Masauni, IGP Wambura waanza safari ya Hanang

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura wameanza safari usiku huu kuelekea mkoani Manyara kwa ajili kuungana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuongeza juhudi za uokoaji kwa waathirika maporomoko ya tope wilayani Hanang.
Katika msafara huo, Masauni ameambatana pia na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Maduhu Kazi na Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Haji.
Maporomoko hayo yaliyoua watu 47 na kujeruhi watu 85 yametokea leo Jumapili Desemba 3, 2023 Alfajiri katika maeneo ya Katesh na Gendabi wilayani Hanang mkoani humo.
Maporomoko hayo ya udongo yametokana na mvua zilizoanza kunyesha jana Jumamosi Desemba 2, 2023 saa tatu usiku kuendelea hadi leo asubuhi ilayani Hanang mkoani Manyara.
Maafa hayo yameharibu baadhi ya miundombinu, makazi, maduka na kusimamisha kwa muda shughuli za kijamii na usafiri.
Leo Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Dubai katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) alitoa salamu za pole huku akisema Serikali itaelekeza nguvu zote wilayani Hanang kwa ajili ya uokozi na kuzuia maafa zaidi.
"Nimeelekeze nguvu zote za Serikali zielekezwe katika uokozi ili kuzuia maafa mengi, imani yangu Serikali ikiwepo basi huduma zote zinazotakiwa zitapatikana niwape pole wananchi, nipo njiani kurudi kushirikiana nao," alisema Rais Samia.