwahi kushuhudia mjamzito akianguka kisa tu cha kelele zilizokuwapo. Hii ni kero inayohitaji ufumbuzi wa haraka,” amedai.
Simba anafafanua kuwa katika miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000 hakukuwa na matumizi ya vipaza sauti au spika, na biashara zilikuwa zikifanyika vizuri.
“Haya mambo ya dijitali yametuharibia, lakini si muhimu sana kutumia spika, sana ajiri wauzaji au wapiga debe waje wavutie wateja.Serikali itusaidie kuondoa hii kero,” anasema Simba.
Athari zake
Kwa mujibu wa baadhi ya madaktari waliozungumza na Mwananchi, kelele hizo zina athari mbalimbali katika mwili wa binadamu hasa kwa wanaotumia muda mrefu kuwepo katika masoko hayo.
Daktari bingwa wa masikio kutoka Hospitali ya Saifee, Khuzema Rangwala, anasema wateja na wauzaji wanaokuwapo sokoni kwa muda mrefu wapo katika hatari kubwa ya kiafya. Ingawa wengi wao hawatambui kinachoendelea, miili yao tayari inaanza kuathirika na matatizo mbalimbali.
Dk Rangwala anafafanua kuwa athari hizo hutegemea kiwango cha sauti pamoja na muda ambao mtu anakaa katika mazingira hayo.
“Mtu akikaa kwa saa sita hadi saba akisikia kelele kali mfululizo, madhara yake huwa makubwa na ya kudumu.
“Kwa hali hiyo, mtu anaweza kuanza kupata matatizo ya kiafya tuliyoyazungumzia awali, ikiwemo matatizo ya moyo, ubongo na afya ya akili kwa ujumla,” anasema mtaalamu huyo.
Naye, mtaalamu wa masikio (audiolojia), Dk Salum Seif, anasema sauti zinazotokana na shughuli za masoko ni tatizo la afya ya umma linalojitokeza kwa kasi, lakini mara nyingi hupuuzwa kwa sababu halionekani kama hatari ya moja kwa moja.
“Katika masoko ya wazi na kampeni za kibiashara, matumizi ya sauti kali kwa muda mrefu huzidi viwango salama vinavyopendekezwa kitaalamu, hali inayoongeza hatari ya athari za kiafya.”
“Athari za kelele hazijitokezi ghafla. Huanzia na usumbufu wa masikio na kupungua kwa umakini na, kwa muda mrefu, huweza kusababisha upungufu wa kudumu wa uwezo wa kusikia,” anaeleza Dk Seif.
“Kitaalamu, masikio hayazoei kelele kali. Kila mlio wa sauti kupita kiasi huongeza hatari ya uharibifu wa mfumo wa kusikia hata kama dalili hazionekani mapema.”
“Tatizo hili haliwahusu wateja pekee bali pia wafanyakazi na wafanyabiashara wanaofanya kazi karibu na vyanzo vya sauti kwa muda mrefu kila siku.”
“Mbali na athari kwa masikio, kelele huongeza msongo wa mawazo, huathiri mawasiliano ya kawaida na hupunguza ufanisi wa kazi,” anasema.
Naye, mtaalamu wa saikolojia, Yisambi Mbuwi, anasema kitendo cha mtu kukaa muda mwingi kwenye kelele kinaweza kumuathiri kisaikolojia kulingana na namna alivyoyapokea na kuyachukulia makelele hayo.
Anasema mtu anaweza kuathirika kisaikolojia kwa kupata ugonjwa wa wasiwasi au sonona kutokana na mvurugano wa kelele ambao hajauzoea katika maisha yake na hakutamani kukutana na hali kama hiyo.
“Lakini kama mtu amekwenda kwenye makelele, amekaa na haoni shida, basi ataendelea na maisha kama kawaida. Hawezi kuathirika kisaikolojia. Kinachomwathiri mtu ni mapokeo na tafsiri ya kitu kinachofika mbele yake,” anasema Mbuwi.
Itaendelea kesho