Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masharti mapya ya vibali vya ujenzi haya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuweka sharti la upandaji wa miti katika vibali vya ujenzi wanavyovigawa.


Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuweka sharti la upandaji wa miti katika vibali vya ujenzi wanavyovigawa.

Dk Jafo aliyasema hayo jana, wakati wa shughuli ya upandaji miti iliyoandaliwa na Shirika la Taifa la Madini (Stamico) kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya shirika hilo.

“Naomba nitoe maelekezo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri, mnapogawa viwanja kwenda kujenga nyumba, mnapotoa building permit (vibali vya ujenzi) lazima alete ramani inayoonyesha miti kama miwili ama mitatu,” alisema.

Alisema iwapo kila kiwanja kitapandwa miti isiyopungua mitatu basi maeneo yote yatakuwa ni kijani.

Alisema mabadiliko ya tabianchi yameleta athari nyingi, ikiwemo katika maeneo mengine wanyama kufa kwa kukosa maji na malisho.

“Hili jambo linasababisha hata uchumi umeshuka, leo hii utaona hata kiwango cha chakula kinachozalishwa imekuwa ni changamoto kubwa,” alisema.

Alisema uzalishaji wa chakula umeshuka kwa sababu mvua zimepungua na kusababisha ukame ambao umepunguza uzalishaji.

Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko aliagiza Stamico kuhakikisha miti itakayopandwa inaonekana hata miaka 10 ijayo na kwamba hata kama itatokea mti umekufa basi upandwe mwingine.

“Tunapanda miti si kwa ajili ya kupiga picha, tunapanda miti kwa ajili ya utunzaji wa mazingira. Miti yote itakayopandwa ionekane hata baada ya miaka 10 ijayo,” alisema Dk Biteko.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwasse alisema kuwa katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo, watapanda miti 10,000 katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kati ya miti hiyo, 2,000 itapandwa mkoani Dodoma katika maeneo ambayo mkoa utayaainisha.

“Leo tutapanda miti 540 na tutahakikisha kuwa inatunzwa na kulindwa hadi itakapokua,” alisema Mwasse.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alitaka miti inayopandwa iwe na mfanano ili iweze kukidhi mahitaji mawili ya utunzaji wa mazingira pamoja na kuupendezesha mji.