Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashujaa wa Vita ya Uganda wataja siri ya ushindi wa Tanzania

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo yaliyowafanya kushinda kirahisi ni hamasa ya Watanzania, mafunzo ya kutosha ndani ya jeshi, nidhamu ya wanajeshi na moyo wa utoaji waliokuwa nao wananchi wa Tanzania.

Dodoma. Mashujaa waliopigana Vita ya Uganda ya 1978/79 wametaja mambo manne yaliyobeba siri ya ushindi wa vita hiyo, huku makomandoo wakieleza jinsi walivyovuka Mto Kagera bila kuwepo daraja.

Miongoni mwa mambo yaliyowafanya kushinda kirahisi ni hamasa ya Watanzania, mafunzo ya kutosha ndani ya jeshi, nidhamu ya wanajeshi na moyo wa utoaji waliokuwa nao wananchi wa Tanzania.

Wapiganaji hao wametaja siri ya ushindi wao leo, Julai 25, 2026, katika kilele cha Siku ya Mashujaa kwenye sherehe zilizofanyika katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan ameongoza sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zilizofanyika leo Jumamosi Julai 25, 2026 kitaifa katika Uwanja wa Mashujaa, uliopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Brigedia Jenerali Mstaafu Wilfred Mwakalambile amesema baada ya tangazo la vita, bila kutegemewa na kwa hiari yao, wananchi walianza kuchangia gharama za mapambano hayo, jambo lililofanya ionekane vita nyepesi.

Mwakalambile, ambaye alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa kwanza kuvuka Mto Kagera, anakiri kuwa bila hayo huenda vita ingekuwa ngumu, licha ya ukweli kwamba walikuwa wamejiandaa.

“Mwalimu alipotangaza vita akiwa Songea, mimi na wenzangu tulifuatwa na ndege Zanzibar na moja kwa moja Jenerali Kiwelu aliniagiza nifanye kila namna makomandoo wavuke upande wa pili ili tujue nguvu ya adui, na niliwaongoza wenzangu tukavuka,” amesema Mwakalambile.

Amesema makomandoo walipovuka walifanya tathmini ya uwezo wa adui na ndipo mizinga ikaanza kupiga, huku kikosi cha wahandisi kikisonga mbele kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Kagera, ambalo wakati huo lilikuwa tayari limebomolewa.

“Niwaombe vijana kuwa wazalendo katika nchi yao, watunze amani hii na walioko jeshini wapewe mafunzo ya kutosha kwa ajili ya nchi yao,” amesema.

Kwa upande wake, mwanamke wa kwanza kwenda vitani, Brigedia Jenerali Mstaafu Mary Hiki, amesema licha ya mbinu walizokuwa nazo, hamasa ya Watanzania iliwapa morali kubwa.

Mary, ambaye hata baada ya vita alibaki Uganda akifanya kazi ya Ofisa Mawasiliano Ikulu, amesema sifa za ushindi zilibebwa na hamasa na michango ya wananchi, lakini nidhamu ya wapambanaji ilikuwa ya hali ya juu.

“Mimi nilikuwa mwanamke pekee kwenda uwanja wa mapambano. Hata hivyo, iliamuliwa nirudishwe kutokana na mazingira yalivyokuwa, lakini baada ya kuuteka mji wa Kampala, niliitwa tena Uganda, ndipo nikabaki huko kwa muda mrefu,” amesema Mary.

Kama ilivyo kwa wastaafu wenzake, amesisitiza umuhimu wa mafunzo ya kisasa kwa vikosi vya ulinzi ili kuendana na mahitaji ya wakati, huku akiwataka vijana kuitikia wito wa kuitumikia nchi yao kwa wivu na nidhamu ya hali ya juu.